Rubani Rubaga aliwazuia watoto wake kusomea urubani

Ndege ya Precision Air iliyopata ajali Ziwa Victoria Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 24 ikitolewa kwenye maji.

Muktasari:

  • Imezoeleka wazazi na walezi wengi hutamani kuwarithisha watoto wao kazi na taaluma zao, lakini kwa aliyekuwa rubani wa ndege ya Precision Air 5H-PWF, ATR 42-500, marehemu Buruhani Rubaga hali ilikuwa tofauti, kwani aliwazuia watoto wake kusomea taaluma ya urubani.

Bukoba/Mwanza. Imezoeleka wazazi na walezi wengi hutamani kuwarithisha watoto wao kazi na taaluma zao, lakini kwa aliyekuwa rubani wa ndege ya Precision Air 5H-PWF, ATR 42-500, marehemu Buruhani Rubaga hali ilikuwa tofauti, kwani aliwazuia watoto wake kusomea taaluma ya urubani.

Siri hiyo imefichuliwa na David Rubaga, mtoto wa kwanza wa rubani Rubaga wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika juzi nyumbani kwao kijiji cha Kagarama, Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.

Alisema enzi za uhai wake, baba yao alimkataza yeye na ndugu zake wengine kusomea na kufanya kazi ya urubani, badala yake aliwaasa kusoma na kufanya kazi nyingine zitakazowapa fursa ya kujiendeleza kitaaluma hadi kufikia ngazi nyingine huku wakiwa karibu na familia.

“Alisema mtu akiwa rubani atakuwa rubani maisha yake yote, tofauti na taaluma na kazi nyingine inayowezesha watu kapanda na kuwa tofauti,” alisema David, ambaye ni miongoni mwa watoto saba wa rubani Rubaga.

Alisema jambo lingine la msingi lililomfanya baba yao kuwataka kufanya kazi tofauti na urubani, ni kupata fursa ya kukaa karibu na familia kwa sababu urubani siyo tu humfanya rubani kusafiri mara kwa mara, bali pia haina siku za sikukuu wala mapumziko ya mwisho wa wiki.

“Alituambia kama yeye mwenyewe alivyo, rubani muda mwingi hakai na familia,” alisema David

Alisema marehemu aliwashauri kwanza kupata elimu, taaluma na kozi itakayowawezesha kufanya kitu tofauti ndipo wafikirie taaluma ya urubani kwa atakayependa kuongeza taaluma nyingine.


Kuheshimu taaluma hadi kifo

Wakati wengi wakijiuliza ilikuwaje rubani Rubaga kuwa kati ya watu 19 waliofariki ajali ya ndege ya Precision 5H-PWF, ATR 42-500 badala ya kujiokoa, David alisema alijua asingetoka ndani ya ndege bila abiria wote kuokolewa hata ikibidi kufa.

“Baada ya kupata taarifa za ajali inayohusisha ndege anayorusha baba, nilijua hatotoka ndani ya ndege hata ikibidi kufa hadi abiria wote waokolewe,” alisema David

Aliongeza: “Baba aliipenda, kuiheshimu na kuzingatia kanuni zote za kitaaluma, ikiwemo la rubani kuwa mtu wa mwisho kutoka ndani ya ndege, kujiokoa au kuokolewa wakati wa dharura hadi abiria wake wote watoke au kuokolewa. Zaidi ya yote aliwathamini abiria wake na hakuwa tayari kuwa sehemu ya kukwamisha kazi zake”.


Familia na jamii

Akizungumzia suala la familia na uhusiano kijamii, David alisema marehemu baba yake alichanganya vyote kwa kuipenda, kuijali na kuihudumia kwa nguvu na uwezo wake wote familia pamoja na jamii yake.

“Marehemu baba alisimama imara katika suala zima la familia; aliipenda familia yake na kila mtu aliyekuwa jirani; upendo wake huo ulidhihirika wakati wa mazishi yake kwa watu wengi kuhudhuria,” alisema

Alisema wakati wa uhai wake, marehemu Rubaga alitumia kila alichojaaliwa kuisaidia na kuiendeleza tu siyo familia yake, bali pia jamii inayomzunguka kwa kushiriki ujenzi wa msikiti na madrasa kijijini kwake kwa lengo la kuwakuza na kuwalea watoto katika imani na misingi mizuri kidini na kimaisha.

“Marehemu baba yangu alichukia uvivu, na kila wakati alitusisitizia suala la kuamka mapema na kufanya kazi kwa bidii, kuwa na upendo na mshikamano miongoni mwetu na jamii kwa ujumla,” alisema.

Alisema kifo cha rubani huyo siyo pigo na pengo kubwa kwa familia pekee, bali pia jamii yake, wakiwemo wachezaji wa timu za soka alizozisaidia kama njia ya kuwafanya vijana kutambua na kuendeleza vipawa na vipaji vyao kimchezo.

Abdallah Miraji, mmoja wa majirani wake, alisema familia na jamii ya wana Kanyigo imempoteza mtu mkweli, mwajibikaji, mpenda haki, mkweli na aliyependa maendeleo ya wote.