Rufaa yakataliwa, mganga wa jadi kuendelea na kifungo cha miaka 30 jela
Muktasari:
- Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya, imetupilia mbali rufaa ya Derick Sichone aliyekuwa akipinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka binti wa miaka 15 baada ya kujifanya mganga wa jadi.
Arusha. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya, imetupilia mbali rufaa ya Derick Sichone aliyekuwa akipinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka 15, hivyo kuacha adhabu hiyo iendelee kutekelezwa.
Katika hukumu iliyotolewa Julai 6, 2026 na Jaji Moses Pomo, mahakama imeeleza upande wa mashtaka ulithibitisha bila kuacha shaka vipengele vyote muhimu vya kosa la ubakaji, ikiwemo umri wa mwathirika, tendo la kupenya na utambulisho wa mshtakiwa.
Nakala ya hukumu hiyo imewekwa kwenye mfumo wa Mahakama.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Sichone aliwasili katika familia moja wilayani Songwe akijitambulisha kuwa mganga wa jadi aliyekwenda kumtibu baba wa mwathirika aliyedaiwa kuwa na matatizo ya akili.
Hata hivyo, badala ya kutoa huduma hiyo, aliondoka na binti huyo ambaye alipatikana baada ya siku tatu akiwa pamoja naye, hali iliyosababisha kukamatwa kwake na kufikishwa mahakamani.
Mahakama imeelezwa kuwa matukio hayo yalitokea kati ya Novemba 3 na 5, 2025 katika Kijiji cha Udinde, Wilaya ya Songwe. Sichone alishtakiwa kwa makosa matatu ya ubakaji kinyume na Kifungu cha 130(1)(2)(e) kikisomwa pamoja na Kifungu cha 131(1) cha Kanuni ya Adhabu.
Desemba 24, 2025, Mahakama ya Wilaya ya Songwe ilimpata na hatia na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela, hatua iliyomfanya kukata rufaa Mahakama Kuu.
Katika rufaa yake, Sichone alidai upande wa mashtaka haukuthibitisha kosa hilo kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.
Alisema ushahidi wa kitabibu haukuonyesha kuwepo kwa tendo la kupenya, mwathirika hakupiga kelele wala kutoa taarifa wakati wa tukio, huku akipinga pia kupokewa kwa maelezo yake ya onyo akidai hayakufuata utaratibu wa kisheria.
Aidha, alidai mashahidi muhimu hawakuitwa, utetezi wake haukuzingatiwa ipasavyo na adhabu ya kifungo cha miaka 30 ilikuwa kubwa kupita kiasi.
Pia, alipinga hoja kwamba maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) yaliyobainika kwa mwathirika yalihusishwa naye, akisema hakukuwa na ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali aliomba rufaa itupiliwe mbali akisema ushahidi wa mwathirika uliungwa mkono na ushahidi wa mazingira pamoja na matokeo ya uchunguzi wa kitabibu.
Akitoa uamuzi, Jaji Pomo alisema ushahidi wa mwathirika ulimtambua moja kwa moja Sichone kuwa ndiye aliyembaka, huku mazingira ya kukutwa naye baada ya kutoweka kwa siku tatu yakiimarisha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Jaji huyo alisema kwa kuwa mwathirika alikuwa na umri wa miaka 15, suala la ridhaa halikuwa na nafasi yoyote kwa mujibu wa sheria.
Mahakama pia ilikubaliana na hoja kwamba maelezo ya onyo ya mrufani yalipokewa kinyume cha utaratibu wa kisheria na kuyaondoa kwenye rekodi ya ushahidi.
Hata hivyo, Jaji Pomo alisema dosari hiyo haikuathiri msingi wa kesi kwa kuwa ushahidi mwingine uliowasilishwa ulikuwa wa kutosha kuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.
Kuhusu hoja ya maambukizi ya VVU, mahakama ilisema suala hilo halikuwa msingi wa kuamua kesi hiyo, kwani kilichokuwa mbele yake ni shtaka la ubakaji ambalo lilithibitishwa kupitia ushahidi wa mwathirika na ushahidi mwingine wa mazingira.
Kutokana na sababu hizo, Mahakama Kuu ilitupilia mbali rufaa hiyo na kuacha hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Songwe iendelee kutekelezwa.