Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baba hatiani kwa kumuua mwanawe mwenye ulemavu

Muktasari:

  • Mahakama ilieleza kuwa mtoto huyo hakuwa na uwezo wa kutembea, kujilisha wala kujiokoa, hivyo kitendo cha baba yake kumwacha peke yake katika mazingira hayo kilichangia moja kwa moja kifo chake.

Arusha. Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma, imemtia hatiani Oscar Daudi kwa kosa la kumuua bila kukusudia mwanawe, Davies Oscar, aliyekuwa na ulemavu wa kupooza ubongo, baada ya kubaini kuwa alimtelekeza katika shamba la miwa akijua hakuwa na uwezo wa kujisaidia.

Mahakama ilieleza kuwa mtoto huyo hakuwa na uwezo wa kutembea, kujilisha wala kujiokoa, hivyo kitendo cha baba yake kumwacha peke yake katika mazingira hayo kilichangia moja kwa moja kifo chake.

Hata hivyo, nakala ya hukumu iliyopandishwa katika mtandao wa Mahakama imeeleza tu Oscar ametiwa hatiani bila kutaja adhabu aliyopewa au miaka aliyofungwa,  lakini kwa mujibu wa kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, aliyotiwa nayo hatiani adhabu ya juu ikiwa ni kifungo cha maisha jela.

Ushahidi ulionyesha kuwa Davies alikuwa akiishi chini ya uangalizi wa bibi yake katika Kata ya Murubona, wilayani Kasulu mkoani Kigoma, baada ya mama yake kufariki dunia.

Kutokana na ulemavu wa mwili na akili aliokuwa nao tangu utotoni, mtoto huyo alikuwa akihitaji uangalizi wa karibu na alitumia kiti cha magurudumu.

Ilidaiwa mahakamani kuwa Januari 27, 2025, Oscar alimchukua mtoto huyo kutoka kwa bibi yake na kumpeleka nyumbani kwake katika eneo la Sofya, lakini hakumrudisha kama alivyokuwa akifanya awali.

Kwa mujibu wa ushahidi na maelezo yake mwenyewe, Januari 30, 2025, mshtakiwa alimpeleka mtoto huyo katika shamba la miwa lililopo eneo la Mwilamvya, wilayani Kasulu na kumtelekeza.

Februari Mosi, 2025, Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, aliyekuwa akifuatilia ustawi wa mtoto huyo kupitia mpango wa usaidizi wa kijamii wa HelpAge International, alifika nyumbani kwa familia hiyo kutaka kujua maendeleo yake.

Mahakamani ilielezwa kuwa mtoto hakukutwa nyumbani na familia ikaeleza kuwa alikuwa ameenda kucheza na watoto wenzake.

Februari 7, 2025, dereva wa HelpAge International alifika tena nyumbani hapo kwa ajili ya kutoa msaada wa kijamii, lakini hakumkuta mtoto huyo. Kutokana na kukuta kiti chake cha magurudumu kikiwa nyumbani, alishuku kuwa huenda alikuwa katika hatari na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.


Ushahidi ulivyokuwa

Mahakama ilielezwa kuwa uchunguzi uliofuata ulimfikisha Oscar mikononi mwa polisi, ambapo alikiri kuwa alimchukua mwanawe na baadaye akamtelekeza katika shamba la miwa.

Kutokana na maelezo hayo, aliwaongoza polisi hadi eneo alilodai kumwacha mtoto huyo, ambako walikuta mabaki ya mwili yaliyokuwa yameharibika kutokana na kuoza.

Ripoti ya daktari ilithibitisha kuwa mabaki hayo yalikuwa ya mtoto huyo, lakini kutokana na hali ya mwili haikuwezekana kubaini chanzo halisi cha kifo hicho.

Katika utetezi wake, Oscar alikana kuwa alikuwa na nia ya kumuua mwanawe. Alidai alikuwa akipitia msongo mkubwa wa mawazo uliotokana na hali ya afya ya mtoto, changamoto za malezi na mazingira magumu ya kifamilia.

Pia alidai kuwa siku ya tukio alikuwa amelewa na alishindwa kumfikisha mtoto kwa ndugu ambaye alikuwa amepanga kumpelekea. Alikiri kumtelekeza shambani, lakini akadai aliamini angeonekana na kuokolewa na watu wengine.


Mahakama ilivyoamua

Hukumu hiyo ilitolewa Juni 29, 2026 na Jaji Augustino Rwizile baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi wa mshtakiwa, ambaye awali alikuwa akikabiliwa na shitaka la mauaji.

Katika hukumu yake, Jaji Rwizile alisema ushahidi ulionyesha wazi kuwa Oscar ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na mtoto huyo akiwa hai na ndiye aliyewaongoza polisi hadi eneo mabaki ya mwili yalipopatikana.

Mahakama pia ilikubaliana na upande wa mashitaka kuwa ungamo la mshtakiwa lilitolewa kwa hiari na kwa kuzingatia taratibu za kisheria, hivyo lilikubalika kama ushahidi.

Jaji alisema ingawa hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha namna mtoto alivyokufa, mazingira yote ya tukio yalionesha kuwa kitendo cha kumtelekeza mtoto asiyeweza kujisaidia katika eneo la porini kilichangia moja kwa moja kifo chake.

Mahakama ilibaini pia kuwa baada ya kumwacha mtoto huyo shambani, mshtakiwa hakuchukua hatua yoyote kufuatilia hali yake wala kutoa taarifa kwa mtu yeyote kuhusu alikokuwa amempeleka.

Kwa mujibu wa Jaji Rwizile, mwenendo huo ulionyesha uzembe mkubwa na kutowajibika kwa mzazi aliyekuwa akifahamu hali ya kiafya ya mwanawe.

Hata hivyo, mahakama ilisema upande wa mashitaka haukuweza kuthibitisha pasipo shaka kuwa mshtakiwa alikuwa na nia ya kumuua mtoto wake, jambo ambalo ni sharti muhimu katika kuthibitisha kosa la mauaji.

Mahakama ilibaini kuwa hakukuwa na ushahidi wa matumizi ya silaha, majeraha kwenye mwili wa marehemu wala ushahidi unaoonyesha nguvu ilitumika dhidi yake.

Kutokana na mazingira hayo, Mahakama ilibadili shtaka la mauaji na kuwa la kuua bila kukusudia.

Jaji Rwizile alisema upande wa mashtaka ulifanikiwa kuthibitisha kuwa Oscar alisababisha kifo cha mwanawe kwa kumtelekeza mahali ambapo alijua hakuwa na uwezo wa kuishi au kupata msaada.

Kutokana na ushahidi huo, Mahakama Kuu ilimtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia chini ya Kifungu cha 195 kinachosomwa pamoja na Kifungu cha 198 cha Kanuni ya Adhabu.