Mwanamke, mtoto wauawa Pwani, miili yachomwa moto
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limesema hadi sasa utambulisho wa marehemu hao pamoja na waliohusika na mauaji hayo bado haujafahamika.
Kibaha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linafanya uchunguzi wa tukio la mauaji ya mwanamke mmoja na mtoto, yaliyotokea katika Kitongoji cha Nung’uli, Kijiji cha Kwang'andu katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, huku likiomba ushirikiano wa wananchi kufanikisha uchunguzi huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Juni 29, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, tukio hilo lilitokea Juni 2, 2026 saa 9:00 alasiri ambapo watu wawili walikutwa wameuawa na miili yao kuteketezwa kwa moto.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa marehemu ni mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 20 hadi 25 na mtoto mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka mitatu hadi sita, ambaye jinsia yake haikuweza kufahamika kutokana na mwili kuungua vibaya.
“Hadi sasa utambulisho wa marehemu hao pamoja na waliohusika na mauaji hayo bado haujafahamika,” imesema taarifa hiyo.
Polisi wamebainisha kuwa katika eneo la tukio walikuta tiketi mbili za basi la moja ya kampuni zinazofanya safari kutoka Dar es Salaam kwenda Miono kupitia Chalinze, zilizokatwa Mei 31, 2026 zikiwa na majina ya Adela na Modest, ambazo ni miongoni mwa vielelezo vinavyoendelea kufanyiwa uchunguzi.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Msoga, Wilaya ya Bagamoyo wakati uchunguzi ukiendelea.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa mtu yeyote anayewafahamu marehemu hao au mwenye taarifa zinazoweza kusaidia kuwatambua na kubaini waliohusika na tukio hilo kufika Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani au kufanya mawasiliano.