Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Katambi akaliwa kooni, LHRC kukimbilia kortini

Muktasari:

  • Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi kufuta agizo la kusitisha mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kikidai linakiuka Katiba na sheria, kikisisitiza kuwa kipo tayari kuchukua hatua za kisheria iwapo halitaondolewa.



Dar es Salaam. Agizo la Serikali kusitisha mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa limeendelea kuwa moto na sasa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinakusudia kulifikisha suala hilo mahakamani ikisema ni uvunjaji wa Katiba na kufifisha uhuru na shughuli za kisiasa nchini.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi alitoa agizo hilo kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillius Wambura Juni 26,2026 bungeni jijini Dodoma akieleza hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama na kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza.

Alisema Serikali imebaini uwepo wa matishio ya kiusalama, ikiwemo watu wanaodaiwa kukamatwa wakiwa na silaha, mafuta ya petroli na wakipanga vitendo vya uhalifu, hivyo vyombo vya ulinzi na usalama vimepewa maelekezo ya kuongeza ulinzi katika maeneo yenye viashiria vya hatari.

Tangu kutolewa kwa agizo hilo, kumekuwa na mjadala wa kulipinga kutoka makundi mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa kwamba linakwenda kinyume na Katiba.

Hata hivyo, Katambi mara mbili sasa akiwa Shinyanga na Dar es Salaam ametetea uamuzi wake akisema yuko sahihi huku akishangazwa na wanaodai hana mamlaka ya kutoa maelekezo hayo.

Leo Jumatatu, Juni 29, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amekutana na waandishi wa habari na kuwaeleza kwa mujibu wa Ibara ya 3 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, mfumo ambao msingi wake mkuu ni uhuru wa wananchi kushiriki katika shughuli za kisiasa bila hofu wala vikwazo visivyo halali kisheria.

Henga amesema haki za msingi za binadamu haziwezi kusimamishwa au kuwekewa zuio kwa matakwa ya mtu yeyote au mamlaka yoyote, isipokuwa tu katika mazingira maalumu ya hali ya hatari yaliyotangazwa rasmi na Rais kwa mujibu wa Ibara ya 32 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Amesema Kifungu cha 7 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, Sura ya 322 [Rekebu ya mwaka 2023], hakimpi Waziri mamlaka ya kusitisha mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, bali kinaweka wajibu wa kiutawala na usimamizi wa jumla wa masuala ya usalama bila kuondoa haki za msingi zinazolindwa kikatiba.

“Hivyo, hatua ya Waziri ya kusitisha mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa bila kuwepo kwa tangazo la hali ya hatari ni kinyume cha Katiba na nje ya mipaka ya mamlaka yake ya kisheria,” amesema

Amesisitiza kwa mtazamo wa LHRC katazo hilo si tu kwamba linakosa msingi wa Kikatiba na kisheria, bali linakiuka misingi ya demokrasia, utawala wa sheria na haki za msingi za binadamu.

“Tunatoa wito kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi kuliondoa mara moja tamko hilo kwani linakiuka Katiba ya nchi, sheria, mikataba ya kikanda na kimataifa na linahatarisha ulinzi wa haki za binadamu na utawala wa sheria nchini,” amesema Henga.

Wakati LHRC wakieleza msimamo wao, leo Juni 29, 2026 akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Katambi amesema anashangazwa na wanaodai hana mamlaka ya kuzuia mikutano ya hadhara, akisisitiza hatua aliyoieleza haihusiani na kutangazwa kwa hali ya hatari, ambayo Kikatiba ni mamlaka ya Rais.

Katambi amesema mamlaka ya Rais kuhusu kutangaza hali ya hatari ni tofauti na wajibu wa kila wizara katika kusimamia masuala yaliyo chini ya dhamana yake.

Amesema moja ya majukumu ya Wizara ya Mambo ya ndani ni kusimamia masuala ya kisera yanayohusiana na sheria

“Kuhusu wanaosema nimekiuka Katiba, Ibara ya tatu ya katiba ya Tanzania inatambua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia, kijamii na isiyofungamana na dini.

“Ibara ya tatu ya Katiba ibara ndogo ya pili inaeleza pamoja na masharti yaliyowekwa kutakuwa na utaratibu masharti yatakayotolewa jinsi sheria nyingine kuratibu masuala mbalimbali yawe ya kisiasa au kijamii,” amesema.

“Ibara ya nane ibara ndogo 1b inaeleza kuwa wajibu mkuu wa msingi wa Serikali ni kuhakikisha kuna ustawi wa watu,” amesema.

Pamoja na ufafanuzi alioutoa Katambi, Jumapili Juni 28, 2026 katika ibada maalumu ya kilele cha harambee iliyofanyika Usharika wa Amani wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kati, mjini Singida, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alisema wanaposema kupunguza mikusanyiko hawana ugomvi na vyama vya siasa.

Alisema hatua hiyo inalenga kukabiliana na mbinu ya watu wanaoingia na silaha ambazo zingine tayari wamezikamata na kukamata wengine wakiwa wanasajili.

“Pia tumekamata mawasiliano yao yakisema tufanye tukio hilo siku ya mikusanyiko mkubwa, watu wanaowaza hivyo wanaweza kufanya kwenye mkutano mmoja wa chama cha siasa ili ionekane ni Serikali, waliwahi kufanya mwaka fulani kwenye mkutano mmoja wa chama cha siasa,” amesema.