Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vuguvugu la maandamano, ulinzi usipime

Muktasari:

  • Hatua hiyo imekuja wakati kukiwa na vuguvugu la maandamano ya Julai 7 na siku chache baada ya Serikali kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Polisi wanasema ni utaratibu wa kawaida wa kuimarisha usalama na si maandalizi ya tukio maalumu.



Dar es Salaam. Kunani mijini? Ni swali linaloakisi uhalisia wa hali ilivyo katika majiji mbalimbali nchini, ambako askari wa Jeshi la Polisi wameenea kila kona.

Katika Jiji la Dar es Salaam, mathalan, eneo ambalo kwa kawaida ungekuta gari moja lenye askari wawili hadi watatu, kwa sasa kuna magari matatu yenye makumi ya askari kila moja.

Ukiacha maeneo yaliyozoeleka kuwepo askari, mambo yamekwenda mbali zaidi na sasa baadhi ya askari wamesimama katika maeneo mapya wakiwa na bunduki.

Magari ya maji ya washawasha na mengine maalumu ya polisi ambayo si kawaida kuonekana mitaani, kwa sasa yapo hadharani, yameegeshwa kando ya barabara yakiwa na askari ndani yake.

Hali ilivyo Dar es Salaam ndivyo ilivyoshuhudiwa katika baadhi ya mikoa kama Simiyu, huku mikoa mingine ikiwemo Mbeya, Kilimanjaro na Mwanza ikiendelea kuwa shwari.

Idadi ya askari na vifaa vya ulinzi vinavyoshuhudiwa katika maeneo hayo ni vilevile kama ilivyokuwa baada ya vurugu za Oktoba 29, 2025.

Hali hiyo ya kuimarishwa kwa ulinzi inashuhudiwa wakati ambao katika mitandao ya kijamii kumekuwapo vuguvugu la maandalizi ya maandamano Julai 7, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali katika mitandao hiyo, maandamano hayo yanalenga kushinikiza kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, aliyeko mahabusu kwa kesi ya uhaini, na wafungwa wengine wa kisiasa.

Ulinzi unaimarishwa siku nne tangu Serikali ilipotangaza marufuku ya kutolewa vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vyote vya siasa, ikisema inatumika kuhamasisha uvunjifu wa amani.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limesema ulinzi huo ni wa kawaida na sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya jeshi hilo.


Dar es Salaam

Maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, hali ya ulinzi na usalama imeimarishwa, huku askari wa Jeshi la Polisi wakionekana kufanya doria na kuweka ulinzi katika vituo muhimu na makutano ya barabara.

Mwananchi imetembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo na kushuhudia askari wamepangwa katika vikundi kwenye vituo vya mabasi yaendayo haraka na makutano ya barabara zinazoelekea katikati ya jiji, ikiwemo Magomeni, Buguruni, Tazara, Ubungo, Uhasibu, Fire na Mwenge.

Mbali na askari waliokuwa na silaha, wengine walionekana wakiwa wamevalia vifaa vya kutuliza ghasia. Pia, yalikuwepo magari ya maji ya washawasha na mengine ya doria yaliyokuwa yakizunguka huku na kule.


Ni tahadhari

Akizungumzia hali hiyo, mchambuzi wa masuala ya usalama wa jamii na kamishna wa zamani wa Jeshi la Polisi, Jamal Rwambow, amesema suala la ulinzi na usalama halina muda maalumu, bali ni jukumu la kila wakati.

“Suala la ulinzi ni la wakati wote. Watu hujifunza kutokana na makosa yaliyopita, na hatutamani kuona matukio kama hayo yakijirudia. Tahadhari ni bora kuliko kusubiri madhara yatokee,” amesema.

Rwambow amesema ni muhimu kuchukua hatua za tahadhari kabla ya matukio kutokea kuliko kusubiri kuyashughulikia baada ya kutokea.

“Kinachoendelea ni jambo la kawaida. Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuimarisha usalama, hivyo wananchi hawapaswi kulitazama kwa jicho la tofauti,” amesema.

Amesema ingawa baadhi ya wananchi wanaweza kuona hatua hizo kama usumbufu, jamii inapaswa kuzitambua kama sehemu ya kuhakikisha usalama wa watu na mali zao.

“Unapotakiwa kujieleza au kuulizwa maswali na askari usiwe na wasiwasi. Mara nyingi wanahitaji taarifa kwa ajili ya uhakiki ili kubaini wanaozingatia sheria na wanaokiuka sheria,” amesema.

Rwambow pia amesema Watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa mazingira ya kiusalama hubadilika na hivyo ni muhimu jamii kuwa tayari kuvumilia hatua zinazolenga kulinda amani.


Sio kwa ajili ya Sabasaba pekee

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema kuonekana kwa askari wakifanya doria na kuimarisha ulinzi ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kawaida ya jeshi hilo.

“Labda leo umeona kwa sababu unazunguka, lakini hali hii imekuwepo kwa muda mrefu. Ni wajibu wetu kuhakikisha wananchi na mali zao wanakuwa salama,” amesema.

Muliro amesema ulinzi huo hauhusiani na Maonesho ya Sabasaba pekee, bali unalenga kuhakikisha usalama wa wakazi wote wa Dar es Salaam.

“Ulinzi huu ni kwa wananchi wote, kuanzia Kibamba, Tegeta, Kunduchi, Bunju B, Kitunda, Mwanagati, Msongola, Chanika hadi Kigamboni. Lengo ni kuhakikisha maeneo yote ya Dar es Salaam yanakuwa salama, si eneo la Sabasaba pekee,” amesema.

Ameeleza mpango wa kuimarisha ulinzi ulianza tangu mwaka jana na tayari wananchi wengi wameuzoea kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.

Jeshi hilo, amesema, limekuwa likipokea mrejesho chanya kutoka kwa wananchi, ambao wengi wao wameonesha kufurahishwa na uwepo wa askari katika maeneo yao.

“Wananchi wengi wanafurahia uwepo wa askari na hata hutamani huduma hii ipatikane katika mitaa yote. Wapo wanaotamani hata maeneo ya makazi yao yawe na ulinzi wa aina hii,” amesema.

Muliro ameongeza kuwa hata watoto wameanza kujenga ukaribu na askari wa polisi, na baadhi yao huwasimamisha wazazi wao ili wapige picha na askari.

“Watoto hufurahia kuwaona askari wakiwa kazini. Kwao ni jambo la kuvutia na linaonesha taswira nzuri ya Jeshi la Polisi,” amesema.

Muliro amesema wananchi wanaozingatia sheria hawapaswi kuwa na hofu wanapoona ulinzi ukiimarishwa, kwa kuwa hatua hizo zinalenga kulinda usalama wa wote na si kuwabughudhi raia wema.


Hali ilivyo Simiyu

Mkoani Simiyu, Jeshi la Polisi limeongeza doria za usiku na ukaguzi wa maeneo mbalimbali ya biashara na malazi kuelekea sikukuu ya Sabasaba.

Katika siku za hivi karibuni, askari polisi wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika nyumba za kulala wageni ili kuhakikisha kila mgeni aliyepo ameandikishwa.

Mbali na ukaguzi huo, polisi pia wamekuwa wakisimamia utekelezaji wa muda wa kufunga baa na kumbi za starehe. Kila baa inapofika saa sita usiku hufunga huduma.

Doria za polisi zimeonekana kuongezeka katika mitaa mbalimbali, hasa nyakati za usiku, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuzuia vitendo vya uhalifu na kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao kwa amani na utulivu.

Mkazi wa Bariadi mkoani humo, Esther John, amesema hatua hizo zimeongeza hali ya kujiamini na usalama kwa wananchi wa eneo hilo.

“Kuwepo kwa askari katika maeneo ya makazi na biashara kumesaidia kupunguza vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza wakati wa usiku,” amesema.

Mmiliki wa nyumba ya kulala wageni mjini Maswa, Daud Pamba, amesema wanaendelea kuzingatia sheria na kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi za wageni na kufunga biashara zao kwa muda uliowekwa.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema lengo la kuimarisha doria na ukaguzi si kuwabughudhi wananchi, bali kuzuia viashiria vya uhalifu na kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa.


Mbeya, Kilimanjaro, Mwanza hali shwari

Mbali na maeneo yaliyoonekana kuimarishwa ulinzi, hali imeendelea kuwa ya kawaida katika baadhi ya mikoa nchini. Mkoani Mbeya, hakukuwa na viashiria vya ongezeko la askari wala vifaa maalumu vya ulinzi, huku shughuli za kila siku za wananchi zikiendelea kama ilivyozoeleka.

Hali kama hiyo pia imeshuhudiwa mkoani Kilimanjaro, ambako wananchi waliendelea na shughuli zao za kawaida za kiuchumi na kijamii bila kuwepo mabadiliko yanayoashiria kuimarishwa kwa ulinzi. Mitaa, masoko na maeneo ya biashara yaliendelea kuwa na shughuli kama ilivyo siku nyingine za kawaida.

Mkoani Mwanza pia hali iliendelea kuwa ya kawaida bila kuonekana ongezeko la askari kama ilivyoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo mengine. Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu.

“Tuimarishe amani na utulivu, na yeyote mwenye changamoto zake, mamlaka zipo tayari kumsikiliza... Hata hizo nchi zilizoendelea zina changamoto zake, hata ndani ya familia zetu hakuna changamoto?” amehoji.

Amesema matatizo hayaishi kwa sababu ni sehemu ya maisha, hivyo kinachohitajika ni uvumilivu, uzalendo na moyo wa kuijenga nchi.