Rushwa ya ngono kuwa kosa la uhujumu uchumi

Rushwa ya ngono kuwa kosa la uhujumu uchumi

Moshi. Imeelezwa kuwa watakaokamatwa kwa makosa ya rushwa ya ngono kuanzia sasa watafunguliwa shtaka la uhujumu uchumi.

Hayo yameelezwa na mwanasheria kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoa wa Kilimanjaro, Furahini Kibonga katika uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria.

Alisema kosa la kuomba rushwa ya ngono sasa litafunguliwa shitaka kama kosa la uhujumu uchumi kutokana na matokeo ya rushwa hiyo katika utekelezaji wa majukumu na uzalishaji.

“Rushwa ya ngono inasababisha kupata wasomi ambao hawana sifa, pili kuajiriwa watu ambao hawana sifa na wenye sifa wanaachwa, na pia wale wanaoajiriwa uzalishaji wao na utendaji kazi ni mdogo na hivyo kusababisha uzalishaji mdogo na uchumi wa taifa kuwa mdogo,” alisema Kibonga.

Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Mkoa wa Kilimanjaro, David Shillatu, alisema kama wadau wa sheria wanakubali kuwa rushwa ya ngono ipo kulingana na utafiti uliowahi kufanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hata hivyo alionyesha walakini kosa hilo kufanywa kuwa la kijinai.

‘‘Adhabu ya kushtakiwa kosa la rushwa ya ngono kama shauri la uhujumu uchumi ni adhabu kali sana...ni kosa la jinai ambalo halina hata dhamana,’’ alisema.