Rushwa ya ngono, umasikini vyakwaza wanawake katika muziki

Muktasari:

  • Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa kushirikiana na kampuni ya huduma ya muziki ya Mdundo wametoa mafunzo kwa wasanii wa muziki wanawake ya kukabiliana na changamoto za rushwa ya ngono na unyanyasaji katika tasnia hiyo.

Dar es Salaam. Rushwa ya ngono imetajwa kuwa miongoni mwa changamoto kwa wasanii wa muziki wa kike, huku pia wakikabiliwa na unyanyasaji na umasikini.

Hayo yamebainishwa katika semina ya uwezeshaji kwa wasanii wa kike nchini katika jitihada za kuwapa ujuzi utakaowawezesha kukabiliana na changamoto hizo, iliyoendeshwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa kushirikiana na kampuni ya huduma ya muziki ya Mdundo.

Semina hiyo ya uwezeshaji imekuja baada ya Mdundo kufanya utafiti wake Novemba na Desemba, 2022.

Akizungumzia ushirikiano huo jana Machi 22, Meneja Mawasiliano na Uendelevu wa SBL, Rispa Hatibu amesema wako tayari kuunga mkono sauti za kimaendeleo na kupigania ushirikishwaji kulingana na kauli mbiu ya ‘Society 2030: Spirit of Progress.’

“Kwa kutoa msaada wetu kwa wasanii wa kike wa Tanzania kunaimarisha zaidi msimamo wetu wa kusimamia tofauti za kijinsia,” amesema.

Ameongeza, "tulitaka kwanza kuelewa changamoto zinazowakabili wanawake katika muziki nchini Tanzania kwa kushirikiana na Mdundo kufanya utafiti ambapo maswali yalitumwa kwa wasanii wote waliopo kwenye jukwaa la Mdundo na jumla ya wasanii 106 waliwasilisha majibu.”

Kwa upande wake Meneja wa Leseni na Ushirikiano wa Mdundo, Prisna Nicholaus amesema, baada ya kubaini changamoto zilizopo, hatua iliyofuata ni kutengeneza jukwaa ambalo wanawake wa muziki Tanzania wanaweza kukutana, kuungana na kujifunza kutoka kwa wasanii wenzao na wadau wakuu wa tasnia hiyo.

“Watazungumza juu ya changamoto hizi na kutoa ushauri unaofaa, zana na mbinu ambazo wanaweza kutumia kushughulikia maswala yaliyopo na kuhakikisha kuwa wanasonga mbele zaidi ya kupata mrabaha kutoka kwa majukwaa kama Mdundo,” amesema.

Jumla ya wanajopo 10 wakiwemo wawakilishi kutoka Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota), vyombo vya habari, kampuni za usambazaji wa muziki na leseni pamoja na SBL walitoa mafunzo kwenye semina hiyo.