Ruto ashinda kesi ya kibali cha kampeni

Ruto ashinda kesi ya kibali cha kampeni

Muktasari:

Mahakama Kuu nchini Kenya imetoa amri ya kumruhusu Naibu Rais na mgombea urais kupitia Kenya Kwanza, William Ruto kufanya kampeni zake za mwisho kwenye uwanja wa Taifa wa Nyayo.

Kenya. Mahakama Kuu nchini Kenya imetoa amri ya kumruhusu Naibu Rais na mgombea urais kupitia Kenya Kwanza, William Ruto kufanya kampeni zake za mwisho kwenye uwanja wa Taifa wa Nyayo.

Awali Ruto alikosa kibali hicho kutoka kwenye mamlaka husika ya michezo nchini humo hivyo kuishtaki huku akiomba mahakama iridhie ombi lake hilo.

Kambi ya Ruto iliweka wazi kuwa waliwasilisha ombi hilo mapema lakini walishangaa walivyonyima kibali hicho, hali waliyoitafsiri ilikuwa njama za kuwazuia kufanya siasa.

Wiki iliyopita, mamlaka ya michezo Kenya ilimjulisha Ruto, kupitia barua, kwamba ukumbi huo ulikuwa umepangwa kufanyiwa shughuli nyingine katika siku hiyo ambayo Ruto aliuomba.

Barua hiyo ilitumwa kwa Katibu Mkuu wa chama cha UDA, Veronica Maina ambacho mgombea wake ni Ruto na pia ilitumwa kwa Waziri wa Michezo, Joe Okudo.

Barua hiyo ilichukuliwa kama jibu la kuwa kama mahasimu wao wa Azimio la Umoja chini ya mgombea wake Raila Odinga watafanyia hapo mkutano wao wa mwisho.

Ruto na Odinga wote wanawania kiti cha urais katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

“Tunasikitika kuwataarifu kwamba kutokana na kuwepo kwa matamasha ya amani yaliyopangwa kufanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Michezo cha Moi- Kasarani na Nyayo kati ya Agosti 5 hadi 7, mwaka huu Kituo hicho hakitaweza kutumika kwa matumizi yao,” ilisema barua hiyo.

Hata hivyo, baada ya chama cha UDA kukata rufaa mahakamani ilionyesha kuwa tayari imeupata ukumbi huo.

Kambi ya Ruto mara kwa mara imekuwa ikiishtumu ya Odinga inayosaidiwa na Rais Uhuru Kenyatta, kufanya rafu za kisiasa, ikiwemo kusambaza vipeperushi vya kumkashifu

Hata hivyo Rais Kenyatta amesema hana sababu ya kujibu matusi yanayoelekezwa kwake na kuwataka wagombea wasake kura bila matusi.