Ruwa'ichi:2025 ulikuwa mwaka mgumu, mzito
Muktasari:
- Askofu Mkuu Ruwa'ichi amewatakia heri ya mwaka mpya waumini akieleza namna binadamu walivyojaaliwa kuzungumza.
Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Juda Thadaeus Ruwa'ichi amesema 2025 ulikuwa mwaka mgumu na mzito.
Amesema mwaka huo ambao pia ulikuwa Jubilei Kuu, ulikuwa na changamoto hasa kwao kama Watanzania, akisisitiza ulikuwa mgumu, wa majonzi, masikitiko na vifo.
"Lakini hata katika magumu hayo, Mungu hajatuacha, Mungu hajatutupa, Mungu ndiye tegemeo na kimbilio letu," amesisitiza Askofu Ruwa'ichi leo Alhamisi Januari Mosi, 2026, katika Adhimisho la Misa Takatifu ya nadhiri za masista wa Shirika la Dada Wadogo wa Jimbo hilo, jijini Dar es Salaam.
Katika ibada hiyo, Askofu Mkuu Ruwa'ichi alianza kwa kuwatakia heri ya mwaka mpya waumini akieleza namna binadamu walivyojaaliwa kuzungumza.
"Sisi binadamu tumejaliwa kuzungumza, kuzungumza kwa mapana, unaweza kuzungumza bila kufungua kinywa na mara nyingi tunafanya hivyo kimya kimya. Unaweza kuzungumza kwa kutumia mwili kuonyesha kufurahi, kuonyesha hasira na kuonyesha ishara isiyopendezwa na jambo fulani," amesema askofu huyo.
Akisimulia kisa cha mzee mmoja ambaye aliugua sana, Askofu Ruwaichi amesema katika kuugua kwake, jamaa zake wakamchoka na wakamuona amekuwa kero, wakamtelekeza.
"Wewe umewahi kumtelekeza jamaa yako? kama ulishawahi, mtu anayetendewa hivyo huumia sana, uingia katika msongo wa mawazo na kukata tamaa," amesema Askofu Ruwa'ichi.
Akizungumzia ugumu wa mwaka 2025 na uzito wa mwaka huo, Askofu Ruwa'ichi amesema,"Tukiwa tunanza mwaka mpya, jana usiku tumehitimisha mwaka 2025 mwaka mzito, mzito kwa vipi? kwa sababu ulikuwa ni mwaka wa Jubilei, tumshukuru Mungu ametujaza neema nyingi kama watu binafsi, kama kanisa na kama taifa.
"Huo mwaka uliokuwa wa Jubilei Kuu ulikuwa ni mwaka wa changamoto hasa kwetu kama Watanzania, ulikuwa mwaka mgumu, ulikuwa mwaka wa majonzi, mwaka wa masikitiko na mwaka wa vifo," amesema.
Amesema hata katika magumu hayo, Mungu hajawaacha, hajawatupa na Mungu ndiye tegemeo na kimbilio lao.
"Katika safari ya mwaka wa Jubilei Kuu tumetenda mema, tumesali, tumehiji, tumefanya toba, lakini pia tunabaki wadhambi, kwa hiyo tunaalikwa tumuombe Mungu toba kwa yale tuliyovurunda kama watu binafsi, kama jumuiya, kama kanisa na kama taifa.
"Tunamuomba Mungu Baraka, waswahili husema shukuru na kuomba tena, kwa hiyo sisi tunaoshukuru kwa Baraka tulizopewa tunamuomba Mungu tena atubariki, atulinde, atubebe katika mikono yake inayoaminika kwa kipindi chote cha mwaka 2026," amesema Askofu Mkuu Ruwa'ichi.