Ruwasa: Maji ya Ziwa Rukwa ni machafu
Ziwa Rukwa
Songwe. Wakati wadau sekta ya maji wakishauri serikali kujenga mradi wa maji to Ziwa Rukwa, ili kuondokana na tatizo la maji mkoani Songwe, Wakala wa Maji Vijijini na Usafi wa Mazingira (Ruwasa), imesema ziwa hilo ni chafu.
Kwa muda mrefu, kumekuwa na tatizo la maji katika miji ya Viwawa, Mlowo na Tunduma mkoani Songwe, hata hivyo mhandisi wa Ruwasa, Charles Pambe, amesema licha yaw azo kuwa zuri, hofu ni kuwa Ziwa Rukwa halina matoleo ya maji.
“Wazo la kuyatumia maji ya Ziwa Rukwa kama suluhisho la kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji katika maeneo hayo ni zuri, lakini hofu ni kuwa zitahitajika fedha nyingi kulisafisha maana kikawaida ziwa hili linapokea tu maji bila kutoa, limejaa uchafu,” Pambe amefafanua.
Mhandisi Pambe amesema kwa sasa serikali inawekeza nguvu katika ujenzi wa mradi mkubwa wa maji kutokea mto Momba ambapo zitapatikana lita milioni 70 kwa siku huku mahitaji halisi ya sasa ni lita milioni 49 kwa siku.
Ushauri wa wadau wa kutumia maji ya Ziwa Rukwa, umetolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya wadau waliotoa maoni yao kuhusu uhaba wa maji wa muda mrefu katika miji hiyo, unaosababishwa na kukua kwa kasi kwa miji hiyo.
Kwa mfano, Faines Msongole, mkazi wa Tunduma ameona chanzo cha Ziwa Rukwa ni bora Zaidi maana kinaaminika kuliko kutoa maji kwenye vyanzo vingine ambavyo kwa maelezo yake, vimekuwa vikiathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi.
“Hata hizi taarifa tunazopewa za kutoa maji mto Kiwira uliopo wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya, kimsingi chanzo hiki hakiiaminiki kwa kuwa maji yake yanazidi kukakuka kutokana na mabaliko ya tabia nchi,” amefafanua.
Naye Herman Sadick mkazi wa Mlowo amesema uhaba wa maji uliopo katika miji yao unatokana na vyanzo vingi vya maji kuwa na maji kidogo hivyo unahitajika mradi mmoja mkubwa wa uhakika na hivyo kushauri maji ya kutosha yatoke kwenye Ziwa Rukwa.