Ruzuku ya Sh11 bilioni yatolewa kwa vyama vya siasa

Muktasari:

 Katika mwaka 2022/2023 ruzuku iliyotolewa kwa vyama vya siasa ilikuwa Sh17.5 bilioni.

Dodoma. Serikali imetoa ruzuku ya Sh11.7 bilioni kwa vyama vya siasa vyenye sifa ya kupata ruzuku.

Pia imeiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kupewa Sh77.91 bilioni kwa ajili ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ikiwamo kupewa vitendeakazi vipya.

Hayo yamesemwa bungeni leo Jumatano Aprili 3, 2024 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipowasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka  2024/2025.

“Hatua hii imesaidia kuendeleza na kuimarisha uendeshaji wa shughuli za vyama vya siasa na demokrasia nchini,” amesema.

Ruzuku ya Sh11.7 bilioni iliyotolewa kwa vyama kwa wakati huu ni ndogo ikilingansihwa na ya Sh17.5 bilioni iliyotolewa kwa vyama vya siasa katika mwaka 2022/2023.

Vyama vilivyonufaika na ruzuku ya Sh17.5 bilioni ni NCCR-Mageuzi, CCM, Chadema, DP, CUF na ACT-Wazalendo.

Majaliwa kwenye hotuba yake bungeni leo hakuvitaja vyama vya siasa vilivyonufaika na ruzuku ya Sh11.7 bilioni.

Mbali ya hayo, amesema Serikali itaendelea na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ikiwa ni pamoja na kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kuendelea na utoaji wa elimu ya mpigakura.

Amesema maandalizi hayo pia yanahusisha kuandaa nyaraka za uchaguzi mkuu na kujenga mifumo ya kielektroniki kwa ajili ya uchaguzi na utoaji wa huduma za Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.