Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Saba washikiliwa polisi kwa tuhuma za mauaji ya 'Mungu' Mbeya

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga.

Muktasari:

  • Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda tukio hilo Aprili 21 kwa kuvamia na kumshambulia marehemu huyo na kusababisha kifo chake, na sasa upelelezi unaendelea ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu saba kwa tuhuma za mauaji ya Mungu Mamboleo, mkazi wa Ihanga Mkanyageni, Tarafa ya Rujewa, wilayani Mbarali mkoani humo, kwa kumtuhumu kuiba ng’ombe.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Aprili 21 majira ya saa 9 usiku, ambapo kundi la watu hao likiongozwa na Samweli Yohana ‘Fagu’ walivamia kambi ya ng’ombe na kumkamata na kumshambulia Mungu kwa silaha za jadi hadi kufariki.

Taarifa ya Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo, SACP Benjamin Kuzaga, iliyotolewa kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa kufuatia tukio hilo, askari wa kuchunguza matukio ya mauaji walianza msako na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

Imeeleza kuwa waliokamatwa kwa mauaji hayo ni Advero Seng’unda, Sameli Yohana ‘Fagu’, Shija Gidingi, Patrick Yonga, Gasper Mashaka, Neno Paulo na Msifuni Ezekiel, wote wakazi wa Ihanga Mkanyageni wilayani Mbarali.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni kujichukulia sheria mkononi wakimtuhumu marehemu kuhusika na wizi wa ng’ombe. Upelelezi unakamilishwa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa,” amesema Kuzaga.

Kamanda huyo ametoa wito kwa baadhi ya wananchi kutoendelea kujichukulia sheria mkononi wanapowakamata watuhumiwa kwa tuhuma zozote, badala yake wawafikishe kituo cha polisi kwa hatua zaidi.

Amekemea pia vitendo vya kujihusisha na matumizi au biashara ya madawa ya kulevya kutokana na athari zake kiafya na madhara ya kukutwa nayo, akieleza kuwa jeshi hilo linaendelea kulinda usalama wa raia na mali zao.

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa baadhi ya wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, badala yake watuhumiwa wafikishwe polisi kwa hatua za kisheria. Pia tunawataka wananchi kutojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya,” amesema kamanda huyo.