Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yaliyojiri usiku wa mauaji ya mama lishe Moshi, kichanga chake kikilia

Mwili wa Restituta Moshiro (40) mkazi wa Mtaa wa Mnazi, Kata ya Ng’ambo mkoani Kilimanjaro ukiingizwa kwenye gari la polisi. Picha na Yese Tunuka

Muktasari:

  • Tukio hilo lilitokea majira ya saa nne usiku wa kuamkia Aprili 17, 2026 wakati marehemu aliyekuwa akijishughulisha na biashara ya kuuza chakula kandokando ya barabara kuu ya Moshi–Arusha, eneo la Shaa Tours, akirejea nyumbani kwake.

Moshi. Sauti za ndege zisizo za kawaida, mvua kubwa iliyonyesha usiku kucha na kilio cha mtoto mchanga wa miezi saba, ndizo ishara zilizotangulia tukio la kushtua la mauaji ya kinyama ya mama lishe, Restituta Moshiro (40), mkazi wa Kata ya Ng’ambo mkoani Kilimanjaro.

Mwili wa mwanamke huyo ulipatikana umetupwa shambani, ukiwa na majeraha yanayodhaniwa aliburuzwa na kukabwa kabla ya kuuawa, hali iliyoacha maswali mengi kwa jamii.

Tukio hilo lilitokea saa nne usiku wa kuamkia Aprili 17, 2026 wakati marehemu aliyekuwa akijishughulisha na biashara ya kuuza chakula kandokando ya barabara kuu ya Moshi–Arusha, eneo la Shaa Tours, akirejea nyumbani kwake.

Mwili wa marehemu, anayefahamika zaidi kama ‘Mama Baraka’, ulikutwa ukiwa na damu puani, huku nguo yake ya ndani ikiwa imevuliwa na kutupwa pembeni ya mwili wake.

Eneo katika shamba ulipokutwa Mwili wa Restituta Moshiro (40) mkazi wa Mtaa wa Mnazi, Kata ya Ng’ambo. Picha na Yese Tunuka

Aidha, vitu alivyokuwa amebeba kwa ajili ya mtoto wake wa miezi saba, yakiwamo maziwa, unga wa lishe, simu, vocha, fedha za mauzo na mwamvuli wa kujikinga na mvua, vilikutwa vimetapakaa umbali mfupi kutoka ulipolala mwili wake.

Wakati familia ikijiandaa na mazishi, simulizi za usiku wa tukio hilo zinaendelea kuumiza mioyo ya wengi, hasa baada ya kubainika kuwa marehemu ameacha mtoto mchanga wa miezi saba ambaye alilia kwa saa tatu mfululizo usiku wa tukio.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Aprili 19, 2026, Dorcas Maro, aliyekuwa akimlea mtoto huyo usiku wa tukio, amesema kilio hicho hakikuwa cha kawaida na kilimtia hofu kubwa.

“Mtoto alilia sana kuanzia saa nane, saa tisa hadi saa 11 alfajiri. Haikuwa kilio cha kawaida, alikuwa akilia hadi anatetemesha ulimi. Nilijitahidi kumtuliza, nikampikia uji lakini bado alikuwa na mahangaiko makubwa,” amesema Dorcas.

Dorcas, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mwenge (MWECAU), amesema wakati mtoto huyo akilia, nje kulikuwa na sauti za ndege zisizo za kawaida huku mvua kubwa ikinyesha.

Amesema siku ya tukio ilikuwa Ijumaa ambapo alimchukua mtoto huyo aitwaye Grace kutoka kazini kwa mama yake saa 12 jioni na kuelekea naye nyumbani, akimsubiri arejee kama ilivyo desturi.

Amesema hali ilianza kubadilika kuanzia saa nne usiku baada ya mama huyo kutofika nyumbani, jambo lililomfanya mtoto kuanza kuhangaika kutokana na kukosa maziwa ya kunyonya.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Moshi (OCD),Azizi Kalokola akizungumza na wananchi eneo lilipotokea tukio la mauji kata ya Ng'ambo. Picha na Yese Tunuka

“Ilipofika saa nane usiku, mtoto aliamka na kuanza kulia mfululizo hadi saa 11 alfajiri. Wakati huo mvua ilikuwa kubwa na kulikuwa na sauti za ndege zisizo za kawaida,” amesema.

 “Sikuwaza jambo baya, nilidhani labda amekwama kutokana na mvua na ameenda kwa rafiki yake aitwaye Mama Diana. Nilijaribu tu kumtuliza mtoto asipate homa,” amesema.

Dorcas amesema taarifa za kifo hicho zilimfikia saa 12:30 asubuhi kupitia mwenye nyumba wao aliyepokea simu kutoka jirani wa eneo la tukio.

“Mwenye nyumba aliniambia kuna mwili wa mwanamke umeonekana katikati ya mahindi na unafanana na marehemu. Nilipofika kushuhudia, ni kweli alikuwa yeye… walimfanyia unyama mkubwa,” amesema huku akilia.

Amesema marehemu alikuwa mtu mwenye upendo na aliyekuwa akimsaidia kufikia malengo yake ya maisha.

“Aliniambia nimwangalie mtoto kwa ukaribu na nimtunze. Hayo ndiyo yalikuwa maneno yake ya mwisho,” amesema Dorcas.

Kwa upande wake, mtoto wa marehemu, Baraka Maro (18), amesema kifo cha mama yake kimemuachia maumivu makubwa pamoja na jukumu la kumlea mdogo wake.

Baraka, anayefanya kazi ya duka na uwakala wa fedha jijini Dar es Salaam, amesema alipokea taarifa hizo akiwa safarini kikazi.

“Nimewasili leo asubuhi nikitokea Dar es Salaam, safari nzima nimekuwa nikilia maana siamini kilichotokea,” amesema.

Amesema mazungumzo yake ya mwisho na mama yake yalifanyika saa 12 jioni siku ya tukio, ambapo alimpa nasaha za maisha.

“Aliniambia ‘mwanangu pambana, maisha ni magumu’. Sikutegemea ndiyo ingekuwa mara ya mwisho kusikia sauti yake,” amesema.

Baraka ameomba vyombo vya dola kuwabaini wahusika wa tukio hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Inaniumiza sana, mama yangu hakuwa na ugomvi na mtu yeyote. Ameniachia mzigo mkubwa wa kumlea mdogo wangu,” amesema.

Naye Heavenlight Maro amesema marehemu alikuwa mlezi wa familia aliyewalea watoto wa mke mkubwa kwa upendo mkubwa.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Moshi (OCD), Azizi Kalokola akizungumza na wananchi eneo lilipotokea tukio la mauji kata ya Ng'ambo. Picha na Yese Tunuka

“Alitulea tangu tukiwa wadogo na hata baada ya kutengana na baba, aliendelea kuwa karibu nasi. Alikuwa na upendo wa kipekee,” amesema.

Amesema waliendelea kuwa na mawasiliano ya karibu hadi siku chache kabla ya tukio.

“Hakuwa na ugomvi na mtu yeyote. Ni vigumu kuelewa kilichosababisha unyama huu,” amesema.

Kwa sasa mtoto mchanga wa marehemu anaendelea kulelewa na shangazi yake.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumapili, Aprili 19, 2026, kaka wa marehemu, Christian Moshiro, amesema familia inatarajia kupanga ratiba ya mazishi.

Amesema mwili wa marehemu utasafirishwa kwenda kijiji cha Shimbi Mashami, wilayani Rombo kwa mazishi.

Awali akizungumza katika eneo la tukio, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Moshi, Azizi Kalokola, alisema Jeshi la Polisi tayari limeanza upelelezi wa kina kubaini mazingira yaliyosababisha kifo hicho cha kutatanisha.