Prime
Mambo matano ya kuipata Katiba mpya kabla ya 2030
Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi mchakato wa Katiba mpya kuanza ndani ya siku 100 za uongozi wake, na Makamu wake, Dk Emmanuel Nchimbi, amewataka Watanzania kupambana ili kupata Katiba mpya. Swali ni nani anayezuia kuipata?
Ninaamini kuwa kama kweli tunayoyasema yanatoka moyoni na kuna utashi wa kisiasa wa kuhakikisha Katiba mpya inapatikana kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2029 na Uchaguzi Mkuu wa 2030, kuna mambo matano yanapaswa kuanza sasa.
Jambo la kwanza ni lazima tuingie kwenye maridhiano leo na si kesho kwa sababu, bila maridhiano ya kitaifa na katika hali ya mgawanyiko, chuki na kukosekana kwa mshikamano wa kitaifa, ni wazi mchakato wa kupata Katiba mpya ni ndoto.
Ni kupitia maridhiano hayo tutakapokubaliana tunaanzia wapi. Tunarudi kwenye mchakato huo kwa kukusanya upya maoni ya wananchi, au tunaanzia kwenye Rasimu ya Jaji Joseph Warioba, au tunaanzia pale kwenye Katiba inayopendekezwa?
Hatari ya kuanzia kwenye Katiba inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014 ni moja tu. Kuna hatari ya kupigiwa kura ya hapana kwa sababu kuna maoni ya wananchi yaliyofutwa na Bunge hilo.
Miongoni mwa mambo yaliyonyofolewa ni lile lililotaka anayechaguliwa kuwa Rais awe amepata kura za wapiga kura zaidi ya nusu (absolute majority), badala ya utaratibu wa sasa wa mshindi kupata wingi wa kura (simple majority).
Mambo mengine ni kupunguzwa kwa madaraka makubwa ya Rais, ukomo wa ubunge kuwa vipindi vitatu vya miaka mitano mitano, na wananchi kuwa na uwezo wa kumwondoa mbunge wao kabla ya kumaliza kipindi chake cha miaka mitano.
Lilikuwapo pia suala la kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano (siyo hii ya sasa iliyobadili tu jina), uwepo wa mgombea huru katika nafasi ya udiwani, ubunge na urais, pamoja na kiwango cha chini cha elimu.
Kuna mambo karibu 20 yaliyopendekezwa na wananchi lakini yakanyofolewa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutokana na maslahi ya kisiasa, likiwamo suala la muundo wa Muungano ambalo lingetibu kelele tunazozisikia sasa.
Katika maridhiano ninayoyasema ni lazima kuwepo ukweli, na tusiende kuridhiana huku tumeficha mapanga. Hapana. Kuwepo na dhamira ya kweli ya kutaka maridhiano, na hatuhitaji maridhiano ambayo ni kiini macho.
Jambo la pili, tunapaswa kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, toleo la mwaka 2012, ili iendane na mazingira ya sasa ya uandikaji wa Katiba mpya, ikiwamo kubadili mfumo wa kupatikana kwa wajumbe wa Bunge la Katiba.
Sote tunafahamu Bunge Maalumu la Katiba la mwaka 2014 lilitawaliwa na wingi wa wajumbe waliotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), na tukiitisha Bunge Maalumu leo kwa namna lilivyo, tunarudi kule kule kwa mwaka 2014.
Ukisoma Kifungu cha 37(1) cha sheria hiyo, kinasema baada ya matokeo ya kura ya maoni kutangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Rais atatoa amri ya kuivunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Warioba.
Ukienda mbele zaidi ukasoma kifungu kidogo cha (3) cha sheria hiyo, kinasema: “Baada ya kuzinduliwa kwa Katiba mpya, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ndiyo itakuwa imemaliza matumizi yake na itapoteza nguvu ya kisheria.”
Ndiyo maana nasema ni muhimu kuifanyia marekebisho sheria hiyo kulingana na mazingira ya sasa ili, kama katika maridhiano niliyoyasema itakubaliwa tukusanye upya maoni au tuanzie na Rasimu ya Jaji Warioba, basi sheria iruhusu hilo.
Jambo la tatu, ninaloliona linapaswa kufanywa baada ya kuifanyia marekebisho Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ni kuunda Kamati ya Wataalamu wabobezi wa Katiba watakaopitia Rasimu ya Jaji Warioba na Katiba inayopendekezwa.
Jukumu lao kubwa liwe kuoanisha maudhui ya nyaraka hizo mbili ili kuja na Rasimu ya Katiba mpya iliyobeba maoni ya wananchi. Kamati hii isiteuliwe na Rais, bali wataalamu hao waombe kazi na wapimwe hadharani kwa sifa zao.
Baada ya kamati ya wataalamu wabobezi kukamilisha kazi hiyo, ndipo twende kwenye jambo la nne la kuunda Bunge Maalumu la Katiba, ambalo wajumbe wake wataainishwa katika marekebisho yatakayofanywa kwenye sheria niliyoitaja.
Sheria inapaswa kuja na muundo tofauti kabisa wa Bunge Maalumu la Katiba, tofauti na lile la mwaka 2014 ambalo lilitafuna zaidi ya Sh27 bilioni za walipa kodi na kuja na Katiba inayopendekezwa ambayo haina uungwaji mkono wa wananchi.
Mabadiliko ya sheria hiyo yaje na vifungu vitakavyoainisha majukumu ya Bunge Maalumu la Katiba na kuliwekea mipaka lisinyofoe maoni ya wananchi, bali liyaboreshe tu maoni hayo pasipo kubadili mambo ya msingi waliyopendekeza.
Ukisoma Kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kinasema kuvunjwa na kukoma kwa mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba hakutachukuliwa kuwa kunaondoa mamlaka ya Rais kuitisha tena Bunge hilo kwa lengo la kuboresha masharti yaliyomo katika Katiba inayopendekezwa.
Ni kwa msingi huo, baada ya kamati ya wataalamu wa uandishi wa Katiba kukamilisha kazi na kuja na Rasimu ya Tatu ya Katiba iliyobeba maslahi ya wananchi na si maslahi ya wanasiasa, basi Rais aitishe tena Bunge hilo kufanya kazi hiyo.
Jambo la tano, ambalo naona ni muhimu lifanyike baada ya Bunge Maalumu la Katiba kupitisha Katiba inayopendekezwa, ni kufumua muundo wa INEC, ambayo ndiyo itakayosimamia kura ya maoni.
Sasa, kwa yale tuliyoyapitia katika chaguzi za Serikali za Mitaa za mwaka 2019 na 2024, na Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2020 na 2025, kwangu mimi, kwa namna muundo wa INEC ulivyo, hatutatoboa kwenye kura ya maoni.
Kunahitajika INEC iliyo huru, inayokubalika na inayoaminika, lakini kuitumia tume hii hii inayonyooshewa kidole kusimamia kura ya maoni ni kukaribisha mgogoro, labda tu kama kutakuwa na maridhiano ya kitaifa kabla ya kura ya maoni.
Ninatamani mambo hayo matano tuyaone kuanzia sasa katika kauli na matendo ya viongozi wetu wa kisiasa, badala ya kuongea maneno matupu tu kuwa hata Rais anaitaka Katiba mpya, lakini huku chini (kwenye ground) hakuna kinachoendelea.
Tukienda kwa kudema dema huku, nawaambia tutafika mwaka 2028 kabla hatujapiga hatua yoyote ya kuipata Katiba mpya, kama Tume ya Jaji Mohamed Othman Chande iliyochunguza ghasia za Oktoba 29, 2025, ilivyopendekeza.
Katika muhtasari wa ripoti ya tume iliyowasilishwa kwa Rais, Jaji Chande alisema moja ya chimbuko, au kiini, cha vurugu zile za Oktoba 29 ni madai ya Katiba mpya. Sasa kama tume hii imetuonesha tatizo lililopo, kwa nini tusilitatue sasa?
Suala la uwepo wa haja ya kuandikwa kwa Katiba mpya halijaanza leo wala jana. Ni tangu tulipoingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ndiyo maana nimemwelewa Dk Nchimbi akitaka Watanzania wakomae kupigania Katiba mpya.
Lakini niwasihi wahafidhina (conservatives) ndani ya CCM waache kuwajaza hofu viongozi wetu na wanachama kuwa ujio wa Katiba mpya ndiyo kaburi la CCM, na watambue kuwa Katiba si mali ya chama cha siasa, bali ni mali ya Watanzania.
Ni kwa msingi huo, Katiba haiwezi kutolewa kama fadhila au zawadi na mtawala au chama chochote cha siasa, kwani hilo ni takwa la Watanzania, na naamini kuna wana-CCM makini kama Samia na Dk Nchimbi wanaolitambua hilo.
Tuandike Katiba mpya sasa, tusisubiri umma ukanyanyuka na kuidai kwa nguvu.
Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900.