Sababu kifo cha Zelothe yatajwa

Baadhi ya waombolezaji katika msiba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Zelothe Stephen ambao wameongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdurahman Kinana. Picha na Mussa Juma

Arumeru. Makamu Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Taifa, Abdurahman Kinana leo Jumatatu Oktoba 30, 2023 ameongoza waombolezaji kumuaga Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Zelothe Stephen Zelothe ambaye alifariki dunia Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam Oktoba 26 mwaka huu akiwa anasumbuliwa saratani ya tumbo.

Zelothe alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa Arusha, kuanzia mwaka 2019 hadi alipofariki, pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa Rukwa na Kamanda wa Polisi mikoa ya Mtwara, Dodoma, Mbeya na Mwanza.

Mtoto wa Zelothe, William Zelothe akisoma wasifu wa baba yake, amesema alizaliwa Novemba 30, 1950 Kijiji cha IIkiranyi, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha na ameacha watoto Tisa

Amesema Zelothe alianza kuugua Julai mwaka huu na kupelekwa nchini India kwa matibabu na ikagundulika kuwa alikuwa na saratani ya tumbo.

"Alitibiwa India na kurudi nyumbani Tanzania na kupangiwa tarehe ya kurudi Septemba kwa wiki tatu na baadaye alirudi mwezi Octoba kuendelea na matibabu hadi mauti ilipomfika," amesema.

Amesema kwamba familia inamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alimsaidia Zelothe kuanzia matibabu nje ya nchi hadi kutoa ndege kumrejesha Arusha.

"Pia tunamshukuru sana Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Makamu Mwenyekiti wa CCM Mzee wetu Kinana Katibu Mkuu Daniel Chongolo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillius Wambura, Mkuu wa Mkoa Arusha, Waziri Jerry Silaa na Christopher ole Sendeka wa msaada mkubwa waliotupa wakati wote kumuuguza hadi leo," amesema.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosis ya kaskazini kati, Dk Solomon Masangwa amemueleza Zelothe kama kiongozi aliyependa watu na alikuwa Karibu sana na Kanisa.

"Sina mashaka na maisha ya Zelothe kuacha vizuri nyumba yake kwani alikwishasema akifariki azikwe nyumbani kwake, alizingatia upendo wa Mungu, alishirikiana nasi sana, alikuwa Mtanzania mwema kiongozi mzuri aliyejitoa kusaidia nchi yake," amesema.

Askofu Masangwa amesema msiba wa Zelothe unakumbusha watu kutubu na kutengeza yaliyoharibika kwani kifo kinafika wakati wowote.

Katika msiba huo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Kinana ndiye aliongoza na viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Paul Makonda.

Wengine ni wabunge wa mikoa ya Arusha na Manyara, baadhi ya mawaziri, wakuu wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na mamia ya makada wa CCM.