Sababu kuwepo siku ya bia duniani

Muktasari:

Wakati ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Bia leo, wataalamu wameeleza kinywaji hicho kinapewa umuhimu kwa sababu ya kuwaunganisha watu katika jamii, hasa maeneo yenye changamoto za kiusalama.

Dar es Salaam. Wakati ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Bia leo, wataalamu wameeleza kinywaji hicho kinapewa umuhimu kwa sababu ya kuwaunganisha watu katika jamii, hasa maeneo yenye changamoto za kiusalama.

Siku hiyo huadhimishwa kila Ijumaa ya kwanza ya Agosti na lengo lake ni kufurahia kinywaji hicho.

Bia ni kinywaji kinachopendwa na wengi na kina historia ndefu katika jamii tofauti na wamekuwa wakitumia kinywaji hicho kukaa pamoja na kujadiliana masuala mbalimbali au kufurahi pamoja katika matukio ya kijamii.

Ushahidi wa kale unaonyesha kwamba binadamu alianza kutengeneza bia katika miji ya Babylonia na Misopotania. Wataalamu wa historia wanabainisha kwamba viungo vya bia viliandikwa mwaka 4300 K.K.

Hata hivyo, siku hiyo ilianzia huko California, Agosti 2007 kabla ya kusambaa maeneo mengine duniani na malengo makuu yalikuwa ni kukusanyika na marafiki na kufurahia ladha ya bia, kusherehekea wanaotengeneza na kuhudumia bia na kuunganisha ulimwengu wote kupitia bia.

Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu siku hiyo, Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Innocent Shoo alisema siku ya bia duniani ilianzishwa kutokana na umuhimu wa kinywaji hicho katika kuwakutanisha watu wakakaa na kuzungumza.

“Umuhimu wa bia kama kinywaji ndiyo umefanya kuwe na siku ya kimataifa ya bia. Sasa watu wanapokaa pamoja wanaongea, inawakumbusha kwamba bia inaondoa msongo. “Dunia ina mambo mengi ya stress kama vita, ndiyo maana nchi zote zenye vita unakuta viwanda vya bia vipo, kama havipo lazima wataleta bia kwenye hiyo nchi. Nimekaa Burundi, nimekaa Congo kwenye gari kuna bia, nimekaa Sudan kwenye gari kuna bia, kwa sababu ni stress,” alisema Shoo.

Shoo alibainisha kwamba bia pia inaunganisha watu kwa sababu katika diplomasia ya utamaduni, lazima kuna sherehe ndogo inafanyika na sherehe hiyo inahusisha pia unywaji wa bia.

Aliongeza kwamba siku hiyo pia inawakumbusha watu kunywa kistaarabu kwa sababu wakati mwingine imebainika kwamba watu wakilewa wanapigana, wanatukana watu na wakati mwingine kuchochea mauaji.

“Hii siku ni muhimu kwa sababu bia ni muhimu, inakutanisha watu wengi, lakini pia inawakumbusha watu kunywa kistaarabu,” alisema Shoo wakati akielezea kuhusu siku hiyo ya kimataifa.

Kwa upande wake, mnywaji wa bia, Chrispine Magoti alisema hakuwa anaijua siku ya kimataifa ya bia, hata hivyo anakiri kwamba bia imekuwa na umuhimu katika jamii kwa sababu inawaleta watu pamoja na kuwapunguzia msongo wa mawazo.

“Ukifuatilia watu wanaokunywa pombe, mara nyingi hata familia zao zina amani kwa sababu wanapuuzia mambo mengi ya maudhi kutoka kwa wake zao. Ukinywa pombe unarudi nyumbani kulala, kero zote unazipuuzia tu,” alisema.

Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku hiyo, kampuni ya bia Tanzania (TBL) imezindua kwa mara nyingine kampeni yake ya unywaji bia salama, iliyoanza Agosti mosi hadi Agosti 5, ikiwa na nia ya kuwaelimisha wanywaji na kuwakumbusha hatua za unywaji salama wa bia.

TBL pamoja na kampuni mama ya AB InBev, wamechukua jukumu la kusaidia kupunguza matumizi hatarishi ya pombe ulimwenguni. Mwaka 2015, AB InBev ilizindua malengo ya dunia ya unywaji salama ambayo yanatarajiwa kufikiwa mwishoni mwa mwaka 2025.

Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Jose Moran alisema: “TBL inataka kuwapa wateja wake wote dondoo za unywaji salama kwa kuwa tabia ya unywaji salama imekuwa ni sehemu ya utamaduni wa TBL na AB InBev na tungependa kuiendeleza na kuileta kwenye jamii.”

“Unywaji salama ndio unatufanya tufurahie bidhaa zetu kila mara. Unywaji salama ni zaidi ya kunywa kistaarabu, kwani unaruhusu wanywaji kufurahia bia zao kwa kiwango cha juu zaidi,” aliongeza Moran.

Kwa upande wa Tanzania, TBL inalenga kuwahamasisha kuwa na tabia ya unywaji salama na kupunguza matumizi hatarishi ya pombe na vilevi.

Maadhimisho ya wiki ya unywaji salama ya mwaka huu, yamelenga kubadilisha baadhi ya tabia hatarishi za unywaji zilizozoeleka na kuhamasisha unywaji salama kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanywaji wanafurahia bia kila mara bila kupata athari.

Kupitia kampeni hiyo, TBL inahamasisha unywaji salama kwa kuhimiza wanywaji kunywa maji wakati wa kunywa bia, kula chakula wakati wa kunywa na kuita usafiri wa kurudi nyumbani mapema.