Sababu saratani kuathiri zaidi wanawake
Muktasari:
- Ingawa ugonjwa wa saratani huathiri watu wa rika na jinsia zote, wanawake wametajwa kuathirika zaidi ukilinganisha na wanaume kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mapema wiki hii.
Ingawa ugonjwa wa saratani huathiri watu wa rika na jinsia zote, wanawake wametajwa kuathirika zaidi ukilinganisha na wanaume kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mapema wiki hii.
Taasisi hiyo imesema licha ya idadi ya waathirika wa saratani kuongezeka, kati ya wagonjwa wapya 8,000 na wale wa marudio 68,000 waliopokelewa hospitalini hapo mwaka 2021, asilimia 70 ni wanawake na asilimia 30 ni wanaume.
Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Crispin Kahesa anasema wanawake wana hatari zaidi ya kupata saratani ikilinganishwa na wanaume, hasa kutokana na vihatarishi mbalimbali.
Anasema licha ya saratani ya kizazi inayochangia asilimia 36 na ile ya matiti kwa asilimia 12, wanawake wamekuwa wakiathirika kwa kiasi kikubwa katika saratani nyingine, zikiwemo za utumbo mpana, njia ya chakula, ngozi na hata saratani ya damu.
“Ukiangalia saratani zinazoongoza kwanza ni ile ya mlango wa kizazi ambayo inaathiri wanawake na ile ya matiti inachukua nafasi ya tatu, ukijumlisha idadi hizo ni miongoni mwa saratani ambazo zinaleta uwakilishi mkubwa kwa wanawake.
“Na ukiangalia kwa wanaume wao tezi dume ndiyo inawaumiza zaidi, lakini hizi saratani nyingine wanachangia makundi yote. Ukiangalia saratani ya kichwa, utumbo mkubwa wanaathirika wote ila ya mlango wa kizazi na matiti ndiyo inaathiri zaidi wanawake,” anasema Dk Kahesa ambaye pia ni Mkurugenzi wa huduma za kinga hospitalini hapo.
Mtaalamu wa magonjwa ya saratani kutoka ORCI, Dk Maghuha Stephano anasema wanawake wanaugua zaidi saratani kutokana na aina mbili ya saratani kukua kwa kasi kitakwimu nchini.
Anasema licha ya ugunduzi wa haraka kutokana na kupatikana vifaa vya kisasa na elimu kutolewa, wanawake wamekuwa na mwamko mkubwa kujitokeza kuangalia viashiria vya ugonjwa huo katika hatua za awali.
Usiyoyajua kirusi cha HPV
Wakati saratani ya shingo ya kizazi ikitajwa kuathiri wengi, aina hiyo imekuwa ikisababishwa na virusi vinavyoambukizwa kwa njia ya ngono, kirusi cha Human Papilloma (Human Papilloma Virus) ambavyo husababisha saratani ya mlango wa kizazi.
Saratani ya shingo ya kizazi imeelezwa kukua kwa kasi ya asilimia 36 kati ya zile zinazoshambulia hivi sasa, huku wanawake wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) wakiathirika zaidi.
Takwimu za Ocean Road zinaonyesha aina hiyo ya kirusi imechukua asilimia 36 ya saratani zote, huku kati ya wanawake 100 wanaougua, 60 ni saratani ya shingo ya kizazi huku inayofuata kuua ni ile ya matiti kwa asilimia 12.
Wakati takwimu hizo zikitolewa, katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania imeonyesha kuongoza zaidi huku asilimia kubwa ya wanawake wakikutwa na virusi vya HPV namba 16 na 31.
Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani Hospitali ya Aga Khan, Aleesha Adatia anasema mtu anapopata virusi vya HPV hawezi kugundua kwa kuwa havionyeshi dalili yoyote.
“Virusi hivi havionyeshi dalili yoyote, hii ina maana unaweza ukaishi navyo bila kujua na mwanamke anaweza kukaa na virusi hivi kwa muda mrefu kabla havijamletea madhara ya kuugua saratani,” anasema.
Dk Aleesha anasema kuna aina 200 ya virusi vya HPV na kila kirusi kina namba na vinagawanywa katika pande mbili, kwani vipo vyenye hatari zaidi na visivyo vya hatari.
Anasema virusi visivyo na hatari vinaweza kusababisha maudhi madogo madogo kama vivimbe sehemu za siri, huku vile vyenye hatari vipatavyo 13 vikisababisha saratani.
“Virusi hivi vinaambukizwa kupitia ngozi kwa kugusana. Mtu anaweza kuambukizwa akishiriki ngono ya kawaida, kinyume na maumbile au ngono ya mdomo kwa kugusa nyeti za mwenye virusi pamoja na kutumia vitu mbalimbali vya kushirikiana ukeni,” anasema.
Anapoulizwa iwapo matumizi ya kondomu yanaweza kusaidia mhusika kutokupata maambukizi ya virusi hivyo, Dk Aleesha anasema yanaweza kupunguza hatari za kupata maambukizi kwa kiasi fulani.
“Virusi hivi vinazunguka eneo lote la sehemu za siri au nyeti na si eneo ambalo kondomu inaweza kuvaliwa. Kwa wanaume virusi hivi hukaa sehemu yote ya ngozi inayoshikilia uume, korodani na sehemu ya haja kubwa,” anasema.
Anasema mwanamume akipata virusi hivi atamwambukiza kila mwanamke anayekutana naye kimwili na mwanamke akivipata huchukua kati ya miaka 10 hadi 20 kupata saratani ya shingo ya kizazi.
Dk Maghuha anasema wanaume ambao hawajafanya tohara ni rahisi kupata virusi hivyo, VVU kwa uharaka zaidi na husambaza.
“Kwenye virusi vya HPV ambavyo ndivyo husababisha saratani ya shingo ya kizazi, mwanamume ambaye hajafanyiwa tohara, hukaa kwenye mkono wa sweta na atamuambukiza kila mwanamke anayekutana naye, hivyo inakuwa rahisi kusambaza virusi hivyo,” anasema.
Anapoulizwa iwapo virusi hivyo vinatibika, Dk Aleesha anasema, “Hakuna matibabu ya virusi hivi, lakini matatizo yanayotokana na virusi hivyo ndio hutibika, ikiwemo vivimbe sehemu za siri, ugonjwa wa dysplasia na saratani ya shingo ya kizazi.”
Anashauri watu kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara, ili ikigundulika wapatiwe matibabu mapema.
Sababu kanda ya ziwa kuongoza
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya binadamu Tanzania (NIMR), Profesa Yunus Mgaya aliliambia Mwananchi hivi karibuni kuwa utafiti waliofanya kuchunguza sababu ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kuwa na wagonjwa wengi wa saratani ikilinganishwa na maeneo mengine walibaini kuwa ni mwenendo wa maisha ya watu yamezingirwa na mazingira hatarishi, ikiwemo zebaki.
“Watu wananawa maji yenye zebaki, hilo nimelishuhudia kabisa, tuliamua timu mbalimbali ziende, tuje tuimarishe tafiti kuhusu visababishi,” alisema.
Kwa upande wake, Daktari bingwa kutoka kitengo cha magonjwa ya saratani Hospitali ya Kanda Bugando, Lucas Kiyeji anasema huduma wanazozitoa zinategemewa na mikoa yote kanda hiyo ambayo ni Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Geita, Kagera, Tabora na Kigoma, ambayo ina takribani watu milioni 17, hivyo inaweza kuchangia idadi kubwa ya wagonjwa hasa kutokana na shughuli za kiuchumi zinazofanyika.
“Huku kuna shughuli za uchimbaji wa madini, hivyo kuna uwezekano zipo kemikali ambazo ni chanzo cha idadi kubwa ya wagonjwa, lakini pia katika Ziwa Victoria kuna kichocho ambacho ni kisababishi cha saratani ya kibofu cha mkojo,” anasema.
Dk Kijeji anasema pia baadhi ya wakulima hawana utaalamu wa kutunza mazao, hivyo kuchangia kuwapo kwa sumu kuvu ambayo husababisha homa ya ini ambayo humfanya mtu kupata saratani ya ini.
Alitaja kisababishi kingine kuwa ni maambukizi ya virusi vya HPV na utumiaji wa samaki waliookwa kwa moshi ambao ni moja ya sababu kubwa ya saratani ya kichwa, shingo na njia ya chakula.
“Pia idadi ya wagonjwa wanaokuja Bugando inazidi kuongezeka baada ya Serikali kuwezesha utoaji wa tiba kamili ya saratani, ikiwemo mionzi na kemikali, baada ya kununua mashine za kutoa mionzi ya ndani na nje na kutoa dawa.
“Pia kumekuwa na mwamko na uelewa kuwa huduma hizi zinapatikana kanda ya ziwa, maana zamani huduma hizi zilikuwa zikipatikana Hospitali ya Ocean Road pekee,” anasema.
Hata hivyo, anasema idadi ya wagonjwa inatarajiwa kuongezeka baada ya uzinduzi wa jengo la kulaza wagonjwa wa saratani lililojengwa kwa msaada wa Serikali kwa Sh5 bilioni litakalokuwa na vifaa vyote vya radiolojia. Ujenzi huo upo hatua za mwisho.
Anasema baada ya ufunguzi wa jengo hilo, mashine zitaongezwa pamoja wataalamu, ili kuboresha huduma.
Pamoja na hayo, anasema tafiti zinaendelea, ili kujua kwa uhakika vipi ni visababishi vya idadi kubwa ya wagonjwa katika eneo hilo.
Ili kukabiliana na hali hiyo, Daktari huyo anashauri jamii iongezewe uelewa na mwamko wa kufanya vipimo vya magonjwa ya saratani.
Anasema ni muhimu kuwapata wagonjwa wakiwa katika hatua za awali, ili kupata matokeo mazuri ya tiba.
Kuhusu chanjo ya HPV
Katika kukabiliana na virusi hivyo, ipo chanjo ambayo hutolewa kwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka tisa hadi 14.
Tafiti zinaonyesha chanjo hiyo inaleta matokeo chanya pale inapotolewa katika umri huu na hutoa kinga ya muda mrefu dhidi ya virusi hivyo.
Wataalamu wa magonjwa ya saratani wanasema chanjo hiyo haina madhara na ina matokeo chanya inapotolewa katika umri huo.
Dk Kahesa anasema chanjo hiyo hulenga umri huo kwa kuwa inaaminika mabinti wengi hawajaanza kushiriki ngono, lakini ikiwa ameshapata haiwezi kuwa na madhara kwa kuwa ni kwa ajili ya kumkinga na si kumtibu.
Mwaka 2018 Serikali Tanzania ilianza kutoa chanjo kwa wasichana 614,734 wenye umri wa miaka 14, ili kuwakinga na saratani ya shingo ya kizazi.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema asilimia 70 ya wagonjwa wa saratani ni wanawake, hivyo kushauri huduma za uchunguzi zianzie ngazi za chini ili kuwaokoa wengi katika hatua za awali.
Anasema Serikali inatumia Sh5 milioni kumtibu mgonjwa mmoja wa saratani ya shingo ya kizazi, mbali na fedha ambazo familia inatumia kumtibu pamoja na vipimo vingine.