Sababu Serikali kudhibiti kampuni changa
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew
Muktasari:
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew amesema lengo la Serikali kuweka udhibiti kwa kampuni change, ni kuzisaidia kukua na kustawi na sio kuweka vizuizi kama ambavyo wengi hudhani.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew amesema lengo la Serikali kuweka udhibiti kwa kampuni changa, ni kuzisaidia kukua na kustawi na sio kuweka vizuizi kama ambavyo wengi hudhani.
Kundo amesema hayo leo Jumatatu, Desemba 18, 2023 jijini Dar es Salaam katika mkutano wa mwaka uliowakutanisha wajasiriamali na wabunifu wachanga chini chama cha ‘Tanzania Startups Association’ (TSA).
Amesema wizara imeanzisha mchakato wa kutengeneza muongozo wa namna ya kudhibiti bidhaa zinazozalishwa na kampuni changa.
Amesema kuna dhana hasi ambayo imejengeka kwa watu kuhusu udhibiti ambapo wengi hudhani ni kuweka vizuizi kwenye bidhaa za kampuni changa jambo ambalo sio lengo la udhibiti huo.
"Tunataka kukuza na kuendeleza. Tunataka kuwa na muongozo ambao utatuonyesha njia sahihi ya kupita ili kufika kule ambako tunataka kufika," amesema.
Ameongeza kuwa lengo la udhibiti ni kuzisaidia kampuni hizo dhidi ya utapeli ambao umekuwa ukishamiri siku hadi siku kulingana na kukua kupitia teknolojia, hivyo udhibiti utasaidia kumlinda mjasiriamali mdogo ili aweze kukua na kustawi.
Pia amesema Serikali imeanza mchakato wa kuandaa sera hiyo inayowalenga wabunifu wachanga.
Naye mmoja wa wanachama wa TSA walioshiriki katika mkutano huo, Patrick Kas, amesema ni vizuri kuwa na udhibiti lakini ni muhimu zaidi mamlaka kujikita katika kuziwezesha kampuni zinazoanza, kuliko kuegemea zaidi upande wa kodi ambao unawafanya waonekane maadui kuliko wawezeshaji.
"Ni vizuri mamlaka zikatambua kuwa kampuni zinazoanza zinahitaji muda kwa ajili ya kujiimarisha sokoni ndipo ziweze kuwa na uwezo wa kulipa kodi. Ni kweli wanafuata sheria lakini kungekuwa na ahueni kwa wale wanaoanza ili waimarike halafu baadaye mamlaka itakuwa na uhakika wa kupata kodi kuliko kuzikaba kipindi ambacho bado ni changa jambo ambalo linasababisha kampuni nyingi kufa," amesema na kuongeza kuwa kuna kampuni zinaanzishwa kwa fedha za mikopo na ufadhili.
Kas ameshauri mamlaka kuvutia zaidi uanzishaji wa kampuni ikiwemo kampuni kuanzishwa bila kulipia kuliko kujikita zaidi kwenye kuchukua kodi peke yake.
Katika mkutano huo TSA imempatia tuzo aliyewahi kuwa Gavana Mkuu wa Benki Kuu (BoT) Profesa Beno Ndulu katika kutambua mchango wake katika sekta ya ujasiriamali na ubunifu hapa nchini.
Akizungumzia tukio hilo Mkurugenzi Mkuu wa TSA, Zahoro Muhaji amesema chama hicho kimempa Profesa Ndulu tuzo hiyo inayojulikana kama Lifetime Achievement Award.
"Tunafahamu kwamba kipindi akiwa gavana alisaidia sana kwenye masuala ya pesa mtandao. Wakati pesa mtandao inakuja nchini hakukua na sheria kuhusu pesa mtandao lakini yeye ndiye alipambana na kusaidia jambo hilo kutokea hapa nchini," amesema Zahoro.
Kuhusu sera ya ujasiriamali na ubunifu, Zahoro amesema wanategemea hivi karibuni sera hiyo itapelekwa kwa wananchi na wadau ili watoe mapendekezo na hatimaye ipelekwe kwenye baraza la mawaziri na kupitishwa na kuwa sera rasmi.