Sababu ujenzi shule ya Museveni Chato yatajwa

Rais wa Uganda, Yoweli Museveni (kushoto) akikabidhi mfano wa funguo yenye rangi ya bendera ya Uganda kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (kulia) ikiwa ni ishara ya makabidhiano ya shule ya msingi Museveni iliyojengwa wilayani Chato kwa ufadhiri wa serikali ya Uganda. Ujenzi wa shule hiyo umegharimu Sh3.9 bilioni. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema wazo la ujenzi wa Shule ya Msingi Museven lilianza Julai 13, 2019 wakati wa ziara ya Rais wa Uganda, Yoweri Museven aliyoifanya katika Wilaya ya Chato baada ya kualikwa na aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Dk John Magufuli.

Chato. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema wazo la ujenzi wa Shule ya Msingi Museven lilianza Julai 13, 2019 wakati wa ziara ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliyoifanya katika Wilaya ya Chato baada ya kualikwa na aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Dk John Magufuli.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano na ufunguzi wa shule hiyo, Profesa Ndalichako amsema wakati wa ziara hiyo, Rais Museven aliomba eneo ili aweze kujenga shule ya msingi wilayani humo kama zawadi kwa Watanzania.

“Kutokana na heshima kubwa na nia njema ya Rais Museven, Serikali ilitenga eneo lenye ukubwa wa ekari 11.7 kwa ajili ya ujenzi wa shule hii,”amesema

Amesema eneo hilo limepimwa na kusajiliwa plot namba 51/block B nyamilezi ambapo ujenzi huo ulianza Februari 11, 2020 na kukamilika Februari 11 mwaka huu.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), David Silinde amemuhakikishia Rais Samia kusimamia uendeshaji wa shule hiyo kwa kuhakikisha upatikanaji wa watumishi, thamani, vifaa vya kutosha ili kuleta mafanikio yaliyokusudiwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amesema ujenzi wa shule hiyo umeufanya Mkoa wa Geita kuwa na jumla ya shule za Msingi 702 kati ya hizo shule 653 ni Serikali.

“Idadi ya Shule za namna hii ambazo zinafundisha lugha ya kiingereza zipo 50 na leo tunashuhudia tukiongeza shule moja nakufanya shule ambazo zitafundisha lugha ya kiingereza kuwa 51 katika hizo ni shule mbili tu zitakuwa zinamilikiwa na Serikali,”amesema

Amesema katika Wilaya ya Chato kuna shule za msingi 143 ikiwemo hiyo ya Museven.

Amesema shule hiyo imeshasajiliwa mwaka huu na inatarajia kupokea wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza Januari, 2022.

Amemshukuru Rais Yoweri Museveni pamoja na Serikali yake ya Uganda kwa kufadhili ujenzi wa shule hiyo akidai itapunguza changamoto ya wanafunzi kurundikana darasani.