Sababu uwezo wa kuzaa kwa wanawake kushuka

Muktasari:

Je, miaka 30 ijayo mwanamke wa Tanzania atakuwa na uwezo wa kujifungua wastani wa watoto wangapi?


Dar es Salaam. Je, miaka 30 ijayo mwanamke wa Tanzania atakuwa na uwezo wa kujifungua wastani wa watoto wangapi?

Swali hili najiuliza baada ya ripoti ya ‘Tanzania in figures 2021’ kuonyesha uwezo wa kuzaa wa wanawake nchini umeshuka kwa asilimia 18 ndani ya miaka 17.

Ripoti hiyo inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeonyesha kupungua uwezo wa kuzaa kwa wanawake kutoka wastani wa watoto sita 2004/2005 hadi 4.9 mwaka 2021.

Takwimu hizi zinamaanisha kila mwaka wanawake wa Tanzania wanapunguza idadi ya kuzaa watoto kwa asilimia moja.

Licha ya idadi hiyo kuzidi kushuka, kwa upande wa Tanzania bara takwimu zinaonyesha wanawake wa vijijini bado wana uwezo mkubwa wa kupata watoto wengi hadi kufikia sita ikilinganishwa na wale wa mijini ambao hupata watoto wanne tu, ikiwa ni tofauti ya watoto wawili.

Daktari wa magonjwa ya ndani Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila, Innocent Tesha alisema sababu kubwa ya uzazi wa wanawake wa mijini kuwa wa kiwango cha chini ni pamoja na mfumo wa maisha wanayoishi.

“Mfumo wa maisha unaanzia kwenye ulaji wa chakula, muda wao katika familia na matumizi ya kemikali kwenye ulaji na urembo. Kwa upande wa vijijini wanawake wana mazoezi ya kila aina, yakiwamo ya kutembea, kufanya kazi na hata lishe yao ni tofauti na wa mjini,” alisema Dk Tesha.

“Lakini mijini kama mtu hana gari anapanda mwendokasi, kwa hiyo mfumo wa maisha bwete unafanya mishipa ya damu kushindwa kuwa na msaada kwenye masuala ya uzazi.”

Dk Tesha akizungumzia ulaji alisema, wanawake wa vijijini wanakula vyakula asili vyenye virutubishi muhimu kwenye utengenezaji wa mimba, huku wanawake wa mjini wakiwa waathirika wa vyakula vilivyokwisha kuandaliwa haraka ambavyo havina msaada wowote kwenye utungishwaji wa mimba ya mtoto.

Kwa upande wake, Dk Edson Francis alisema wanawake wa mjini wanaogopa maumivu ya kuzaa kwa njia ya kawaida na wengi wanakimbilia kufanyiwa upasuaji ambao unakuwa na ukomo wa idadi ya watoto.

“Kwa mazingira ya mjini wanawake wengi wanatumia mfumo wa maisha ya magharibi, utakuta muda wa kuzaa atazaa lakini ataomba kuzaa kwa upasuaji, sasa mwanamke yeyote anayejifungua kwa upasuaji uzazi wake unakuwa na ukomo,” alisema Dk Francis.

“Ukifanyiwa upasuaji watoto tunashauri mwisho watatu, sasa wanawake wa mijini wanaepuka maumivu wakati wa uzazi kwa njia ya kuomba kufanyiwa upasuaji, tofauti na wa vijijini.”

Jambo lingine alilotaja Dk Francis ni matumizi ya dawa za kuzuia mimba ambazo zimekuwa zikitumiwa zaidi na wanawake wa mijini na huathiri homoni na kuchangia mwanamke kuwa na mtoto mmoja au wachache kulinganisha na vijijini.

Daktari kutoka Kituo cha Afya Haffarod Health Clinic ya Temeke, Ford Chisongela alisema uwezo mkubwa wa wanawake wa vijijini kuwa na watoto wengi ikilinganishwa na wa mijini inatokana kuwa mbali na njia za uzazi wa mpango.

“Pia, wanapata muda mwingi kuwa na wenza wao, jambo lingine utamaduni, wanaona ni fahari kuwa na watoto wengi,” alisema.

Dk Chisongela alisema umaskini unaweza kuchangia wanawake wa vijijini kushindwa kufikia huduma nyingi za afya, hali ambayo huwa na matokeo makubwa kwenye ongezeko la uzazi.

Alitaja ukosefu wa elimu, utamaduni maeneo ya vijijini kuwa na matokeo makubwa kwenye ongezeko la kuzaliana vijijini.

“Kwa watu wa mijini muda mwingine wanachelewa kupata watoto kutokana na kutumia muda mwingi kwenye kusoma, pia wanaume wenyewe hawapendelei kuoa wanawake ambao wamewazidi kipato, hilo linaweza kuchangia pia,” alieleza.


Dawa kunogesha tendo la ndoa

Mkazi wa Mabibo, Dar es Salaam, Veronica Magonjeka alisema wanawake wengi wa mjini wanasumbuliwa na uzazi kwa sababu ya dawa za kuongeza utamu wa tendo la ndoa ambazo nyingi wanazinunua mitandaoni.

“Sasa hivi ukiingia kwenye mitandao ya kijamii unakuta kuna watu wanajiita makungwi ambao wanauza dawa za kuongeza utamu wa tendo la ndoa, mara nyingi maelezo yake ni kuziweka sehemu za siri, kitu ambacho nahisi kina madhara,” alisema Veronica.

Mkazi wa Temeke, Aisha Zuberi alisema, kulingana na hali ya maisha ni nadra mtu kuwa na watoto wengi huku akiwa na kipato chenye shaka.

“Umaskini ni mkubwa kwenye familia nyingi, ukisema uwe na watoto watano utawapa nini, wanaume wengine kwanza kutoa matunzo ya mtoto mmoja wanakimbia,” alisema Aisha.

Kutokana na hali hiyo, Aisha alisema wanawake wengi wamekuwa watafutaji zaidi ya wanaume, hivyo muda mwingi utatumika kutafuta badala ya kujenga familia.

“Ukienda Soko la Tandika, Manzese au kokote asubuhi sana utawakuta wanawake na mizigo ya biashara, ukienda vijijini mwanamume kwa kiwango kikubwa ndiye anayewajibika, kama mwanamke atashiriki, ni kwenye shughuli za nyumbani, hivyo lazima apate muda wa kutosha kuwa na mwenzi wake,” aliongeza.


Hali ilivyo vijijini

Naisioki Mollel, mkazi wa Sekei wilayani Arumeru mkoani Arusha alisema wanawake wengi wa vijijini wanakubali kuzaa watoto kwa sababu wana muda wa kutosha kuwalea.

“Huko mjini wengi wanatumia wasaidizi wa kazi za ndani kwenye malezi wao, wanakwenda kuhangaika kutafuta hela, sisi kwetu huku ni tofauti, tunaangalia zaidi kuongeza familia na hatuhofii suala la mali kwa sababu tuna mashamba, tofauti na wenzetu (wakazi wa mjini),” alisema Mollel.

Alisema wanawake wengi wa mijini wanaogopa kuonekana wazee kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto.

Award Mpandilah, mkazi wa Makete alisema suala la uzazi vijijini huja kama baraka na hakuna matumizi ya uzazi wa mpango.

“Mjini wanapanga uzazi kwa sababu ya hofu ya gharama za maisha, wengine wanapenda watoto wengi lakini wanakumbana na changamoto ya vidhibiti mimba ambavyo huwakosesha watoto wakiwa na uhitaji,” alisema Mpandilah.

Alisema vyakula wanavyokula watoto kijijini ni vya asili na huwasaidia kuwajengea uimara kwenye mfumo wa uzazi na kuwa na watoto wengi.


Geita washindana kuzaa

Jana, mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku “Msukuma” kwenye ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani humo alisema wakazi wa mji mdogo wa Katoro wanashindana kuzaa ili wakajaze madarasa yaliyojengwa kupitia mradi wa Uviko-19.

Pia, alisema katika eneo hilo linalokadiriwa kuwa na kaya zaidi ya 140,000, watoto 3,000 huzaliwa kwenye kituo kimoja cha afya kila baada ya miezi mitatu.

“Busanda peke yake ina wakazi zaidi ya 800,000 na Geita Vijijini ina wakazi 500,000, yaani kila baada ya miezi mitatu hapa tunazaa shule ya msingi, tuna shule zaidi ya 20, pia ikikupendeza kwa vile waziri wa afya yuko hapa atupatie DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) mwingine, ni ngumu sana DMO anatoka Nzera anakuja huku, sote tuna mahitaji,” alisema.


Walichokisema wanasaikolojia

Mwanasaikolojia Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya Kitengo cha Saikolojia Tiba, Yisambi Mbuwi alisema tofauti ya uzazi wa mwanamke wa vijijini na mijini imechangiwa na mapokeo ya elimu ya uzazi wa mpango.

“Wanawake wa vijijini wengi wanatumia njia za asili na muda mwingi wanawaza namna ya kuongeza watoto na kuwa na watoto wengi, tofauti na wa mijini wanaowaza malezi na ukiwa na watoto wengi inaonekana ni fedheha,” alisema mwanasaikolojia huyo.

Mbuwi alisema kutokana na masuala ya uzazi kuonekana sehemu ya sifa kwenye jamii vijijini, ni kawaida mwanamke mwenye umri wa miaka 22 na kuendelea kuwa na watoto zaidi ya sita, pia ni nadra kujifungua kwa njia ya upasuaji ambayo huwa na ukomo wa uzazi.

Jambo lingine alilotaja, wanawake wa mijini wengi kabla ya kuwa na watoto wanawaza mambo mengi, ikiwamo kuwasomesha kwenye shule nzuri na kuwapatia chakula, tofauti na vijijini ambao hawana wasiwasi juu ya vipato vyao na mambo mengine hufuata baada ya mtoto kuzaliwa.

Mwanasaikolojia Naima Omary aliitaja sababu ya hofu ya kufa wakati wa kujifungua kama sababu inayopunguza kasi ya wanawake wa Tanzania kujifungua watoto wengi.

“Kisaikolojia mwanamke anapata hofu pale anapopata simulizi za yale mambo yanayotokea leba (chumba cha kujifungulia). Wengi wanasimuliwa kwamba ni tukio linalohatarisha maisha na watu hufariki dunia,” alisema Naima.

Pia, alisema hofu hiyo inasababisha wanawake wengi kuogopa kuzaa kabisa au kuwa na idadi ndogo ya watoto.


Vifo na uzazi tishio

Ripoti ya Jamii na Afya (TDHS) ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa mwaka 2015/16 inaonyesha kuna vifo 556 vya uzazi katika kila vizazi hai 100,000, huku idadi hiyo ikiongezeka kutoka vifo 432 vya uzazi mwaka 2012 sawa na ongezeko la asilimia 28.7.

Mwaka 2010, TDHS iliripoti kuwepo kwa vifo vya uzazi 454 nchini, huku vikipungua kutoka 578 mwaka 2004/05.

Kwa mujibu wa takwimu za vifo vya uzazi, nchi za Afrika Mashariki zinaonyesha Tanzania inaongoza huku ikifuatiwa na Uganda, yenye wastani wa vifo vya uzazi 368 kati ya vizazi hai 100,000 na Kenya ikiwa na vifo vichache zaidi, 355.


Namna ya kuzuia tatizo hilo

Akieleza namna ya kuzuia tatizo hilo la kupata watoto wachache, Dk Tesha alisema, ni muhimu kwa wanawake kubadili aina ya lishe na kuzingatia zaidi ulaji wa vyakula asilia vyenye matokeo makubwa zaidi kwenye ujenzi wa mwili.

“Jambo lingine ni kutenga muda na familia, wanawake wengine wa mijini wamekuwa watafutaji, hivyo unakuta muda wa kujenga familia na kupata mtoto unakuwa mdogo sana, huku pia wanawake inatakiwa wafanye mazoezi yatakayoushughulisha mwili,” alisema Dk Francis.

Pia, alishauri ni muhimu kubadili mfumo wa maisha, hasa kuchukua tahadhari kwenye uzazi wa mpango, pamoja na kutokimbilia kujifungua kwa njia ya upasuaji.

“Tutumie njia ambazo ni rafiki kwetu, kama hujaandikiwa ujifungue kwa upasuaji si vyema kuomba kujifungua kwa njia hiyo.”

Jambo lingine analoshauri Dk Tesha kama suluhisho la tatizo hilo ni wanawake kupata muda wa kutosha kupumzika ili mwili upate nafasi ya kujijenga zaidi.

“Ukiwa na muda wa chini ya saa sita mpaka nane wa kupumzika unasababisha mwili kukosa nafasi ya kujijenga upya, hivyo mwili kuanza kuchoka na kuchakaa,” alisema.

Hata hivyo, ripoti ya TDHS ya mwaka 2015/16 inaonyesha kuwa wanawake wa Tanzania bara walikuwa na uwezo wa kuzaa watoto 5.2, huku wa Zanzibar wakiwa na uwezo wa watoto 5.1 kabla ya kushuka hadi kufika 4.9 mwaka 2021.

Imeandikwa na George Helahela, Baraka Loshilaa na Mgongo Kaitira