Sababu vijana kupenda uhusiano na watu wazima

Monday September 12 2022
uhusiano pic
By Elizabeth Edward

Wakati takwimu za ndoa zinazovunjika zikizidi kupaa na jiji la Dar es Salaam kuwa kinara, huenda hali ikawa mbaya zaidi kutokana na ugumu wa maisha unaoendelea na kuwafanya vijana wengi wa kiume kuamini katika mapenzi na wanawake waliowazidi umri.

Hivi karibuni taarifa kutoka Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ilionyesha hali ya kuvunjika kwa ndoa katika jiji la Dar es Salaam imezidi kuwa kubwa na takwimu zinaonyesha ndoa 300 zinavunjika kila mwezi.

“Huyu mwanamke lazima nimuache, nikiachana naye sitaki tena kuishi na mwanamke, nitakaa mwenyewe.

Nahitaji kuwa mwanamke mtu mzima ambaye nitakidhi haja zangu za kimwili na atanisaidia kwenye maisha yangu.

“Sioni faida ya kuwa na mwanamke ambaye unamhudumia kwa kila kitu, halafu bado hakuelewi ni bora niende kwa mtu mwenye shida na mimi na atanipatia pesa zitakazonisaidia kuendesha maisha.”

Hiyo ni kauli ya kijana mmoja dereva wa bodaboda, anayezungumza na abiria wake akimueleza hali ya ndoa yake na mpango alionao kumuacha mkewe, ili awe huru na mwanamke mwenye umri mkubwa kuliko yeye (shugamami).

Advertisement

Kijana huyo aliendelea, “Yani nakwambia nimepata mwanamke mtu mzima ana akili zake na anajielewa na kujua maisha ni nini, ana kila kitu na yuko tayari kunisaidia katika changamoto zangu, anachotaka ni kuwa huru hataki kuchanganywa, sasa siwezi kumpoteza huyu kwa sababu ya mke.”

Akionyesha amedhamiria kwa dhati kutekeleza hilo, alieleza hadi mpango wake katika kulifanikisha ikiwemo kuwapeleka kwa wazazi watoto wake, ili awe na uhakika na usalama wao wakati yeye akiwa shugamami wake.

Huo ni mfano mmoja, ila wapo vijana wengi wenye mawazo ya aina hiyo akiwemo Seleman Chota, mkazi wa Mbagala Kongowe anayesema atakuwa tayari muda wowote kuacha mahusiano yake endapo atatokea kupendwa na mwanamke mwenye fedha.

“Hivi nitakuwa mtu wa aina gani kama bahati imekuja mikononi mwangu halafu niiache, akija mwanamke mwenye fedha bila kujali umri wake, ili mradi ameonyesha kunihitaji siwezi kukataa.

Ni bora niwe na mtu atakayenisaidia kwenye maisha kuliko kung’ang’ania hawa wasichana wamejaa kiburi.

“Ukipata mtu mzima kwanza anajua nini maana ya maisha, ameshaishi labda amefiwa na mumewe au wameachana, hivyo atakuwa tayari anafahamu umuhimu wa mwanaume, heshima inakuwepo, hivyo kwenye uhusiano wenu mtakuwa mkiheshimiana,” anasema Chota.

Wakati hao wakiwaza hivyo, mambo ni tofauti kwa George Nickson anayesema kwa namna yoyote ile hawezi kuingia kwenye uhusiano na mtu aliyemzidi umri hata kama kuna kitu anaweza kukipata kutokana na uhusiano huo.

Nickson anakiri kuwa kinachowasukuma vijana wengi kuwa na uhusiano wa aina hiyo ni ugumu wa maisha na ndiyo sababu wako tayari kufanya vitu visivyofaa, ili waweze kuendesha maisha.

“Kama wewe kijana unajitambua utapambana kwa namna yoyote ile, ili uendeshe maisha, ukiona mtu hadi anafikia kuwa kwenye uhusiano na mwanamke mwenye umri wa sawa na mama yake au aliyemzidi kwa namna yoyote ile ni wazi kuwa uvivu unampeleka huko.

Anafanya hivyo akiamini atapata kila anachotaka na maisha yake yatakuwa mtelezo. Naona vijana wengi wanaangukia kwenye kundi hili na stori ndiyo zimekuwa hivi vijiweni,” anasema.


Kitaalamu hii imekaaje?

Mshauri wa mahusiano, Deogratius Sukambi anasema tatizo hilo ni kubwa kuliko inavyoelezwa na upo uwezekano miaka 15 hadi 20 ijayo, hali ikawa mbaya zaidi kuliko ilivyo sasa kutokana na malezi wanayopewa watoto.

Anasema malezi hayo yanawafanya watoto wa kiume wategemee zaidi kupewa na si kutoa na ndiyo maana wako tayari kuwa kwenye uhusiano na watu waliowazidi umri.

Mtaalamu huyo anaeleza malezi ya hovyo kwa watoto wa kiume yanatengeneza makundi ya wanaume, makundi hayo ni wale ambao wanatambua majukumu yao, lakini hawana uwezo, hivyo wanaacha kwa wenza wao huku kundi la tatu likiwahusisha wanaocha kwa makusudi kuhudumia familia pindi wanapoona mwanamke anabeba majukumu yake.

Anaeleza kundi la mwisho ni hatari zaidi na kukabiliana nalo ni muhimu mwanamke kutambua mwisho wa majukumu yake na kumuacha mwenza wake atimize ya kwake kinyume na hapo mwanaume ataona amedharaulika.

“Si kitu cha kawaida mwanaume kutegemea kuhudumiwa na mwanamke au kuacha majukumu yake yafanywe na mkewe.

Inapofika hatua hii, lazima tujiulize tumekosea wapi maana tusipoangalia kama wanajamii hali itakuwa zaidi ya ilivyo sasa.

“Wazazi tuache kuwalea watoto wetu kama kuku wa kizungu, yani kila anachokitaka anakipata kwa wakati anaotaka yeye.

Hii haimsaidii mtoto anakuwa akiamini kwamba anatastahili kupewa kila anachohitaji.

Hili ni bomu lingine linalokuja miaka 20 ijayo kutokana na wazazi wengi tunavyolea watoto,” anasema Sukambi.

Mshauri huyo anaeleza ili kubadili mwenendo huo ni muhimu kuanzia sasa watoto walelewe katika mazingira yatakayowajengea kuchangamsha ubongo na si kuwa na uhakika wa kila anachokiamini.

“Mtoto anapaswa kuelewa si kila anachotaka atapata kwa wakati anaotaka yaani siku hizi utasikia mtoto anaamua shule hii haitaki anataka ile, ni muhimu wazazi tuwafundishe kwamba kwenye huu ulimwengu si kila unachotaka utakipata kwa urahisi.

“Pia tuache kuwafuatilia na kuwalinda kupita kiasi, kuwa overprotective hakumsaidii mtoto, wakati mwingine muache uone namna anavyoweza kushughulisha ubongo wake.

Mpe mtoto nafasi ya kutoa mawazo na afahamu kuwa si kila mawazo yake yatakubaliwa na ikitokea hayajakubaliwa mpe sababu za hilo,”anasema Sukambi.

Advertisement