Sababu wanafunzi wengi nchini kurudia mtihani kidato cha pili

Muktasari:

Wakati idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa kuingia kidato cha kwanza ikiongezeka, inaelezwa kuwa wanafunzi wengi hulazimika kurudia mtihani wa mchujo wa kidato cha pili.

Dar e Salaam. Wakati idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa kuingia kidato cha kwanza ikiongezeka, inaelezwa kuwa wanafunzi wengi hulazimika kurudia mtihani wa mchujo wa kidato cha pili.

Kwa mujibu wa wadau na wachambuzi wa masuala ya elimu, sababu kubwa ni kuwapo kwa wanafunzi wenye uwezo mdogo wanaochaguliwa kujinga na kidato cha kwanza.

Mwaka 2020 asilimia 85 walirudia darasa katika ngazi mbalimbali wakiwamo wa kidato cha pili na asilimia 83 walirudia mwaka 2019.

Ripoti ya Tamisemi inabainisha kuwa kwa miaka mitano mfululizo kati ya 2016 hadi 2020 wanafunzi wa kidato cha pili wanaorudia imeongezeka kwa asilimia 32.16.

Hiyo ikiwa na maana kuwa idadi yao ilitoka 20,426 mwaka 2016 hadi wanafunzi 27,086 mwaka 2020.

Ikilinganishwa na idadi ya jumla ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita waliorudia kwa miaka mitano mfululizo kati ya wanafunzi 142,359 waliorudia, 1155,803 walikuwa wa kidato cha pili. Hiyo ikiwa na maana kuwa asilimia 81.34 ya wanafunzi waliorudia darasa kwa miaka mitano iliyopita walikuwa kidato cha pili.

Wakati hali ikiwa hivyo, wadau wa elimu wanaunyooshea kidole mfumo wa wanafunzi kujiunga na sekondari wanaopotoka shule ya msingi na kupendekeza kuwa, wanafunzi wanaofaulu kujiunga kidato cha kwanza wapewe mtihani kabla ya kuanza masomo na wengine wakishauri wanaojiunga kidato cha kwanza wawe ni wale waliofaulu na si kuchaguliwa.

Kufanya hivyo kumetajwa kuwa kutasaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wanaoshindwa kufaulu mtihani wa taifa kidato cha pili, jambo linalowafanya kusoma darasa hilo mara mbili baada ya kurudia.


Shule za Serikali balaa

Idadi ya wanaorudia darasa hilo katika shule za Serikali ni wengi kuliko wa shule binafsi. Katika mwaka 2020 wanafunzi 1,954 kutoka shule binafsi walirudia darasa huku wa shule za Serikali wakiwa 30,066.


Serikali ina mkakati?

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo alisema wanafunzi wa kidato cha pili wanaonekana kuwa wengi kati ya wale wanaorudia kwa sababu ndiyo darasa pekee ambalo linatoa fursa hiyo.

Kutokana na hilo alisema juhudi za ufundishaji zinaendelea ili kuondoa au kupunguza wimbi hilo la wanaorudia.

“Ni juhudi za kawaida zinazoendelea, hakuna juhudi mahususi zilizowekwa kwa ajili ya darasa hilo pekee, bali wanafundishwa,” alisema Dk Akwilapo na kufafanua kuwa mwanafunzi aliyefundishwa vizuri hawezi kushindwa mitihani yake, huku akibainisha kuwa mbinu hiyo itazaa matunda


Wasemavyo wadau

Nicodemus Shauri, Meneja Programu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) alipendekeza mfumo wa zamani uanze kutumika, ambao badala ya wanafunzi kuchaguliwa kuendelea na sekondari, sasa kigezo kiwe ni kufaulu mitihani tena kwa alama za juu.

“Sasa hivi unakuta hata mzazi anashangaa mwanawe amefaulu vipi kwenda kidato cha kwanza maana hajui chochote na wanachukuliwa hadi wenye ufaulu wa chini,” anasema Shauri.

Anasema kama sio mfumo huo basi wanapochaguliwa kidato cha kwanza wapewe tena mtihani wa kupimwa, ili wabainike wale walio na uwezo wa kuendelea kwa kile alichobainisha kwamba, katika shule za msingi kuna udanganyifu unaofanyika wakati wa mitihani ya mwisho.

‘‘Shule za msingi hivi sasa kuna udanganyifu mkubwa, hasa shule binafsi, kwa sababu tunaangalia kufaulu mtihani sasa ni bora waanze kupimwa kwa uelewa,” anasema Shauri.

Anasema kitendo cha kuwapitisha wanafunzi hadi wasio na uwezo, matokeo yake yamekuwa yakionekana wanapofika kidato cha pili wanapokwama.

“Tukumbuke kuwa uwezo wa mtu hauko katika taaluma tu lakini sera inalazimisha watu wote wawe wana taaluma kitu ambacho hakiwezekani.Kuna watu hawawezi kusoma ila wana vipaji tofauti, lakini hatuwezi kuwaendeleza kwa kutaka wote wawe kwenye barabara moja,’’ anaeleza.

Hata hivyo, anasema tatizo lililopo sasa ni mfumo wa elimu kudhani kuwa wanafunzi wote wana uwezo wa kusoma kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na wote wawe wanafaulu.

Anasema kinachosomwa sasa hakipimi uwezo wa mtu huku akibainisha kuwa mtu asipojua hesabu huenda akawa ni mchoraji mzuri.

Anaungwa mkono na Dk Luka Mkonongwa, mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) aliyesema umefika wakati sasa wanafunzi waingie kidato cha kwanza, kwa kuzingatia alama nzuri za ufaulu na si kuchaguliwa.

Anafafanua, wanafunzi wamekuwa wakichaguliwa kuziba nafasi katika shule zilizo na uhitaji kwa sababu hadi kidato cha nne bado inahesabiwa kama elimu msingi.

“Matokeo yake tunachukua na waliopata alama ndogo sana, ukifika sekondari utawatambua,” anasema Dk Mkonongwa.

Anasema moja ya kitu kinachoweza kupunguza kiwango cha watu kurudia kidato cha pili, ni kuhakikisha wamefaulu mtihani wao wa darasa la saba kwa alama nzuri ili kuhakikisha kuwa wanaoingia sekondari ni wale bora.

Mtafiti wa masuala ya elimu, Muhanyi Nkoronko alitaka uwekezaji kwa walimu na miundombinu ya kujifunzia na kufundishia kuangaliwa kwa ukaribu.

Hiyo ni kwa sababu baadhi ya shule wanafunzi huwa ni wengi katika darasa moja, jambo ambalo linaweka ugumu kwa mwalimu kumfikia mmoja mmoja hivyo, hivyo baadhi kujikuta wanaachwa nyuma.

“Serikali ijenge madarasa zaidi na kuongeza walimu kulingana na idadi ya wanafunzi ili kuboresha ujifunzaji na ufundishaji,” anasema Nkoronko.

Alitumia nafasi hiyo kushauri kuwa njia nyingine inayoweza kuondoa kiwango cha wanafunzi wanaorudia ni Serikali kuwekeza katika elimu ya makuzi kwa wanafunzi wa sekondari ili kuweza kusaidia kuboresha elimu.

Hiyo ni kutokana na kile alichobainisha kuwa wanafunzi wengi wa kidato cha pili, wanatoka kwenye ngazi ya utoto kwenda utu uzima.

“Sasa kukosekana kwa elimu ya makuzi na malezi, wanashindwa kuelewa kuwa wanatakiwa kusoma. Wengi hawatilii mkazo yale masomo. Serikali inatakiwa kuwekeza kuwafundisha elimu ya jinsia, namna ya kusoma, kuishi na kujielewa na kujitambua,” anasema Nkoronko.

Alisema hilo likifanyika vyema, linaweza kusaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wanaorudia darasa tofauti na sasa.