Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu wanaojifungua kwa upasuaji kuongezeka hizi hapa

Muktasari:

  • Takwimu zikionyesha idadi ya wanaojifungua kwa njia ya upasuaji ikiongezeka mwaka 2022, wenye elimu na kipato wanaongoza kwa kutumia njia hiyo, huku wataalamu wa afya na wananchi wakiutaja woga wa uchungu kuwa sababu.

Dar es Salaam. Takwimu zikionyesha idadi ya wanaojifungua kwa njia ya upasuaji ikiongezeka mwaka 2022, wenye elimu na kipato wanaongoza kwa kutumia njia hiyo, huku wataalamu wa afya na wananchi wakiutaja woga wa uchungu kuwa sababu.

Ripoti ya utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS), wa mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), hivi karibuni inaeleza kuwa kiwango cha wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji kiliongezeka kutoka asilimia saba kwenye utafiti wa mwaka 2015/2016 hadi asilimia 11 utafiti wa mwaka 2022.

Hii ina maana mwanamke mmoja kati ya tisa anajifungua kwa upasuaji ikilinganishwa na mmoja kati ya 14 kwa miaka mitano iliyopita kuanzia 2022.

Ufafanuzi unaonyesha ni mwanamke mmoja pekee kati ya 25 asiye na elimu kubwa na waishio katika kipato cha chini, ndio wanatumia njia ya upasuaji katika kujifungua ikilinganishwa na mmoja kati ya watano ya wanawake wenye elimu na mmoja kati ya wanne ya wenye kipato fulani.

Ripoti hiyo pia inaeleza, kiwango cha wanawake kujifungua kwa njia ya upasuaji ni kikubwa zaidi katika hospitali binafsi kwa asilimia 30, kikifuatiwa na hospitali za dini kwa asilimia 28, huku vituo vya kutolea huduma vya umma vikiwa na asilimia 12.

Mkoa wa Njombe unaongoza kwa asilimia 33 ya wanawake wanaojifungua wanaotumia upasuaji, Kilimanjaro ina asilimia 30 na Dar es Salaam ikiwa na asilimia 26.

Mkoa wa Simiyu ambao pia unaongoza kwa wanawake wake kuwa na uwezo wa kupata watoto wengi nchini, lakini ni asilimia mbili pekee hujifungua kwa njia hiyo.

Akizungumzia suala hilo, Daktari wa wanawake, Isaya Mhando alisema ni vyema ukafanyika utafiti mwingine ili kujua sababu zilizofanya watu hao kujifungua kwa upasuaji ili iwe rahisi kushughulikia kiini cha tatizo.

Hiyo ni kutokana na kile alichoeleza, upasuaji hufanywa ikiwa kuna visababishi mbalimbali, ikiwemo mtoto kutokaa vizuri au kuwa mkubwa, jambo ambalo linaweka ugumu kujifungua kwa kawaida.

“Lakini kuna wengine ni woga tu wanaamua kujifungua kwa upasuaji, hivyo ni vyema kuangalia kwa kina ili tujue sababu ni nini na hili litajulikana kupitia utafiti mwingine,” alisema Dk Mhando.

Alisema hilo litawezekana kupitia kuangalia takwimu za wanawake waliojifungua kwa njia ya upasuaji katika vituo mbalimbali kupitia sababu zilizotolewa na madaktari waliowazalisha.

Kwa upande wa wanawake waliosoma walisema huenda ikawa inachangiwa na utashi wa wao kujua vitu kutokana na kusoma.

Baadhi ya wanawake wamezungumzia suala hilo wakisema wapo wanaoamini kujifungua kawaida kunaharibu maumbile yao.

"Mimi nina ndugu yangu huwa anaomba mwenyewe kufanyiwa upasuaji kwa sababu anasema hawezi hekaheka, pia huwa anataka watoto wake wazaliwe siku anazohitaji yeye, hivyo kutokana na kuwa na haki ya kuchagua njia ya kujifungulia huwa anafanikiwa,” alisema Rahel Mzamilu, mkazi wa Gongo la Mboto.

Neema Swai, mkazi wa Gongo la Mboto pia alisema vijana wengi wa sasa wamekuwa wakikimbilia upasuaji wakiona kuwa ni njia rahisi ambayo inaweza kuwafanya waendelee kubaki katika mwonekano wautakao.

"Nahisi kwa sababu pia wanasoma vitu vingi mtandaoni, baadhi pia wakisikia habari za mtu kuumwa uchungu siku mbili au siku nzima wanaogopa, wengine wakiambiwa unaweza kuchanika wanaogopa hivyo wanajiwahi," alisema Neema.

Maneno yao yanaungwa mkono na Said Mpauka, mkazi wa Ilala jijini hapa, ambaye alieleza woga walionao wanawake wa sasa ndio unaowafanya wakimbie njia za uzazi za kawaida.

Alitoa angalizo kuwa ni vyema ikatolewa elimu zaidi kwa wanawake wajawazito ili wajue faida na hasara za kujifungua kwa njia zote mbili.

"Tuwaelimishe, tuwaondoe hofu na kuwaambia kuwa njia ya kawaida haina madhara katika kujifungua na wapewe mifano hai ya wanawake waliojifungua kawaida ikiwezekana mara nyingi na wako salama," alisema.

Alisema pia ni vyema kuwaambia ukweli kuwa kujifungua kawaida kunawapa nafasi ya kuwa na watoto wengi zaidi kuliko kwa njia ya upasuaji.

Akitoa maoni yake kuhusu hilo, Daktari wa kinamama, Cyrill Massawe alisema upasuaji kwa mtu asiyekuwa na tatizo lolote si jambo jema, lakini kwa sababu watu wanaona ni haki yao kuwa na chaguo la njia ya kujifungua hivyo hupewa kile wanachohitaji.

Alisema upasuaji unatakiwa kufanyika ikiwa njia ya kawaida imeshindikana na hatua hiyo hufikiwa ili kumuokoa mama au mtoto au wote wawili, lakini kwa wasiokuwa na tatizo ni vyema wakatumia njia za kawaida.

Alisema wanawake ambao hawana elimu inaweza kuwa rahisi kufuata ushauri wa daktari, tofauti na wale waliosoma na wenye fedha.

Wenye elimu pia wanajisomea vitu vingi mtandaoni, lakini wanashindwa kuvichanganua vizuri kwani vinahitaji muda zaidi wa kuelimishana na daktari au mkunga, tofauti na wasiopata huo muda wa kuelimishwa.

Shirikila la Afya Duniani (WHO) linashauri njia ya upasuaji kutumika pale tu inapohitajika, huku likionya kuwa matumizi ya njia hizo bila kuwapo ulazima wa kitabibu huweza kuwaweka wanawake katika hatari ya matatizo ya afya ya muda mrefu au mfupi.

Licha ya kutoweka kiwango kinachohitajika kwa ajili ya wanawake wanaojifungua kwa njia hiyo, lakini utafiti wao wa mwaka 2015 unaonyesha kuwa kiwango cha kujifungua kwa upasuaji kinapokuwa juu ya asilimia 10 hauhesabiwi kama moja ya njia ya kupunguza vifo vya kinamama wakati wa kujifungua na vifo vya watoto wachanga.