Sababu ya kuadhimisha Siku ya Dunia

Muktasari:

  •  Kwa mwaka huu, Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka duniani kote yatakutana jijini Ottawa nchini Canada ili kuendelea kujadili masharti ya Mkataba wa Kimataifa wa Plastiki wa Umoja wa Mataifa ya Siku ya Dunia

Dar es Salaam. Unafahamu kwamba dunia tunayokaa yenye watu zaidi ya bilioni nane hufanyiwa maadhimisho? Acha nikujuze kuwa leo Aprili 22, 2024 ni siku ya kimataifa ya dunia.

Siku hii kwa mara ya kwanza iliadhimishwa Aprili 22, 1970, huku kauli mbiu rasmi kwa mwaka huu wa 2024 ikiwa  ni, "Dunia na Plastiki,” lengo likiwa ni kuonesha msaada kwa ulinzi wa mazingira.

Katika hili, ushiriki wa ulimwengu ulisaidia kuleta masuala ya kimazingira kwenye jukwaa la dunia na kutengeneza njia kwa mikutano na mijadala zaidi ya kimataifa ya mazingira, kama vile Mkutano wa Dunia wa Umoja wa Mataifa wa 1992 huko Rio de Janeiro.

Kwa mwaka huu, Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka duniani kote yatakutana jijini Ottawa nchini Canada ili kuendelea kujadili masharti ya Mkataba wa Kimataifa wa Plastiki wa Umoja wa Mataifa siku hii.

Plastiki zinatajwa kuhatarisha maisha duniani hata kwa upande wa watoto. Ripoti zinatoa muhtasari wa baadhi ya utafiti wa hivi karibuni unaochunguza athari za plastiki kwenye afya ya watoto wachanga na watoto.

Dunia imedhamiria kwenye ahadi ya kukomesha plastiki kwa ajili ya afya ya binadamu na sayari, na kudai kupunguzwa kwa asilimia 60 kwa utengenezaji wa plastiki zote ifikapo 2040.

Waandaaji wa siku hii adhimu wanasema ni ya ukumbusho wa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na uendelevu, wakituhimiza kushikamana pamoja na kuchukua hatua kwa ajili ya utunzaji wa sayari kwaajili ya siku zijazo.

Lengo lake ni kuongeza ufahamu, kuhamasisha mabadiliko na kukuza uhusiano wa kina ikisisitiza katika juhudi za kuilinda dunia hii leo na kwa vizazi vijavyo ili kuleta matokeo yenye maana na kuunda ulimwengu endelevu zaidi.

Pia, siku hii muhimu inaangazia muunganisho wa viumbe hai wote na kubainisha umuhimu wa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa na upotevu wa viumbe hai.

Hata hivyo, kuna Kitabu cha Rachel Carson "Silent Spring" cha mwaka 1962, ambacho kilichukua jukumu katika kuongeza ufahamu wa umma juu ya masuala ya mazingira na athari za uchafuzi wa mazingira kwa viumbe hai na afya ya binadamu.

Ni siku ambayo watu kote ulimwenguni wanakusanyika kudai hatua za kisiasa kwa ulinzi wa mazingira. Kuadhimisha siku hii kunasisitiza wajibu wetu wa pamoja wa kuhakikisha ustawi wa sayari yetu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Jinsi ya kusherehekea

Kwa mwaka huu katika maadhimisho ya siku hii, unapaswa kupunguza matumizi ya plastiki kwa kutumia mifuko inayoweza kutumika tena, chupa, na njia mbadala endelevu za kupunguza taka.

Unashauriwa kupanda miti au bustani hii sio tu inaongeza hali ya ukijani zaidi kwenye mazingira yako, lakini pia inachangia hewa safi. Aidha, unatakiwa kutumia muda mwingi kujifunza kuhusu ulinzi wa mazingira.

Vilevile unapaswa kushiriki kwenye matukio ya kusafisha  mazingira ikiwa ni njia moja wapo ya kupunguza uchafuzi wa mazingira na kulinda viumbe vya baharini.