Sababu za makinikia kutosafirishwa nje ya Tanzania

Muktasari:

  • Katika jitihada za kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali zilizopo nchini hasa madini, Serikali iliunda kamati mbili kuchunguza biashara hiyo na zikatoa ripoti Mei na Juni 2017 zilizobainisha changamoto kadhaa zilizopo.

  

Katika jitihada za kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali zilizopo nchini hasa madini, Serikali iliunda kamati mbili kuchunguza biashara hiyo na zikatoa ripoti Mei na Juni 2017 zilizobainisha changamoto kadhaa zilizopo.

Ripoti ya kamati ya pili iliyoongozwa na Profesa Nehemiah Osoro kuchunguza masuala ya kiuchumi na kisheria ilieza masuala kadhaa yanayofanywa kwenye makinikia yaliyokuwa yanasafirishwa na kampuni ya Acacia Mining inayomiliki migodi ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi. Kwa sasa Acacia inaitwa Barrick.

Ripoti ya Profesa Osoro ilisema uuzaji wa makinikia ulikuwa ukifanyika kwa udanyanyifu hasa na kampuni ya Bulyanhulu Gold Mines Limited na Pangea Minerals Limited hivyo kuipotezea Tanzania mabilioni ya shilingi.

Sababu za makinikia kutosafirishwa nje ya Tanzania

“Jumla ya thamani ya madini katika makontena 61,320 yaliyosafirishwa kati ya mwaka 1998 hadi 2017 ni wastani wa kati ya Sh183.597 trilioni na Sh380.499 trilioni. Serikali imepoteza Sh68.59 trilioni katika kipindi hicho. Robo ya fedha hizo zingetosha kujenga reli ya standard gauge kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza,” alisema Profesa Osoro alipowasilisha ripoti yake kwa Rais John Magufuli.

Licha ya upotevu wa mapato kwa Serikali ambayo ripoti hiyo inasema yanafika Sh108.46 trilioni kwa kipindi chote cha usafirishaji, kwenye mapendekezo yake, kamati ilipendekeza Serikali iendelee kuzuia usafirishaji wa makinikia mpaka kampuni za madini zitakapolipa kodi, mrahaba na tozo zote stahiki kwa mujibu wa sheria.

Vilevile, Profesa Osoro alishauri: “Serikali ianzishe utaratibu utakowezesha ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji makinikia ili kuondoa upotevu wa mapato na kutengeneza ajira kwa Watanzania.”

Kamati hiyo pia ilipendekeza Serikali ipime kiasi cha metali (madini) zote zilizomo kwenye makinikia ili kujua thamani halisi ya mrahaba unaopaswa kulipwa na kampuni inayosafirisha makinikia.

Miaka mitano baada ya mapendekezo ya kamati ya Profesa Osoro kampuni ya Barrick inasema imeachana na usafirishaji wa makinikia kwani sasa hivi inakusanya kiasi kikubwa cha dhahabu hivyo kutokuwa na sababu ya kusafirisha makinikia.

Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow anasema kwa sasa wanazalisha dhahabu kwa asilimia 94 kutoka kwenye makinikia na asilimia tatu ni shaba ambayo ni ndogo isiyoweza kuzidi gharama za kuyasafirisha.

“Kwa sasa tunayo teknolojia inayotuwezesha kupata dhahabu nyingi zaidi. Madini mengine yaliyomo kwenye makinikia yanahitaji kuongezewa thamani tofauti na dhahabu lakini, kiwango chake sio kikubwa kiasi hicho,” anasema Bristow.

Kwenye ripoti ya kamati hiyo, ilipendekezwa Serikali iwe na hisa kwenye kampuni zote za uchimbaji madini nchini na mwaka Oktoba 2019 makubali na Barrick yaliwezesha kuundwa kwa Twiga Minerals Corporation Limited ambayo inamilikiwa kwa asilimia 84 na Barrick huku Serikali ya Tanzania ikiwa na asilimia 16.

Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya anasema kampuni ya Twiga yenye wawakilishi kutoka serikalini na kampuni ya Barrick imetafuta namna nzuri, kwa kutumia teknolojia ya kisasa kutoa dhahabu nyingi tofauti na zamani yalipokuwa yanabeba dhahabu, shaba na fedha.

“Kampuni ya Twiga imekuja na teknolojia mpya itakayoondoa kiasi chote cha dhahabu kuacha shaba na fedha. Twiga inataka kuweka legacy katika biashara ya madini, kwa sasa sekta hiii inachangia asilimia 6.7 kwenye pato la Taifa lakini mpaka mwaka 2025 tunataka ifike asilimia 10,” anasema Profesa Manya.

Wadau wanena

Menaja mkazi wa Natural Resource Governance Institute (NRGI), Silas Olan’g anasema siku zote teknolojia huboresha mbinu za uzalishaji na kumaliza tatizo lililokuwepo hivyo kama Barrick wameipata haukna haja ya kusafirisha makinikia.

Hata hivyo, anasema kwa siku za hizi karibuni kumekuwa na usiri mkubwa kwenye mkataba wa Serikali na kampuni hiyo tofauti na ilivyokuwa mwaka 2017 hivyo wadau wengi hawajui kinachoendelea.

“Katika taarifa walizowahi kuzitoa huko nyuma, Barrick walisema wameondolewa sharti la kutosafirisha makinikia na makontena yaliyokuwapo bandarini yakaondolewa. Vilevile walisema migogoro inaweza kutatuliwa katika mahakama za nje na wamesamehewa kujenga mtambo wa kuchenjua madini,” anakumbusha Olan’g.

Agnes Paschal anasema kamati ya uchunguzi ilifanya kazi nzuri ya kufichua mambo mengi ambayo wengi hawakuwa wanayafahamu lakini utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa ndio hauendi kama ulivyotarajiwa na wengi.

“Kamati ilisema Acacia walikwepa kodi dola 190 bilioni hivyo inatakiwa kuzilipa lakini haikuwa hivyo. Utekelezaji wa pendekezo la kujenga mtambo wa kuchenjua dhahabu ulisubiriwa kwa hamu ila leo tunapewa taarifa nyingine. Walikuwa wapi kuja na hiyo teknolojia tangu mwaka 1998 walipoanza kuchimba madini yetu,” anahoji

Agnes, mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam.

Mdau huyu anakumbusha kuwa kamati ilisema makinikia yale yalikuwa na kiasi kikubwa cha madini tofauti na kilichokuwa kinaelezwa kwenye taarifa Acacia hivyo uchenjuaji nchini ungekuwa na faida nyingi zaidi ilivyo sasa.

“Vijana wengi zaidi wangepata ajira, masoko ya madini yangechangamka zaidi ya sasa kwani ni wachimbaji wadogo ndio wanayatumia,” anasema Agnes.

Vijiji havitimizi sheria

Kutokana na shughuli inazofanya, kama ilivyo migodi mingine nchini, Bulyanhulu nao unatakiwa kurudisha sehemu ya faida yake kwa wananchi hasa waliopo kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi huo kwa mujibu wa sheria.

Mbunge wa Msalala, Iddi Kassim Iddi anasema wananchi wake wanazo kero kadhaa ambazo mgodi huo ungeweza kuzimaliza ila hakuna kilichofanyika.

“Tunahitaji ukarabati wa barabara japo kwa kiwano cha changarawe ili ipitike mwaka mzima, hat amitaro nayo haiko sawa pamoja na miundombinu ya afya. Sijui mgodi una mpango gani?” aliuliza Iddi kwenye kikao kilichomjumuisha Naibu Waziri wa Madini, profesa Manya na menejimenti ya Twiga.

Hata hivyo, Bistow anasema baadhi ya wajumbe wa kamati ya maendeleo ya jamii wanataka wapewe fedha taslimu tofauti na matakwa ya sheria.

“Tunatoa kipaumbele kutatua kero za maji, afya, elimu na kilimo lakini katika baadhi ya vijiji mfano cha Msalala kilichopo wilayani Nyang’hwale hawatupi suhirikiano. Wao wanataka tuwape fedha taslimu jambo ambalo hatuwezi kulifanya,” anasema Bistow.

Ili kukabili changamoto hiyo, Profesa Manya anasema wizara uitaandaa utaratibu wa kuwaelimisha wananchi ili wajue namna ya kusimamia haki zao kwa kufuata sheria zilizopo.

“Ni kweli sheria haitaki mgodi utoe fedha taslimu bali usaidie kukamilisha miradi itakayowanufaisha wananchi. Tutawaelimisha,” anasema.