Safari ya mauti ya wafanyabiashara wa Mahenge yaanza

Safari ya mauti ya wafanyabiashara wa Mahenge yaanza

Muktasari:

  • Januari 7, 2006: Safari ya mauti ya wafanyabiashara wa Mahenge yaanza.

Simulizi ya kina kesi ya Zombe na askari wenzake 12

Januari 7, 2006: Safari ya mauti ya wafanyabiashara wa Mahenge yaanza.

Ni Jumamosi, Januari 7, 2006 ambapo wafanyabiashara wa madini wawili, Sabinus Chigumbi, maarufu kama Jongo na ndugu yake Ephraim Sabinus Chigumbi wanaondoka Mahenge mkoani Morogoro kwenda Arusha kupitia Dar es Salaam wakitumia gari la Jongo aina ya Toyota Landcruiser Prado.

Hawa walikuwa wakijishughulisha na uchimbaji na uuzaji wa madini aina ya rubi na spinal katika migodi yao iliyopo katika kijiji cha Epanko, Mahenge.

Pamoja nao alikuwamo Protasi Lunkombe. Huyu alikuwa mdogo wake Mathias Lunkombe (mfanyabiashara mwenza wa kina Jongo). Baadaye Protasi, ambaye pia ni jirani yao akina Jongo, akageuka kuwa shahidi wa Serikali katika kesi ya mauaji ya wenzake.

Pia alikuwamo mjomba wao kina Jongo, Emmanuel Ekonga, ambaye ndiye alikuwa dereva wa gari walilotumia. Pia walikuwamo mabinti wawili wa Jongo, Theobister na Bernadetta.

Lengo la safari hiyo lilikuwa ni kwenda kuuza madini yao na pia kuwapeleka shuleni watoto hao, ambao walikuwa wanasoma katika Shule ya Sekondari ya Mukidoma. Madini waliyobeba yalikadiriwa kuwa na thamani ya kati ya Sh Sh150 na 200 milioni.

Wafanyabiashara hawa waliingia Dar es Salaam na kufikia katika hoteli ya Bondeni iliyoko eneo la Magomeni; karibu kabisa na eneo la Jangwani. Hapa waliweka makazi yao kwa muda. Mjomba wao akina Jongo, Ekonga (dereva) aliamua kwenda nyumbani kwake.


Watua Arusha

Siku iliyofuata (Januari 8, 2016) wafanyabishara hawa waliondoka kwenda Arusha wakiwa na furaha, amani na matumaini makubwa ya kuweka kibindoni mamilioni ya shilingi baada ya kuuza madini yao.

Safari ilianza vizuri na walipofika Arusha walianza kwa kuwapeleka watoto wao shule ya Sekondari Mukidoma iliyopo eneo la User River kisha wao wakapanga katika hoteli ya Manu.

Kesho yake, Januari 9, walifanya shughuli za kuzungumza na wateja na kufanikiwa kuuza sehemu ya madini yao. Waliuza madini kidogo tu ya Sh18 milioni, lakini wakalipwa Sh8 milioni taslimu baada ya kukubaliana na mnunuzi kuwa angewatumia Sh10 milioni iliyobaki kwenye akaunti ya Jongo. Kisha waliuza madini mengine kidogo sana ya Sh1.5 milioni.


Wanarudi tena Dar

Baada ya kufanya biashara hiyo kidogo huko Arusha, wafanyabiashara hao walirudi tena Dar es Salaam Januari 12, 2006 na kufikia katika hoteli ya Bondeni.

Wakati akina Jongo wakirudi Dar es Salaam kutoka Arusha, Mathias Lunkombe na mwenzake ambaye wanashirikiana katika leseni ya uchimbaji madini, Venance Mchami, waliondoka Mahenge kuja Dar es Salaam kwa lengo la kununua vifaa vya kurahisisha uchimbaji. Basi la abiria walilokuwa wakisafiria liliharibika hivyo wakalazimika kulala Morogoro. Kesho yake, Januari 13 ndipo wakaingia Dar es Salaam.

Mchami alikwenda nyumbani kwake na Lunkombe alielekea Bondeni Hotel kwani, naye hupenda kupanga katika hoteli hiyo anapokuwa Dar es Salaam. Walikubaliana kukutana siku iliyofuata.

Siku hiyo hiyo, Ekonga (dereva wa akina Jongo) alilipeleka gari lao---Land Cruiser Prado katika gereji ya Yamungu Mengi iliyopo eneo la Ilala Bungoni kwa matengenezo.

Alipelekwa katika gereji hiyo na Vasco Kamandu, ambaye ni dereva wa daladala linalomilikiwa na Jongo. Kamundu alikuwa anafahamiana na fundi magari, Rajabu Saidi. Hata hivyo, matengenezo hayakukamilika siku hiyo. Waliondoka na kuliacha gari lao gereji.

Kina Jongo waliitumia siku hiyo kununua mahitaji yao kama vile simu na vipuli vya gari.


Januari 14, 2006: Giza la mauti latanda

Asubuhi ya Januari 14, Protasi aliagana na wenzake na kwenda Morogoro kumsalimia dada yake baada ya kupata taarifa kuwa alikuwa mgonjwa.

Mchami na Lunkombe walikutana kama walivyokubaliana na kuelekea mjini katika maduka mbalimbali kuangalia na kununua vifaa vya shughuli zao za uchimbaji madini. Baada ya kukamilisha kazi hiyo, waliachana na kukubaliana siku inayofuata.

Wakati huo biashara ya madini ilizidi kuwaendea vizuri akina Jongo. Walifanikiwa kuuza madini mengine ya Sh15 milioni na kuendelea na mizunguko yao mingine.

Saa tatu asubuhi walifika katika gereji ya Yamungu Mengi kukagua gari lao lililokuwa matengenezoni wakitumia gari dogo aina ya Toyota Chasser lenye namba za usajili T 617 AAS lililokuwa na rangi ya kijivu.

Gari hili lilikuwa teksi ya Ndugu Juma, mkazi wa Manzese. Ni dereva ambaye akina Jongo walipenda kumtumia katika shughuli zao kila mara wawapo Dar es Salaam.

Huko gereji waliwakuta Ekonga na Vasco tayari wameshafika kuandelea na matengenezo ya gari.

Jongo alimtuma mdogo wake Vasco kwenda mjini kununua taa. Anaporudi alikuja na taarifa mbaya; kwamba kulikuwa na ujambazi uliotokea mjini. Wakiwa wamepumzika, akina Jongo walichangia taarifa hiyo kila mmoja kwa maoni yake.

“Kwa sasa hali ni mbaya, mtu ukiwa na pesa ni lazima kuchukua tahadhari sana,” alisikika Jongo akisema bila kujua uvuli wa mauti ulikuwa umetanda juu yake. Mazungumzo yalivyoendelea, Jongo alihitaji soda na hapo yule fundi wao, Said, alimwelekeza baa ya jirani na maarufu, Bonga baa.

Baadaye, yapata saa saba mchana, Jongo na wenzake walikwenda kupata chakula katika mgahawa wa Yamungu Mengi, kisha wakarudi gereji.

Upande mwingine Lunkombe alimpigia simu Mchami akimjulisha kuwa amekutana na ndugu zake ambao wamerudi kutoka Arusha na kwamba, ametoka nao kuburudika huku akimwahidi kukutana naye kesho yake asubuhi.

Ilipofika saa 10 jioni jamaa hawa walirudi tena Bonga baa na wakiwa hapo walipigiwa simu na mchimbaji mwenzao kutoka Mahenge, Alex Ngonyani, akiwaomba waende nyumbani kwake eneo la Sinza Palestina ili wampatie mkewe pesa kidogo za matumizi.

Kabla ya kuanza safari ya Sinza, fundi aliwajulisha kuwa matengenezo ya gari lao yalikuwa yamekamilika. Bila kujua yatakayowapata saa chache zijazo, Jongo alimtaka fundi aende kulijaribu gari lao kabla ya kuwakabidhi na kumuaga kuwa walikuwa wakielekea Sinza wakitumia teksi ile ya Juma Ndugu. Unafahamu safari ya Sinza ilianzaje na nini kilitokea? Fuatilia simulizi hii ya kusisimua kesho.