Sakata la Kichuya doa jingine TFF

New Content Item (2)
Sakata la Kichuya doa jingine TFF

Muktasari:

Baada ya kuamuriwa kulipa Sh294,348,662 na Kitengo cha Usululishi cha Migogoro cha Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (Fifa) kwa kukiuka taratibu za usajili wa winga Shiza Kichuya, uongozi wa Simba umesema watajadili adhabu hiyo na kutolea uamuzi.

Dar es Salaam. Baada ya kuamuriwa kulipa Sh294,348,662 na Kitengo cha Usululishi cha Migogoro cha Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (Fifa) kwa kukiuka taratibu za usajili wa winga Shiza Kichuya, uongozi wa Simba umesema watajadili adhabu hiyo na kutolea uamuzi.

Mbali ya kutozwa faini hiyo, Simba pia inakabiliwa na adhabu ya kuzuiwa kusajili wachezaji wapya misimu miwili endapo watashindwa kulipa fedha hizo ndani ya siku 45 kuanzia Novemba 24 mwaka huu na rungu hilo likimwangukia Kichuya, ambaye atafungiwa miezi sita kutocheza kwa ukiukwaji wa usajili.

Simba ilimuuza Kichuya 2019  kwa mkataba wa miaka minne na nusu kwa klabu ya Pharco na mara baada ya mchezaji huyo kuwasili Misri, alikosa nafasi katika klabu hiyo, uongozi wa Pharco uliamua kumpeleka kwa mkopo ENPPI ya nchini humo.
ENPPI ilimtumia Kichuya kwa msimu mmoja na baadaye kumrejesha Pharco kwa mujibu wa makubaliano yao.

Baada ya kichuya kurejea Pharco mwanzoni mwa mwaka huu, hakuweza kupata nafasi na klabu hiyo ilipanga kumpeleka klabu nyingine, jambo ambalo mchezaji huyo alilikataa na kurejea nchini aliposajiliwa na Simba tena bila ya ridhaa ya Pharco.
Akizungumza jana, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda alikiri kupokea barua hiyo na wamepanga kukutana ili kuijadili na baadaye kuitolea uamuzi.
Kaduguda alisema suala hilo ni nyeti kwani lina masuala ya kisheria na watawashirikisha wadau mbalimbali ili kupata uamuzi sahihi.

“Tutajadili suala hili kwenye bodi yetu kwani kufungiwa misimu miwili kwa  kukosa kulipa fedha hizo ni pigo. Kutokana na unyeti wa suala lenyewe, lazima tuwakutanishe wataalamu mbalimbali na kufikia uamuzi,” alisema Kaduguda.
Alisema kama watafikia uamuzi wa kukata rufaa, watafanya hivyo kwa kutumia vigezo ambavyo wataona vitawapa nafasi ya kushinda rufaa yao.

Kaduguda alifafanua kuwa klabu yao itakutana na uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wadau wengine ili kuona sakata hilo linatatuliwa kwa njia iliyo bora zaidi.
Msemaji wa Namungo FC, Kindamba Namlia alikiri kupokea barua hiyo na kusema watatafuta ushauri wa kisheria ili kupata jibu sahihi kwani klabu yao itaadhibiwa kutokana na makosa ya klabu nyingine. “Sisi tumemsajili kama mchezaji huru na kumtumia katika mechi za ligi na mashindano ya kimataifa, hatukuwa na tatizo katika usajili na ndiyo maana tumepata leseni zote,” alisema Kindamba katika mahojiano na kipindi cha michezo cha Redio ya Wasafi, jana.
Alisema kwa vile yeye ndiye anaishughulikia suala la uhamisho wa wachezaji kupitia mtandao (TMS), aliipata barua hiyo ya Fifa.
Katibu mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah alisema sakata hilo linaacha maswali mengi kuliko majibu.
“Ikumbukwe kuwa klabu ya zamani ya Kichuya  ilishatahadharisha kuwa mchezaji huyo asisajiliwe na timu yoyote hadi suala lake litakapoisha na walishapeleka hilo jambo kwenye Kamati ya Usuluhishi ya Fifa.
“Sasa swali  ni je hapa nchini TFF walitumia nyaraka gani kupitisha usajili wa Kichuya kuichezea Simba wakati timu yake ya Misri ilishasema asijajiliwe hadi watakapomalizana naye?” alihoji.
Alisema jambo hilo linafanya waamini kuwa kuna tatizo kubwa kwa mtu anayeshughilikia usajili wa TMS  pale TFF.
Mwenyekiti wa zamani wa BMT, Kanali mstaafu, Iddi Kipingu alisema mambo hayo yanatokea kwa sababu ya baadhi ya watu kutofuata taratibu na wanaosimamia usajili TFF hawako makini.
“Haya mambo ya usajili yana taratibu zake  sasa kama taratibu hizo au miongozo haikufuatwa ndiyo haya majanga yanayotokea.
“Kwa nini watu wanaosimamia masuala ya usajili wasiwe makini? Maana jambo hili linaonyesha kabisa kuwa kuna mtu anayesimamia usajili (ndani ya TFF) hakuwa makini,” alisema Kipingu.