Sakata la kupanda kwa bei za mafuta latinga bungeni, wabunge waanza kujadili

Muktasari:

Sakata la kupanda kwa bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa limetinga bungeni baada ya Mbunge wa Kilindi (CCM), Omary Kigua kutoa hoja Bunge liahirishwe ili wabunge wajadili hoja hiyo iliyozua taharuki kwa wananchi.

Dodoma. Mbunge wa Kilindi (CCM) Omary Kigua ametoa hoja ya kutaka Bunge liahirishwe ili wabunge wajadili suala la kupanda kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Kigua ametoa hoja hiyo leo Alhamis Mei 5, 2022 baada ya kipindi cha kutambulisha wageni bungeni.

“Ukweli usiopingika kuna changamoto ya kupanda kwa haraka kwa petroli na ukipandisha mafuta ya taa umepandisha bei ya kila kitu. Kelele ni mafuta,” amesema.

Amesema wabunge wanawajibu wa kusimamia na kushauri Serikali na kwamba wananchi wamewapa dhamana ya kuwasemea na kukaa kimya watakuwa hatuwatendei haki wananchi.

Amesema anafahamu Serikali ya CCM ni sikivu na anauhakika ina uwezo wa kufanya kazi na hivyo akaomba wabunge wazungumze kuhusu hoja hiyo ili wasikie Serikali inasema nini.

Akijibu Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amesema pamoja na Serikali kuchukua hatua ya kuwaita mawaziri na kutoa maelekezo na hivyo kukubali kujadiliwa na wabunge.

Hoja hiyo imekubaliwa na tayari wabunge wameanza kuijadili.