Mawaziri wakutana kutathmini bei ya mafuta, gharama za maisha
Muktasari:
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ambazo zitapunguza gharama ya maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ambazo zitapunguza gharama ya maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Wazizi Mkuu imesema kuwa, Majaliwa amesema hayo katika kikao kilichofanyika usiku wa kuamkia leo Alhamisi Mei 5, 2022 jijini Dar es Salaam, cha kufanya tathmini ya bei ya mafuta na kuangalia namna gani Serikali inaweza kufanya ili kupunguza athari ya bei ya mafuta na kuleta unafuu wa gharama za maisha kwa Watanzania.
Kikao hicho ambacho kimewahusisha baadhi ya mawaziri wakiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nishati, January Makamba, Makatibu Wakuu, pamoja na watendaji wakuu wa taasisi za EWURA, TPDC na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), kimefanyika siku moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za petroli, dizeli na mafuta ya taa.
Juzi Jumanne Ewura ilitangaza bei mpya za petroli, dizeli na mafuta ya taa ambazo zilianza kutumika jana Jumatano huku bei ya nishati hiyo ikizidi kupanda na kufikia zaidi ya Sh3,000 kwa lita.
Majaliwa amesema "Nawaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na waiamini Serikali yao kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha tunapunguza gharama za maisha kwa wananchi," amesema.
Amesema kikao hicho kimefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameagiza viongozi wa sekta husika wahakikishe wanatafuta suluhisho la kupanda kwa bei ya mafuta hata kama bei hiyo inaendelea kupanda duniani.
"Rais ameona changamoto wanayopitia Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, hivyo kikao hiki ni matokeo ya maagizo yake ya kuhakikisha sisi kama viongozi tunatafuta suluhisho la muda mfupi na la muda mrefu ili kukabiliana na changamoto hii," amesisitiza.
Majaliwa amesema kuwa tayari Wizara ya Nishati imeanza kutafuta njia mbadala za uagizaji wa mafuta pamoja na kupunguza makato mengineyo ili kupunguza bei ya mafuta.
"Serikali inaangalia njia mbadala za uagizaji wa mafuta, kupitia kwa wazabuni wengine kama ambavyo imeshauriwa na wabunge na tayari mchakato huo umeanza, kwa kutathmini maombi 24 ambayo yaliwasilishwa kwa Wizara na sasa wamebaki wazabuni sita ambao wameingia hatua inayofuata.
Inachokifanya Serikali hivi sasa ni kujiridhisha na uwezo wao wa kusambaza mafuta kulingana na mahitaji na taratibu zilizowekwa na Serikali,” imesema taarifa hiyo.