Sakata la magari mpaka wa Malawi kutua kwa Waziri Mkuu

Hali ilivyo katika kituo cha pamoja cha forodha baina ya nchi ya Malawi ya Tanzania eneo la Kasumuru baada ya magari ya shehena za mizigo kuiwa kuingia nchini.

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera anakusudia kumwandikia barua Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuingilia kati suala la mkwamo wa magari zaidi ya 60 yenye shehena za mizigo ya wafanyabishara wa Tanzania na mataifa mbalimbali yaliyozuiwa nchini Malawi.

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera anakusudia kumwandikia barua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuingilia kati suala la mkwamo wa magari zaidi ya 60 yenye shehena za mizigo ya wafanyabishara wa Tanzania na mataifa mbalimbali yaliyozuiwa nchini Malawi.

Akizungumza na Mwananchi leo, June 7, 2023 Homera amesema kuwa amelazimika kufikia hatua baada ya kuwepo kwa changamoto iliyojitokeza ambayo iko nje ya uongozi wa Mkoa na Wilaya.

“Hayo magari yenye shehena za mizigo yamezuiwa katika mji wa Mzuzu, kilometa zaidi ya 100 kutoka nchini Tanzania huku sababu kubwa ikiwa ni mabadiliko ya sheria za nchi hiyo,” amesema Homera.

Ameongeza kuwa: “leo, June 7, 2023 namwandikia barua Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuomba kuingilia kati suala hilo ili magari yote yenye shehena za mizigo ya wafanyabiashara yaweze kuruhusiwa kuingia nchini kupitia kituo cha pamoja cha forodha baina ya nchi ya Malawi na Tanzania,” amesema.

Homera amesema kwa sasa wanasubiri busara za viongozi wakuu wa nchi kuingilia kati ili kunusuru shehena za mizigo ya wafanyabishara ambazo zimekwama nchini humo.

Aidha ameomba wafanyabishara na wananchi kuwa watulivu wakati Serikali inalishughulikiwa suala hilo ambalo baada ya kufanya mazungumzo litashughulikiwa.

Awali June 5, mwaka huu wanafanyabiashara wa Kasumuru wilayani Kyela Mkoani Mbeya walipanga magogo barabara inayoelekea katika kituo cha pamoja cha forodha kushinikiza magari zaidi ya 60 yaliyozuiwa nchini humo kuachiwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa nchi ya Malawi kuyazuia kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja na nusu hali inayosababisha bidhaa za wafanyabishara kuharibika.

Diwani wa Kata ya Njisi eneo la Kasumuru Omary Rashid amesisitiza suala hilo kushughulikiwa mapema ili kusaidia wafanyabishara kunusuru bidhaa zao zilizohifadhiwa kwenye magari kwa kipindi kirefu.

“Tunaiomba Serikali kuharakisha kushughulikua suala hilo kwani linaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii ambayo ilikuwa ikitegea ajira katika mpaka wa Kasumuru baina ya Tanzania na nchi jirani ya Malawi,” amesema.

Kwa upande wa Mfanyabishara Azole Mwakyusa amesema wanasubiri busara za Serikali kuzungumza na Serikali ya Malawi kutatua kero hiyo sambamba na kushirikisha sheria zilizobadilishwa.