Sakata la mama kubadilishiwa mtoto DNA yamaliza utata

Muktasari:

Sakata la aliyebadilishiwa mtoto limechukua sura mpya baada ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuchukua sampuli na kutoa majibu yaliyoonyesha kuwa mtoto wa kike ni wa mlalamikaji kwa zaidi ya asilimia 80.

Dar es Salaam. Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa Salma Mwae, mama aliyelalamika kubadilishiwa mtoto wa kiume na kupewa wa kike na Hospitali ya Temeke, hazina ukweli baada ya majibu ya vipimo vya DNA kutoka.

Taarifa za mama huyo kubadilishiwa mtoto wa kiume na kupewa wa kike, zilisambaa mwanzoni mwa wiki katika mitandao ya kijamii na mumewe, Khalfan Mhina alilalamika kuwa nyaraka za awali zilionyesha mtoto aliyezaliwa ni wa kiume lakini wakapewa wa kike.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Oktoba 5, 2019, Mhina ambaye ni mkazi wa Mtoni Mtongani mashine ya Maji, amesema majibu ya vipimo vya DNA yametoka leo na kuonyesha mtoto ni wao kwa zaidi ya asilimia 80.

Alipoulizwa kuhusu taarifa zaidi za majibu hayo, Ofisa Habari wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Sylvester Omari alisema, “Kama tumeikabidhi hospitali wao ndiyo wanatakiwa kutoa hiyo taarifa, wao ndiyo waliomba sisi tufanye huo uchunguzi hivyo tumeshawakabidhi hiyo ripoti wanatakiwa kusema sisi tumefanya uchunguzi na majibu tumewapa wao,” amesema.

 

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Meshack Shimwela alipoulizwa kuhusu sakata hilo amesema hospitali iliamua kufanya uchunguzi wa DNA kati ya mlalamikaji na mlalamikiwa na kubaini hakuna kosa lililotokea kwa upande wa hospitali.

Amesema chanzo kilianzia kwa mume wa Salma ambaye alidai kuwa mtoto aliyepewa si wake.

“Hakuna tatizo lolote ambalo lilitokea kwa upande wetu, ila chanzo kilianzia kwa mume wake alitaka mtoto wa kiume na hilo ndilo lilileta shida. Kama hospitali tuliamua kufanya vipimo vya DNA ili kujiridhisha na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa mtoto ni wake,” amesema Shimwela.

Awali, Mhina amesema mke wake alijifungua Septemba 23, 2019 saa 5 kamili usiku na kwamba, aliyembadilishia mtoto mke wake alijifungua saa 5 kamili asubuhi ya siku tajwa.

“Kulikuwa na tofauti ya saa 5, mke wangu alijifungua saa 5 usiku lakini baada ya malalamiko hospitali ilifanya uchunguzi na walichomtilia shaka yule mwenye mtoto wa kiume nyaraka yake ilijazwa mke ikafutwa ikaandikwa mume.

 

“Vipimo vya DNA vilichukuliwa Septemba 27, vimekaa pale vilipelekwa Jumanne kwa Mkemia Mkuu baada ya taarifa kutoka ITV na mitandaoni, jana usiku wamefanya kazi na majibu leo yametoka,” amesema Mhina.

Hata hivyo, Mhina anakiri kuwa makosa ni ya hospitali kuchanganya taarifa katika nyaraka.

“Makosa ni ya hospitali vipimo vimepimwa ni kweli mtoto wa kike ni wa kwetu, na nimepokea majibu mbele ya mkuu wa idara ya upelelezi, timu kutoka wilayani na mkuu wa wilaya ya Temeke pia alikuja asubuhi kabla majibu hayajasomwa.”

Hata hivyo Mhina amesisitiza kuwa hospitali lazima imlipe fidia kwa kuwa imeshindwa kuwa makini katika kazi yake kwa makosa ya uandishi wa nyaraka, suala ambalo Dk Shimwela amesema haliwezekani kwa sababu hakuna nyaraka zilizokosewa.