Sakata la walimu wakuu kuadhibiwa kisa wimbo wa Zuchu latua bungeni

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Muktasari:

  • Spika amesema si jambo jema kuwasimamisha watu bila ya kuwasikiliza lakini akataka majibu ya taarifa kuwa waliosimamishwa hawakuwepo shuleni iweje waadhibiwe wao.

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameagiza walimu wakuu waliosimamishwa kutokana na watoto kucheza muziki wa wimbo wa msanii Zuchu uitwao Honey kurudishwa kazini ili wapewe nafasi ya kusikilizwa.

Spika Tulia ameagiza hayo leo Jumatatu Novemba 6, 2023 baada ya kueleza kuwa zipo taarifa kuwa walimu hao wamesimamishwa wakati siku ya tukio hawakuwepo shuleni hapo.

Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda aliagiza kusimamishwa kwa walimu wa wakuu Novemba 2, 2023 baada ya kusambaa kwa video iliyoonyesha walimu na wanafunzi wakicheza wimbo wa Honey ambao unatajwa kuwa na maudhui yasiyokuwa na misingi mizuri kwa wanafunzi.

Leo Spika ametoa nafasi kwa Mbunge wa Viti Maalum, Husna Sekiboko ambaye ametolea maeleo kuhusu video hiyo na hatua zilizochukuliwa.

Sekiboko amesema nyimbo za muziki kupigwa  kwenye taasisi za dini na mashule zinaharibu utamaduni wa Mtanzania na kwamba wimbo uliopigwa Tunduru kwenye Shule ya Msingi na watoto wadogo kucheza ni kosa hivyo kuitaka  Serikali itoe kauli ni nyimbo zipi zinatakiwa kupigwa maeneo hayo na hatua gani zitachukuliwa kwa wahusika.

Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali inalojukumu la kusimamia malezi shuleni na kudhibiti ikiwemo muziki wenye nyimbo zinazochochea ngono, pombe na kadhalika.

Profesa Mkenda amesema siyo kila kitu kinachokubaliwa uraiani kitaruhusiwa na mashuleni ikiwemo muziki, hivyo watakuwa makini kuhakikisha maadili hayavunjwi.

Baada ya kauli hiyo, Spika wa Bunge amemuuliza waziri aseme kuhusu taarifa za kuwasimamisha wakuu wa shule wakati siku ya tukio hawakwepo kama ni sahihi.

“Hatua za kinidhamu zinapande mbili, lazima mtu asikilizwe ndipo hatua zichukuliwe, kwa nini haikuwasikiliza na kama kuna hatua hizo basi tujue kuwa zilifuatwa,” amehoji Spika na kuongeza.

“…Tunazo taarifa kuwa  hawakuwepo shuleni na mamlaka ya nidhamu imechukua hatua wakati hawakuwepo, hivyo kusema kuwa watakati rufaa si sahihi bali warejeshwe ndipo wajieleze lakini siyo kuwasimamisha ndipo kutaka wajieleze siyo sahihi,” ameagiza.

Spika amesema wako mawaziri na wabunge huwa wanacheza muziki na watoto wa shule pindi wakitembelea shule na kwamba anazo video za ushahidi hivyo ni muhimu kwenda mbele zaidi ili kujua miziki gani inachezwa ili waanzie hapa.

Dk Tulia ameagiza kuwa watu wasichanganye imani ya dini na maadili ya Mtanzania  kwani si jambo jema.