Samia aagiza utafiti ongezeko magonjwa ya moyo, saratani
Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi, wageni mbalimbali pamoja na wananchi baada ya kuzindua jengo la tiba mionzi (Radiotherapy Unit) katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), leo Juni 24, 2026 Moshi mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
- Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatato Juni 24, 2026 wakati wa uzinduzi wa jengo la tiba ya mionzi katika Hospitali ya KCMC baada ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Mwenyekiti wa Bodi ya KCMC, Dk Alex Malasusa, kueleza kuwa wagonjwa wengi wa moyo wanaofika hospitalini hapo wanatoka katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini
Moshi. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka watafiti nchini kufanya uchunguzi wa kina kubaini sababu za ongezeko la magonjwa ya moyo na saratani hususan katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 24, 2026 wakati wa uzinduzi wa jengo la tiba ya mionzi katika Hospitali ya KCMC baada ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Mwenyekiti wa Bodi ya KCMC, Dk Alex Malasusa, kueleza kuwa wagonjwa wengi wa moyo wanaofika hospitalini hapo wanatoka katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
"Hapa nataka nizungumze kuongezeka kwa maradhi ya saratani na moyo kwa watoto ndani ya Taifa letu. Zamani tulijua saratani ni za watu wazima, lakini sasa hivi ni watoto wadogo kwa namba kubwa tu, wanapatwa na maradhi hayo," amesema Rais Samia.
Rais Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa, kuashiria uzinduzi wa jengo la tiba mionzi (Radiotherapy Unit) katika Hospitali ya KCMC, Moshi mkoani Kilimanjaro.
"Sasa nielekeze hili ni suala la kuangaliwa kwa kina hasa kwa watafiti wetu, vituo vyetu vya tafiti za afya kwa kushirikiana na waliotuzidi ujuzi duniani, tuzame kutafuta sababu zinazoleta ongezeko la maradhi haya kwa watoto wetu kwa kutoa elimu ya kutosha kwa jamii yetu ili kuepuka yale yote yanayofanya kuleta maradhi haya.
"Hapa nimemsikia Askofu Malasusa akisema kwamba, wenye maradhi ya moyo wanatoka kaskazini na kwamba tukimalizia jengo lile litasaidia wagonjwa kutokwenda JKCI watatibiwa hapa," amesema Rais Samia.
Amesema lengo ni kutaka watafiti waseme sababu ni zipi za maeneo hayo kuleta wagonjwa wengi wa moyo.
Ongezeko la magonjwa ya moyo Kanda ya Kaskazini, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka KCMC zinaonesha kuwa yamekuwa mzigo mkubwa wa afya katika ukanda huo.
Kati ya mwaka 2020 na 2025, wagonjwa 24,585 waliolazwa KCMC walikuwa na magonjwa ya moyo, sawa na asilimia 14.4 ya wagonjwa wote waliolazwa hospitalini hapo.
Aidha, magonjwa ya moyo yalichangia takribani asilimia 18.3 ya vifo vyote vilivyotokea hospitalini.
Hivi karibuni, Profesa Mohamed Janabi amekuwa akisisitiza kuwa Kanda ya Kaskazini inakabiliwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, hususan magonjwa ya moyo akitaja visababishi kuwa ni mtindo wa maisha, ulaji wa nyama choma, nyama zenye mafuta na matumizi ya pombe kupita kiasi.
Akizungumzia sababu za magonjwa ya moyo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo katika Hospitali ya KCMC, Profesa Kajiru Kilonzo ametaja matumizi ya pombe na sigara, mtindo usiofaa wa maisha, shinikizo la damu, ugonjwa wa kisukari pamoja na sababu nyingine nyingi za kiafya na kimazingira.
Kuhusu ongezeko la wagonjwa wa magonjwa ya moyo na saratani Kanda wa Kaskazini, Profesa Kilonzo amesema suala hilo linahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo chake na kuwezesha hatua stahiki za kinga na tiba kuchukuliwa.
"Hatuwezi kusema sababu ni nini za moja kwa moja, lakini linahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina," amesema Profesa Kalonzo.
Kutokana na ongezeko hilo, KCMC imeanza ujenzi wa Kituo Kikubwa cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa kitakachohudumia Kanda ya Kaskazini na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda Dar es Salaam au nje ya nchi.
Huduma za saratani
Aidha, Rais Samia amesema uzinduzi wa huduma za tiba ya mionzi KCMC ni hatua muhimu ya kusogeza huduma za saratani karibu na wananchi wa Kanda ya Kaskazini na maeneo jirani.
Amesema kuwa huduma hiyo itapunguza gharama na usumbufu wa kusafiri kwenda Dar es Salaam au Mwanza kwa ajili ya matibabu hayo.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuboresha huduma za afya nchini kwa kusogeza huduma maalumu kama tiba ya saratani na upasuaji wa moyo karibu na wananchi.
Rais Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mfizikia Tiba, Rehema Ramadhan kuhusu utendaji kazi wa mashine ya kutibu saratani baada ya kuzindua jengo la tiba mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Moshi mkoani Kilimanjaro.
"Uzinduzi wa huduma hii ya tiba mionzi ni hatua muhimu katika kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kanda hii ya kaskazini, kwa kuwepo kwa huduma hii ya tiba mionzi ni faraja kubwa kwa familia nyingi zikizokuwa zikibeba gharama na usumbufu kwa kusafiri kwenda mikoa mingine kufuata huduma ikiwamo Dar es salama na Bugando," amesema Rais Samia.
"Kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani Tanzania pia tunakabiliwa na changamoyo ya ugonjwa wa saratani, huu sio ugonjwa wa mtu au familia moja au kabila fulani ni changamoto inayogusa afya ya kila mmoja wetu, lakini pia inaingia kwenye uchumi na ustawi wa jamii na Taifa kwa jumla.”
Amesema Serikali itaendelea kusogeza huduma karibu na wananchi ili waweze kupata huduma hizo kwa urahisi.
"Tiba za mionzi zimeshakwisha anza kutolewa, na hapa KCMC nimetembelea jengo na kuona hali za wagonjwa, kungekuwa na kituo kimoja cha kutolea huduma wengi wa wagonjwa niliowaona ndani wangeshindwa kuja na kubaki na maradhi yao, watoto ambao wangeshindwa kuhudumia na kukua na kuwa watoto wema wa Taifa hili," amesema.
"Kuanza kwa huduma hii ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo na kusaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaopelekwa Ocean Road na hivyo kuwapunguzia gharama na kurahisisha matibabu kwa wananchi wanaotokea kanda hii ya kaskazini na maeneo ya jirani.”
Akizungumza Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema uwepo wa huduma hiyo KCMC ni hatua kubwa kwa wananchi wa kanda hiyo na maeneo jirani ambao hapo awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Ocean Road jijini Dar es Salaam kwa ajili ya huduma hiyo.
"Kuanzishwa kwa huduma hizi hapa KCMC kutasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda Ocean Road, kupunguza msongamano wa wagonjwa katika taasisi hiyo na pia kupunguza gharama na usumbufu kwa wagonjwa pamoja na familia zao wanapotafuta matibabu nje ya nchi," amesema Mchengerwa.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mkazo katika kuimarisha huduma za matibabu ya saratani nchini kwa kuwekeza katika miundombinu, vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wa afya.
"Kupitia uwekezaji huu, wananchi wataweza kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.Tutaendelea kushirikiana na KCMC kuhakikisha huduma hizi zinaendelea kutolewa kwa ubora na kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
Rais Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo la tiba mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, leo Jumatano Juni 24, 206 Moshi mkoani Kilimanjaro
Akizungumza mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Gileard Masenga amesema uwekezaji ambao umefanywa na hospitali hiyo kwa kushirikiana na Serikali utasaidia wananchi kupata huduma ya mionzi kwa wakati.
Profesa Masenga amesema tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo jumla ya wagonjwa wa saratani 82 wamepatiwa tiba ya mionzi ambao kwa sasa wanaendelea vizuri na matibabu.
"Huu ni uwekezaji mkubwa ambao umefanywa hapa KCMC kwa kushirikiana na serikali yetu. Tunajivunia ushirikiano huu,” amesema.
Amesema hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa wa saratani 1,400 kwa mwaka ambao walikuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma hiyo Ocean Road, jijini Dar es Salam.
"Hospitali ya KCMC tumeendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na kwa wakati. Pia, tumeendelea kutoa huduma bobezi katika hospitali hii," amesema Profesa Masenga.