Samia ataja sababu mgawo wa maji, atoa maagizo

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani amesema  uvamizi wa  vyanzo vya maji, kukata miti na kuchepusha maji kwa ajili ya matumizi ikiwemo kilimo na mifugo ni chanzo cha upungufu wa maji katika maeneo mengi nchini.


Mwanza. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani amesema  uvamizi wa  vyanzo vya maji, kukata miti na kuchepusha maji kwa ajili ya matumizi ikiwemo kilimo na mifugo ni chanzo cha upungufu wa maji katika maeneo mengi nchini.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya Hospitali ya Kanda ya Rufaa Bugando (BMC), Rais Samia amesema  anatambua miji mingi mikubwa inakabiliwa na uhaba wa maji unaosababisha mgawo wa maji na upungufu wa umeme na kutaja sababu hizo.

“Kuna watu wanalima karibu na vyanzo vya maji haya yote mawili yanapelekea vyanzo vya maji kupungua. Yanapungua na hayaendi kule yanapotakiwa yaende."

“Kwa maana hiyo mtiririko katika maeneo  ambayo maji yanachukuliwa yanasafishwa na kupelekwa kwa matumizi ya watu yakiwa maji safi na salama unapungua kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Ametaja sababu ya shida ya maji jijini Dar es Salaam ni kupungua kwa kina cha maji na kusababisha  kuathiri mchakato wa kupeleka maji kwa wananchi.

“Mfano Jiji la Dar es Salaam linatumia mto Ruvu, Ruvu Juu na Ruvu Chini, kima cha maji kinachochukuliwa kwa siku katika Mto Ruvu Chini kimepungua kwa nusu nzima na kufanya  mchakato wa kupeleka maji kwa wanachi kupungua kwa kiasi kikubwa na  ndio maana Dar es Salaam kumekuwa na mgawo mkubwa wa maji,”amesema.

Amesema walipoenda kutazama kwenye mto walikuta watu wamejenga na kuchepusha maji kwa ajili ya kilimo na matumizi mengine hivyo kuyazuia yasiende kwenye mto.

“Hii kuna maana mbili moja kutumika maji kwa kilimo lakini la pili ni uhujumu wa makusudi, kuzuia maji kwenda kutengenezwa na kufanywa maji safi na kwenda kwa wananchi."

"Baada ya kuendeshwa kwa operesheni jana na leo inaendelea pamoja na zoezi la kutoa mchanga kwenye huo mto tunategemea kina kikubwa cha maji kitakwenda kuchakatwa yawe maji safi na Dar es Salaam iendelee kupata maji. Kutakuwa na mgawo wa maji lakini utapunguawa,”amesisitiza.

Amesema ana uhakika hata mito mingine wanayoitegemea kutengeneza maji safi na salama hali ipo hivyo, akidai taarifa zilizopo sasa katika bonde la Ruvu na Ruaha kuna mifugo mingi baada ya watu kukimbia ukame na kupeleka mifugo yao huko.

Rais Samia amewataka wananchi wasiilaumu Serikali wakiwatoa watu kwenye vyanzo vya maji kwa kuwa lengo ni kuhifadhi ikolojia ya maeneo hayo ili kuendelea kupata maji ya kutosha.

Pia, ameagiza wakuu wa mikoa, kamati za ulinzi na usalama na wakuu wa wilaya kuhakikisha wanaweka ulinzi kwenye vyanzo vyote vya msingi vya maji na kuwachukulia hatua  wote wanaochepusha maji.