Samia ateua watatu, avunja bodi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Rais Sarnia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi Watatu huku wawili kati yao amewateua kuwa mabalozi na mmoja kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Dar es Salaam. Rais Sarnia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi Watatu huku wawili kati yao amewateua kuwa mabalozi na mmoja kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Katika mabadiliko hayo pia Rasi Samia na kuvunja bodi amevunja bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Walioteuliwa ni pamoja na Balozi James Gilawa Bwana ambaye sasa atakuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika kusini. Balozi Bwana anachukua nafasi Balozi Meja Jenerali Gaudence Salim Milanzi ambaye amestaafu.

Pia Rais amemteua Balozi Said Hussein Massoro kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, akichukiua nafasi ya Balozi Said Shaib Mussa ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Aidha amemteua Kaimu Abdi Mkeyenge kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, kabla ya uteuzi huu Mkeyenge alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).

Kwa mujibu wa taarifa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus; Mkeyenge anachukua nafasi ya Dk Elirehema Doriye ambaye atapangiwa kazi nyingine na kwamba uteuzi huu unaanza mara moja.

Kwa upande mwingine Rais Samia ametangaza kuivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Bodi hiyo ilikuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhandisi Othuman Sharif Khatib imevunjwa kuanzia Novemba 7, 2023.

Mhandisi Khatib aliteuliwa Septemba 2022 na Rais Samia kushika wadhifa huo akichukua nafasi Dk Jones Kilembe ambaye uteuzi wake teuzi ulitenguliwa.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania, Zuhura Yunus aliyoitoa leo Alhamisi, Novemba 9, 2023 haijaeleza sababu za kuvunjwa kwake.

Zuhura ametoa taarifa hiyo akiwa Marrakesh nchini Morocco ambako Rais Samia amekwenda kushiriki Mkutano wa Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika ulioanza jana Jumatano, Novemba 8, 2023.