Samia kutembelea nchi tatu, kukutana na Papa Francis

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara katika nchi tatu Januari na Februari na katika kipindi hicho anatarajia kupokea ugeni wa viongozi kutoka nchi tatu ambazo ni Poland, Cuba na China.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kitaifa Vatican City, Vatican kufuatia mwaliko wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.

Ziara hiyo atakayofanyika Februari 11 na 12, 2024, itatanguliwa na ile atakyoifanya nchini Indonesia kati ya Januari 24 na 26, mwaka huu na baaaye Februari 13 na 14, mwaka huu nchini Norway.

Katika ziara yake ya Vatican ambayo pia atafanya mazungumzo na kiongozi wa Kanisa Katoliki, duniani, Rais Samia anatarajiwa kuambatana na viongozi watano wa Kanisa Katoliki kutoka Tanzania.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Januari 21, 2024, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Vatican.

Mwaka 2016, aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano, Hayati John Magufuli alimwalika kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, Papa Francis kutembelea Tanzania.

Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiafya, ziara hiyo haikuwezekana na badala yake kwa wakati huu, Rais Samia Suluhu Hassan amekubali mwaliko wa kiongozi huyo wa kufanya ziara Vatican.

Kwa mujibu wa Makamba, katika ziara hiyo ya nchini Vatican mbali na kufanya mazungumzo na Papa Francis, pia atazungumza na Katibu wa Vatican, Pietro Parolin.

Katika ziara hiyo, wanalenga kukuza uhusiano wa kidiplomasia baina ya Vatican na Tanzania ambao ulianza miaka ya 1960 wakati Vatican ilipoanzisha Ubalozi nchini Tanzania.

“Katika hilo, pia nchi hizi zinalenga kukuza ushirikiano katika sekta ya elimu ambapo Kanisa Katoliki limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa kabla na baada ya uhuru kwa kutoa elimu kwa Watanzania wa dini zote,” amesema Makamba.

Kanisa Katoliki linakadiriwa kumiliki zaidi ya shule za chekechea 240, shule za msingi 147, shule za sekondari 245, vyuo vya ufundi 110 na vyuo vikuu vitano.

Kupitia shule na vyuo hivvyo, Kanisa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania zimechangua kuzalisha viongozi na wataalamu mahiri kwenye maeneo mbalimbali.

Kwenye sekta ya afya, Vatican kupitia Kanisa Katoliki imeendelea kutoa huduma bora za afya kwa Watanzania ambapo inakadiriwa hadi sasa kanisa hilo linaendesha takriban taasisi za afya 473 nchini.

“Taasisi hizi zimechangia kuzalisha wataalamu wa afya nchini. Pia, mchango wa kanisa kwenye sekta ya afya umesaidia kuimarisha afya za watu na kupunguza vifo,” amesema Makamba.

Ziara nyingine

Katika ziara ya kitaifa nchini Indonesia itakyofanyika kati ya Januari 24 hadi 26 kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Joko Widodo, mambo mbalimbali yanatajiwa kufanyika ikiwemo mikutano ya kibiashara.

Pia, Rais Samia anakwenda Indonesia ikiwa ni baada ya Rais wa nchi hiyo kutembelea Tanzania, Agosti 2023.

“Ziara hii inalenga kukukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Indonesia kupitia sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, madini, mifugo, uvuvi, uchumi wa buluu, elimu, utalii na ulinzi,” amesema Makamba.

Amesema pia ziara hiyo inalenga kukuza uhusiano wa kidiplomasia. Kupitia ziara hiyo kwa mujibu wa Makamba, hati sita za makubaliano zinatarajiwa kusainiwa ikiwemo ya ile inayohusu kuundwa kwa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC).

Hati nyingine ni ile ya inayohusu uondoaji wa viza kwa wamiliki wa pasipoti za kidiplomasia na huduma na hati ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya nishati.

Makamba amesema pia kutakuwa na hati ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya afya.

“Pia, tutasaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika eneo la umeme kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na PLN. Hati ya makubaliano ya ushirikiano katika shughuli zinazoendana na mafuta na gesi katika biashara ya kuongeza mnyororo wa thamani kati ya Shirika la Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta na Gesi ya Indonesia (Pertamina).

Katika hati nyingine, makubaliano yatahusisha sekta ya madini kati ya shirika la madini nchini (Stamico) na kampuni ya MIND ID.

Ziara ya Norway

Makamba amesema ziara ya Norway ambako Rais Samia atatembelea kwa mwaliko wa Mfalme Herald na Malkia Sonja, itakuwa ya kwanza ya kitaifa ya Tanzania nchini humo tangu mwaka 1976.

Mbali na mazungumzo na Rais wa nchi hiyo, pia atashiriki kongamano la biashara kati ya Tanzania na Norway pamoja na kogamano la nishati la Oslo.

Pia, ziara hiyo inalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Norway kupitia sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, nishati kama mafuta na gesi, elimu na masuala ya kodi na utawala bora.

"Ziara hii inalenga kuimarisha na kukuza sekta ya nishati hususan kutekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini, kushirikiana katika programu za utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi, kukuza sekta za biashara, uwekezaji na utalii,” amesema Makamba.

Ziara za marais nchini

Mbali na Rais Samia kufanya ziara tatu kati ya mwezi huu na ujao, pia anatarajia kupokea ugeni wa Rais wa Poland na viongozi wengine kutoka China na Cuba.

Rais wa Jamhuri ya Poland, Andrzej Duda atafanya ziara nchini Februari 8 na 9, mwaka huu ambapo mbali na mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Samia, ziara hiyo inatarajia kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo katika ulinzi na usalama, nishati na gesi, madini, usafiri, ulinzi wa mitandao, utamaduni na uchumi wa buluu.

Kwa upande wa China, Liu Guozhong ambaye ni Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na mjumbe wa kamati kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti (CPC) ndiye atakayeitembelea Tanzania.

Liu atafanya ziara hiyo Januari 22 na 23 ambapo atafanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko. 

Kutoka Cuba, anayetarajia kuitembelea Tanzania ni Salvador Valdes Mesa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba na anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi kati ya Januari 23 – 25, mwaka huu.

Katika ziara yake, mbali na mazungumzo na Rais Samia, pia atafanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango na Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson.

“Pia, katika ziara hii atakayofanya, atazungumza kwa Dk Husein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,” amesema Makamba.

Pia, kiongozi huyo atamtembelea mjane wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere na atashiriki katika mkutano wa wanachama wa urafiki kati ya Tanzania na Cuba, Watanzania waliosoma Cuba na Taasisi ya PanAfrican Movement pamoja na kutembelea kiwanda kinachozalisha dawa ya Biolarvicide cha Kibaha mkoani Pwani.