Samia kuzindua jengo la tiba ya mionzi KCMC
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akizungumzia ujio wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan mkoani humo ambapo atafanya ziara ya siku moja, ikiwemo kuzindua jengo la tiba ya mionzi hospitali ya KCMC. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 1,500 kwa mwaka litaondoa adha ya mamia ya wagonjwa wa Kanda ya Kaskazini ambao walikuwa wakilazimika kwenda Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam kutafuta huduma hiyo.
Moshi. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua jengo la huduma ya tiba ya mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC, lililogharimu zaidi ya Sh17 bilioni.
Inaelezwa kuwa hatua hiyo itapunguza adha ya wananchi wa Kanda ya Kaskazini ambao husafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma hiyo jijini Dar es Salaam.
Jengo hilo lenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa takribani 1,500 kwa mwaka, linatarajiwa kuzinduliwa Juni 24, 2026, ambapo linatajwa kuwa miongoni mwa miradi muhimu ya kuboresha huduma za tiba ya saratani katika Kanda ya Kaskazini.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewaambia waandishi wa habari leo Jumatatu, Juni 22, 2026 kuwa Rais Samia atafanya ziara ya siku moja mkoani humo, pamoja na shughuli nyingine, atazindua rasmi jengo hilo la tiba ya mionzi.
“Rais anatarajia kufanya ziara ya siku moja mkoani kwetu Juni 24, mwaka huu. Katika ziara hiyo, atazindua jengo la tiba ya mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC,” amesema Babu.
Ameongeza kuwa gharama za mradi huo ni zaidi ya Sh17 bilioni na Serikali imechangia Sh5.5 bilioni ikiwa ni sehemu ya jitihada za kushirikiana na wadau wa maendeleo na taasisi zisizo za kiserikali kuboresha huduma za afya nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC, Profesa Geleard Masenga, amesema kukamilika kwa jengo hilo ni mafanikio makubwa kwa wakazi wa Kanda ya Kaskazini ambao kwa muda mrefu walilazimika kusafiri hadi Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam kupata huduma ya tiba ya mionzi.
Amesema huduma hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa mzigo kwa wagonjwa wa saratani na familia zao, sambamba na kuboresha upatikanaji wa tiba kwa wakati.
“Uwepo wa huduma hii hapa KCMC ni mafanikio makubwa sana. Kwa miaka mingi wagonjwa wetu wamekuwa wakipelekwa Ocean Road kwa ajili ya tiba ya mionzi. Sasa huduma hii italeta ahueni kubwa kwa wagonjwa wa saratani,” amesema Profesa Masenga.
Amebainisha kuwa hospitali hiyo kwa sasa inahudumia idadi kubwa ya wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo ya saratani, ambayo ni miongoni mwa changamoto kubwa za kiafya katika ukanda huo.
Amesema kati ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo, idadi kubwa ni wa magonjwa yasiyoambukiza, huku saratani ikiwa miongoni mwa yanayoongoza kwa kuhitaji huduma maalumu za tiba.
Profesa Masenga amesema asilimia 60 hadi 70 ya wagonjwa wa saratani huhitaji tiba ya mionzi kama sehemu muhimu ya matibabu yao.
Ameongeza kuwa tangu Februari 25, 2026, hospitali hiyo ilipoanza kutoa huduma za tiba ya mionzi, tayari wagonjwa zaidi ya 80 wamepata huduma hiyo, huku kwa sasa wastani wa wagonjwa zaidi ya 30 wakihudumiwa kila siku.
Amesema kwa mwaka, hospitali hiyo inatarajia kuhudumia zaidi ya wagonjwa 1,500 wanaohitaji tiba ya mionzi, hatua inayoonesha ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo katika Kanda ya Kaskazini.