Samia: Lema amerudi hakuna kilichotokea

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wananchi wa Usa River, Arumeru Mkoani Arusha Jumapili Machi 5, 2023 wakati akielekea KIA baada ya Mkutano wa Faragha wa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) bado kiko imara kisiasa na ndiyo maana hata aliporudia mwanasiasa wa Kanda ya Kaskazini, akimaanisha Godbless Lema, hakuna kilichotokea.

Pia, amesema kama nchi iko vizuri katika uchumi, kwenye maendeleo ya jamii na watu ikiwemo maji, umeme, elimu na afya huku ikiendelea kujitahidi kuimarisha miundombinu ya maeneo hayo ya kaskazini ili wananchi wapate huduma zaidi

Samia alitoa kauli hiyo jana wakati akisalimiana na wakazi wa Wilaya ya Arumeru eneo la Usa River, alipokuwa safarini akitoka kufunga mkutano wa mawaziri, naibu waziri, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu jijini Arusha.

Samia alisema kitendo cha mwanasiasa wa kanda hiyo kurudi nchini na hakuna kilichotokea ni ishara kuwa siasa zao ziko vizuri.

“Nadhani hili tendo la juzi la mtu wao wa kanda hii kurudi nchini na hakuna kilichotokea inaonyesha kuwa siasa zetu ziko imara sana.

“Ziko imara sana, Mtanzania yeyote ambaye ni wa chama chochote cha siasa tunachotofautiana ni mawazo tu na fikra, mimi sichukulii upinzani kama maadui, nawachukulia kama watu watakaonionyesha changamoto zilipo, nizitekeleze ili CCM iimarike,” alisema Samia.

Akitoa mfano wa kusikilizana, alisema “mdogo wangu (hakumtaja) aliniambia ‘mama nataka kurudi’m nikamwambia rudi.

“Kasema mama nina kesi, nikamwambia nazifuta, rudi. Amerudi tuimarishe siasa, si ndiyo? Mwanamume ni yule anayejiamini na, mwanamke ni yule anayejiamini, kwahiyo kwenye uwanja wa siasa tunajiamini, tuko vizuri na tutakwenda vizuri,” alisema Rais Samia

Wakati Rais akizungumza hilo alisindikizwa na kelele za shangwe kutoka kwa wananchi waliokuwa wakimsikiliza katika eneo hilo huku baadhi wakiwa wamevalia sare za CCM.

Kuhusu wananchi waliopo ndani ya eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Rais Samia alisema Serikali imekamilisha tathmini ili iweze kuwalipa waliopo ndani ya eneo hilo wakatafute makazi mengine.

Pamoja na kuwa wamevamia lakini Serikali imekubali kulipa fidia ili waachie hilo eneo, tathmini imeshafikishwa serikalini nadhani ni kama Sh11 bilioni, Serikali inakwenda kulipa ili watu hao wakatafute maeneo mengine, ni wavamizi lakini tutawalipa fidia kwa sababu wameshajenga nyumba zao za kuishi pale.

Awali, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba ya Maendeleo na Makazi, Geofrey Pinda alisema wapo baadhi ya wananchi waliopo ndani ya uwanja huo eneo ambalo ni la Serikali alimtaka mbunge wa eneo hilo kuwasilisha maombi maalumu juu ya eneo hilo, kama yapo.

“Niliongea na mbunge na kumueleza kuwa kama kuna maombi maalumu, yanayohusu hilo eneo yawasilishwe kwetu ili tuyachakate kwa sababu bado tunagawagawa ardhi hizi, basi wale wananchi wapishe hilo eneo, tusiiangalie Arusha na Kilimanjaro kwa miaka 10 inayokuja bali 100 ijayo,” alisema Pinda.

Hoja nyingine ambazo ziliibuliwa katika mkutano huo ni uhitaji wa barabara ambapo Mbunge wa Arumeru Mashariki, John Pallangyo alisema kutokana na eneo hilo kuwa na milima mingi, tiba yake ni ujenzi wa barabara za tabaka gumu, kwani bila kufanya hivyo ni sawa na kujaza maji katika gunia.

“Mhesimiwa Rais hapa tulipo tuna ahadi ya ujenzi wa kilomita 5 ya kiwango cha lami, ahadi ambayo ilitolewa na Rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli tunaomba utoe tamko leo,” alisema.

Pia alitaka changamoto ya maji kufanyiwa kazi kwani licha ya fedha kutolewa bado baadhi ya maeneo hayajapata huduma hiyo.