Samia, Sugu walivyoipandisha Hip Hop katika Dream Concert

Muktasari:

  • Kadi ya kielektroniki ya mwaliko ilitoa uhuru kwa waalikwa kuingia ukumbi wa Margquee katika Hoteli ya Serena kushuhudia tamasha la "Dream Concert", kuvaa vazi lolote ili mradi liwe "muafaka".

Kadi ya kielektroniki ya mwaliko ilitoa uhuru kwa waalikwa kuingia ukumbi wa Margquee katika Hoteli ya Serena kushuhudia tamasha la "Dream Concert", kuvaa vazi lolote ili mradi liwe "muafaka".

Lakini ni kama waalikwa walikubaliana kuvaa suti au majaketi ya rangi nyeusi na shingoni kupachika tai, mithili ya waalikwa wa hafla za hadhi kubwa za mashirika au serikali.

Muonekano huo ni tofauti na utamaduni wa mavazi wa matamasha ya muziki, hasa wa Hip Hop ambao mashabiki wengi huvalia suruali aina ya jeans, au cadet na fulana kubwa zenye maandishi makubwa.

Lakini Jumanne katika ukumbi wa Marquees, waalikwa waliingia na suti na tai zao kuhudhuria tamasha la Hip Hop, kitu kilichokuwa ishara ya kwanza kwamba usiku huo muziki wa rap ulikuwa unaelekea kuweka alama mpya ya kimtazamo, kimapokeo na kiutamaduni baada ya kuanza kwa kudhaniwa kuwa ni wa kihuni na usiostahili jukwaa la hadhi ya hoteli ya nyota tano kama Serena.

Mr ll au Sugu, mwanamuziki mkongwe wa hip hop nchini na ambaye jina lake halisi ni Joseph Mbilinyi, alikuwa akiadhimisha miaka 30 tangu aingie katika sanaa hiyo mwanzoni mwa miaka ya tisini.

Pia, tofauti na matamasha mengine ya muziki, upangaji wa viti kwa waalikwa ambao walikuwa takriban 300, ulikuwa wa hadhi ya hafla za hadhi ya juu ambazo muziki wake ni wa utulivu na si huo unaoitwa "wa kufokafoka". Waalikwa

walikaa katika meza za watu takriban 10, zikiwa zimepangwa vifaa vyote muhimu; kuanzia glasi za juisi, mvinyo hadi vinywaji vikali pamoja na sahani za chakula.

Hip Hop ilikuwa inaendelea kupanda jukwaa la juu zaidi na Mr ll ama Sugu alikuwa akiongoza mabadiliko hayo kwa kuonyesha historia ya muziki huo nchini huku akienzi wakongwe waliotangulia mbele za haki.

Na zaidi ya yote, kilichoheshimisha zaidi muziki wa Hip Hop usiku huo, kilikuwa ni ushiriki wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye sasa amekuwa kiongozi wa kwanza wa nchi kuhudhuria tamasha la muziki huo akiwa madarakani.

"Leo tunatengeneza historia nyingine kwa muziki wa kizazi kipya na tasnia ya sanaa kwa ujumla kwa uwepo wako hapa Mheshimiwa Rais," alisema Sugu.

"Pamoja na ratiba ngumu na majukumu yako kama rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa upendo mkubwa umeweza kutenga muda wako na uko hapa na sisi katika kuadhimisha miaka 30 ya mimi kufanya kazi ya muziki."

Na baada ya kutumbuiza kibao cha "Haki", Sugu alifungua moyo wake kuonyesha kilichomo.

"Ni heshima kubwa sana kwangu kutumbuiza mbele ya Rais usiku huu," alisema Sugu.

"Wakati nikiwa Marekani, ikifikia hatua kama hii unasema kama nikifa usiku huu, ni sawa kwa sababu nimeshafanya show mbele ya Rais."

Sugu alieleza kuwa safari yao ilikuwa ngumu hadi kufikia hapo walipo na kwamba matatizo bado yapo na hivyo kwa kuwa Rais amefungua mlango kwa wasanii kumpelekea hoja zao, watatumia fursa hiyo vizuri.

Akizungumza katika tamasha hilo, Rais Samia alisema msukumo wa kuhudhuria ulitokana na ukweli kwamba Sugu ni mwanake na hivyo anajisikia fahari mtoto wake anapopata mafanikio.

"Mama kushuhudia mafanikio ya mwana ni fahari na leo nimeshuhudia na najisikia fahari," alisema Samia.

"Lakini sababu ya pili ni kwamba nimevutiwa na wazo la kujiandikia kitabu kinachoitwa 'Muziki na Maisha: From the Street To The Parliament'.

"Si wengi wanaopenda kuandika historia yao, hasa ikiwa haina mwanzo mwema. Lakini nimevutiwa na wazo hilo na uwazi aliokuwa nao, nikasema nakwenda kumsupport."

Alisema pamoja na kwamba alikuwa hajasoma kitabu hicho, anahisi kitakuwa kimejaa simulizi za maisha ya Sugu, visa na miaka ya kuhuzunisha na mafanikio, huku akisema msanii huyo anaangaliwa tofauti na tabia yake halisi.

Joseph Kusaga, mkurugenzi mtendaji wa Clouds Media Group naye alielezea mabadiliko ya mtazamo na hadhi ya muziki wa hip hop pamoja na uzito uliowekwa na Rais Samia katika onyesho hilo.

"Wakati sisi na Mr ll tunahangaika kujenga kilichojengwa leo, ilikuwa inaonekana ni uhuni wa ajabu kabisa kabisa. Yaani, isingekuwa rahisi kumwambia baba au mama leo aje kwenye show amevaa tai, amevaa suti; impossible (haiwezekani)," alisema Joseph Kusaga ambaye

kampuni yake pia imefanya kazi kubwa ya kuinua vipaji vya muziki vya vijana.

"Uzuri wa Mr ll ni uthubutu. Yaani mimi nimekaa na Mr ll miaka 30 yote hii, meli imeenda juu imeshuka chini, lakini amethubutu na alikuwa na vision (maono) na ameenda nayo mpaka amefika hapa. Katika watu ambao wamefungulia dunia wengi, hasa vijana ni Mr ll."

Maneno kama hayo ya kushukuru uwepo wa Rais Samia pia yalisemwa na wasanii na wengine waliohudhuria tamasha hilo.

"Sisi (wasanii wa hip hop) ni watu ambao tunatambulika kwa kujisifu sana kati ya watu wote wanaofanya muziki," alisema MwanaFA baada ya yeye na wasanii wengine kutumbuiza pamoja wimbo wa "Kilimanjaro".

"There is nothing higher than this (Hakuna kikubwa zaidi ya hiki). Kama tumeweza kuwa na rais, a sitting president wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye show ya hip hop, kwenye kuwitness (kushuhudia) historia ya muziki huo, jinsi safari yake nzima hadi hapa tulipofika, hakuna kitu kitatop (kitapanda juu ya) hii tena."

Mabadiliko mengine makubwa ya muziki huo yaliyoonekana usiku wa Dream Concert ni matumizi ya bendi, tofauti na kawaida ya Hip Hop Tanzania na duniani ambako mazoea yalikuwa ni kutumia midundo iliyorekodiwa.

Jumanne wasanii wote waliopata nafasi ya kutumbuiza; Weusi, Lady Jay Dee, AY na MwanaFA

walitumia bendi hiyo ya Sugu.

Na ili kuonyesha anamudu live na kuwajua vilivyo watumbuizaji, Sugu alitumia sehemu ya mwisho ya wimbo wa "Ana Miaka Chini ya 18" kumhamasisha mpiga gitaa la solo achangamshe wimbo kwa madoido na baadaye kwenda kwa mpiga kinanda na kumalizia kwa mpiga drums.

"Niliwaambia jamaa kuwa nakuja na bendi, wakasema 'Sugu unakuja na bendi kwani wewe ni Asha Baraka wa kiume?'" alisema Sugu kw autani mwanzoni mwa wimbo wa "Sugu". Asha Baraka ni mmiliki wa bendi ya African Stars, maarufu kwa jina la Twanga Pepeta. 

Dream Concert ya Hip hop haikuwa ya burudani pekee, bali pia ilikuwa chembechembe za kuunganisha watu, hasa wanasiasa. Mbali na Rais Samia, waalikwa wengine walikuwa ni pamoja na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, makamu mwenyekiti wa CCM, Abdulrahaman Kinana, katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika, mawaziri, watendaji wakuu wa mashirika na taasisi binafsi, mabalozi na watu wengine maarufu.

Akijibu swali kama mkusanyiko wa watu tofauti katika tamasha la Dream ni mwanzo mzuri wa safari ya kisiasa, Mbowe alisema "siwezi kusema ni mwanzo mzuri kwa sababu tumeshakutana na tutaendelea kukutana na tutaendelea kutoa taarifa hatua kwa hatua kwa namna ambavyo tunaendelea kukutana".

"Kwa hiyo ni sehemu ya safari na si mwanzo wa safari na tumeonyesha kuwa we are serious (tuko makini) katika hili, Ni matumaini yangu kwamba Watanzania wenye kupenda mshikamano katika taifa letu wataona umuhimu wa kumaliza tofauti zetu na kuijenga Tanzania kuwa ya ushirikiano na bora zaidi," alisema Mbowe baada ya tamasha hilo.

Pamoja na nyimbo hizo mbili za "Ana Miaka Chini ya 18" na "Haki", Sugu pia aliwarejesha

waalikwa enzi zake alipotumbuiza wimbo wa "Sugu" ambao alishirikiana na

Msanii pekee aliyetumbuiza usiku huo ambaye aina ya muziki wake si Hip Hop alikuwa Lady Jay Dee, ambaye pia ni mmoja wa wasanii walioanza muziki miaka ya tisini.

Hata hivyo, Jay Dee alishiriki kuitikia nyimbo kadhaa za wasanii wa Hip Hop kama Weusi, AY na

Sugu.

Mabadiliko hayo ya Hip Hop yanaendelea kutikisa burudani karibu dunia nzima.

Mapema mwaka huu, kwa mara ya kwanza wasanii wakongwe wa Hip Hop, walitumbuiza wakati wa mapumziko ya mechi ya fainali ya ligi ya mpira wa miguu aina ya Kimarekani (NFL), maarufu kama Super Bowl.

Snoop Dogg, Eminem, Dr Dre, Kendrick Lamar na mwimbaji wa R&B, May J. Blige walitumbuiza na kuandika historia ya mabadiliko ya hadhi ya muziki huo ulioonekana kuwa ni wa gheto.

Na kama ilivyokuwa Serena, onyesho la magwiji hao wa Marekani lilijumuisha upigaji wa ala na muziki uliorekodiwa.Pia matamasha kama la tuzo za filamu la Oscar limeshatambua muziki huo kwa kuanza kutuza wasanii wa Hip Hop ambao nyimbo zao zimetumika katika fulamu, likianza na Eminem na kibao chake cha "Loose Yourself From 8 Mile" mwaka 2003, wakati tamasha la Grammy lilianza kutuza wasanii hao mwaka 2000.