Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Saratani ya damu, tishio watoto mikoa ya kaskazini

Wadau walioshiriki katika kampeni ya kujenga uelewa juu ya saratani za watoto, wakishiriki  kuchora picha pamoja  na watoto wanaopatiwa matibabu ya saratani kituo cha saratani  KCMC..

Muktasari:

  • Saratani ya damu imetajwa kuwa miongoni mwa maradhi yanayoathiri kwa kiwango kikubwa watoto, katika mikoa ya kaskazini.



Moshi. Saratani ya damu imetajwa kuwa miongoni mwa maradhi yanayoathiri kwa kiwango kikubwa watoto, katika mikoa ya kaskazini.

Kutokana na hali hiyo, wadau wa afya wametakiwa kuwekeza nguvu zaidi katika kufanya tafiti ili kubaini chanzo cha tatizo hilo.

Hayo yameelezwa jana Septemba 23, 2022 na Daktari bingwa na mbobezi wa saratani za watoto, Hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Ester Majaliwa wakati wa kampeni ya kuhamasisha na kujenga uelewa juu ya saratani za watoto iliyofanyika hospitalini hapo.

Alisema kwa mwaka 2020/2021, KCMC imefanikiwa kutibu watoto zaidi ya 200 wenye saratani mbalimbali ambapo kati yao asilimia 60 ya watoto  wamemaliza matibabu na kupona kabisa.

Alisema kati ya watoto 200 waliopata matibabu, takribani watoto 40 waligundulika kuwa na saratani ya damu idadi ambayo ni kubwa na wote walitokea katika mikoa ya kaskazini mwa Tanzania.

Akielezea chanzo cha saratani kwa watoto, Dk Majaliwa alisema saratani ya watoto inahusisha mfumo wa taarifa uliopo kwenye vinasaba vya binadamu jambo ambalo linasababisha ugumu katika kujikinga ama kuzuia saratani za watoto zisitokee.

"Saratani za watoto ni tofauti na saratani za wakubwa, ambazo huchagizwa na mfumo wa maisha ya kila siku, kwa watoto nyingi zinahusisha vinasaba (Genetics) na hii inasababisha ugumu katika kuzuia saratani kwa watoto zisitokee," alisema Majaliwa.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji KCMC, Profesa Gileard Masenga alisema saratani za watoto zipo na zinatibika ambapo kwa sasa hospitali hiyo inatoa huduma  ya saratani kwa watoto bure.

"Tiba za saratani kwa watoto ni bure, mtoto anakuja anatibiwa, dawa anapewa, chakula anapata, vipimo anafanyiwa na anapatiwa elimu bila malipo, hivyo wazazi wasiogope kuwaleta watoto ili kuwatibu watoto hawa mapema," amesema Masenga

Mmoja wa wadau wa kukabiliana na saratani za watoto, mwakilishi wa Lions Club of Kibo, Sarah Mandara alisema wakati sasa umefika wa jamii kuungana katika kukabiliana na saratani za watoto kwa kuwapeleka watoto mapema kwenye vituo ili waweze kugundulika mapema na kuanza kupatiwa matibabu.

Akizungumza mzazi mwenye mtoto anayeendelea kupatiwa matibabu  hospitalini hapo, Yustina Kahe aliwataka wazazi kulichukulia suala la saratani ya watoto kwa uzito na kuwapeleka kwenye vituo vya kupatiwa huduma mapema

"Nawaambia wazazi wenzangu msitegemee dawa za kienyeji, madaktari wa kienyeji ni waongo, mimi nimekuja na mtoto wangu alikua na saratani ya damu na macho na sasa anaendelea kupatiwa matibabu na ninaona anaimarika tofauti na nilipokua natumia dawa za kienyeji," alisema