Sasa ukilipia vifurushi WhatsApp, Instagram utapata vipengele hivi vya siri
Muktasari:
- Kifurushi cha Meta One Premium cha dola 19.99 kwa mwezi sawa na Sh52,473 kitawapa watumiaji huduma ya "Thinking Mode", inayoruhusu AI kufanya uchambuzi wa kina katika masuala ya kihesabu, kisayansi na kisheria.
Dar es Salaam. Kampuni ya teknolojia ya Meta imeanzisha mfumo mpya wa vifurushi vya kulipia kwa watumiaji wa mitandao yake ya kijamii ya Facebook, Instagram na WhatsApp.
Hatua inayotajwa kuwa mabadiliko makubwa zaidi kuwahi kufanywa tangu kuanzishwa kwa majukwaa hayo.
Kwa miaka mingi, Meta ilitegemea mapato ya matangazo huku huduma zake zikitolewa bure kwa watumiaji. Hata hivyo, ongezeko la gharama za kuendesha mifumo ya akili unde (AI) na ushindani unaoongezeka katika sekta ya teknolojia vimeifanya kampuni hiyo kuanzisha huduma za ziada zinazolipiwa kila mwezi.
Ukilipia Instagram
Chini ya mfumo huo mpya, watumiaji wa Instagram watakaolipia dola 3.99 za Marekani (sawa na Sh10,473) kwa mwezi wataona ni mara ngapi watu wamerudia kutazama ‘story’ zao (rewatch counts).
Pia, uwezo wa kusoma au kutazama maudhui ya wengine bila kuonekana kwenye orodha ya waliotazama.
Vilevile kubadilisha mwonekano wa wasifu wao (profile) kwa kutumia aina tofauti za maandishi na alama za programu, yaani kuwa na uwezo wa kubadili miundo ya herufi (fonts) kwenye wasifu wako na kubadili mwonekano wa alama ya programu (custom app icon).
Na utaweza kuposti kwa siri kupitia kuweka picha/video moja kwa moja kwenye akaunti yako (profile) bila chapisho hilo kwenda kwenye ‘feeds’ za wafuasi wako.
Kwa upande wa WhatsApp, watumiaji watakaolipa dola 2.99 sawa na Sh7848.74 watakuwa na uwezo wa kubadili rangi za programu (themes), kuweka milio maalumu ya simu kwa kila mtu (custom ringtones).
Pia, kuongeza idadi ya mazungumzo yanayobandikwa juu ya ukurasa (pinned chats) na kupata sticker maalumu zisizopatikana kwa watumiaji wa kawaida.
Facebook nayo itatoa huduma zinazofanana na Instagram, ikiwapa watumiaji uhuru mkubwa zaidi wa kudhibiti mwonekano wa akaunti na namna maudhui yao yanavyowasilishwa.
Mbali na vifurushi hivyo vya kawaida, Meta imeanzisha mfumo unaoitwa ‘Meta One’ unaolenga watumiaji wanaohitaji uwezo mkubwa wa AI.
Kupitia kifurushi cha Meta One Plus cha dola 7.99 kwa mwezi sawa na Sh20,973 watumiaji watapata huduma zote za Plus pamoja na uwezo wa kutengeneza picha na video za kisasa kwa kutumia AI.
Kifurushi cha juu zaidi, Meta One Premium cha dola 19.99 kwa mwezi sawa na Sh52,473 kitawapa watumiaji huduma ya ‘Thinking Mode’, inayoruhusu AI kufanya uchambuzi wa kina katika masuala ya kihesabu, kisayansi na kisheria. Mfumo huo pia umetengenezwa kusaidia watumiaji wa miwani ya kisasa ya Meta inayotumia AI.
Kwa wafanyabiashara na watengeneza maudhui, Meta imeanzisha vifurushi vinavyolenga kuongeza mwonekano na usalama wa akaunti. Miongoni mwa faida zake ni alama ya uthibitisho wa akaunti, ulinzi dhidi ya akaunti feki, uwezo wa kuweka viunganishi vingi kwenye wasifu, pamoja na huduma ya moja kwa moja kutoka kwa wafanyakazi wa Meta pindi akaunti inapopata matatizo.
Kifurushi cha juu kwa kundi hilo kitawawezesha watengeneza maudhui kusukumwa zaidi na mifumo ya mapendekezo ya Facebook na Instagram, kupata taarifa za haraka kuhusu matumizi ya maudhui yao na kusaidiwa kukuza idadi ya wafuasi.
Licha ya maboresho hayo, Meta imesisitiza kuwa huduma za kawaida za sasa za Facebook, Instagram na WhatsApp zitaendelea kutolewa bure kwa watumiaji wote, huku vifurushi vipya vikibaki kuwa chaguo la hiari kwa wanaotaka vipengele vya ziada.