Saudi Arabia yatishia kulipiza kisasi kiuchumi

Muktasari:

  • Onyo hilo la Saudi Arabia limekuja siku moja baada ya soko la hisa la nchi hiyo kuporomoka kwa kiwango cha asilimia saba

Riyadh, Saudi Arabia. Saudi Arabia Jumapili ilitishia kulipiza kisasi dhidi ya vikwazo vyoyote vitakavyotangazwa na mataifa mengine dhidi yake vikihusishwa na sakata la kuuawa kwa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi, shirika la habari la serikali la SPA limeripoti.
Kauli hiyo ya Saudi Arabia imekuja muda mfupi baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kusema taifa hilo la kifalme lenye utajiri wa mafuta linastahili kupata adhabu kali ikiwa itabainika linahusika na kutoweka au pengine kuhusika na madai ya kuuawa mwandishi huyo na mkosoaji mkubwa wa serikali.
Onyo hilo la Saudi Arabia limekuja siku moja baada ya soko la hisa la nchi hiyo kuporomoka kwa kiwango cha asilimia saba kwa wakati fulani.
Taarifa hiyo imetolewa wakati wasiwasi kimataifa ukiongezeka kuhusiana na mwandishi huyo aliyetoweka wakati alipozuru ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul zaidi ya wiki moja iliyopita.
Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kwa pamoja zimetoa wito kutaka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusiana na kutoweka kwa Khashoggi, mkosoaji mkubwa wa utawala wa Kifalme chini ya Prince Mohammed bin Salman (MBS), na mkazi wa Marekani.
"Ufalme umethibitisha kwamba ikiwa hatua yoyote itachukuliwa dhidi yake, itajibu vikali,” shirika la SPA lilimnukuu ofisa ambaye hakutajwa jina.
"Ufalme inasisitiza kwamba wanapinga vikali vitisho na majaribio yoyote yenye lengo la kuidhuru kwa kutishia kuiwekea vikwazo vya uchumi au matumizi ya shinikizo la kisiasa,” ofisa huyo aliongeza na akasema uchumi wa Saudi ni “muhimu na una ushawishi” mkubwa kwa uchumi wa dunia.