Saut yakemea kitendo cha mwanafunzi wake kutupa kichanga

Thursday June 23 2022
mtotopic
By Mgongo Kaitira

Mwanza. Zikiwa zimepita siku nne tangu Mwananchi iripoti taarifa ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) Mwanza kunusurika kipigo kutoka kwa wananchi baada ya kujifungua na kutupa mtoto, uongozi wa chuo hicho umekemea kitendo hicho huku ukiwataka wanafunzi wake kuzingatia masomo, maadili na kuepuka makundi hatarishi.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Juni 23,2022 na Ofisi ya Uhusiano SAUT imesema mwanafunzi huyo (Jina limehifadhiwa) anasoma fani ya sheria mwaka wa tatu chuoni hapo.

Pia imesema mwanafunzi huyo anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando chini ya uangalizi wa Maofisa wa Jeshi la Polisi baada kukutwa katika hali mbaya kiafya aliyoipata wakati wa kujifungua.

"Chuo kinasubiri taarifa ya kitabibu kutoka hospitalini na kisha mwongozo wa Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine za kisheria kukamilisha uchunguzi wake,"


Iliongeza; "Tunatoa rai kwa jamii ya wanafunzi kutilia maanani dhumuni la msingi la kuwapo chuoni hususani kuzingatia masomo, maadili na kutojiingiza katika makundi hatarishi. Tukio la namna hiyo linaweza kukatisha ndoto za wanafunzi na kutokuwa na tija na msaada kwa familia zao, jamii, na taifa kwa ujumla," amesema.

Advertisement

Tukio hilo lilitokea Jumatatu Juni 20, 2022 katika mtaa wa Silivini kata ya Luchelele jijini Mwanza baada ya mwanafunzi huyo kijifungua na kutupa kichanga chake  nyuma ya nyumba anayoishi na kusababisha kifo chake huku akiishia mikononi mwa wananchi wenye hasira kali muda mfupi baada ya kutekeleza kitendo hicho.

Baadhi ya wakazi wa mtaa huo wakikitaka chuo hicho kuchukua hatua dhidi ya wanafunzi wanaopata na kutoa mimba ili kukomesha vitendo hivyo.

Mkazi wa Mtaa wa Silivini eneo la Sweya, Wambura Mwita alisema ili kukomesha vitendo hivyo kwa wanafunzi, serikali na uongozi wa chuo unatakiwa kuchukua hatua za kisheria kwa watu wanaobainika kufanya hivyo.

Advertisement