Semakafu awaonya wanaobeza elimu ya Tanzania
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Avemaria Semakafu
Muktasari:
- Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dk Avemaria Semakafu amewataka Watanzania kuacha tabia ya kujidhalilisha na kujirudisha nyuma kwa kuzungumzia vibaya shule za Serikali pamoja na walimu.
Dodoma. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Avemaria Semakafu amewataka wanaoithamini elimu ya nchi jirani na kuibeza ya Tanzania kuwa haifai kuachana na tabia hiyo.
Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Mei 4 jijini Dodoma katika hafla ya kuwatunuku vyeti washindi wa kitaifa wa shindano la uandishi wa insha za Jumuiya ya Maendeleo za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema wapo Watanzania wanaoibeza elimu inayotolewa Tanzania wakisema ya mataifa jirani ni bora zaidi akiwataka kuacha kujidhalilisha.
“Hawa watoto walioshinda wamesoma hapa Tanzania na wameenda kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo na wamewashinda wao ambao ndio wanaonekana elimu yao ipo bora kuliko Tanzania,” amesema Dk Semakafu.
Amesema tukio la kuwatunuku washindi hao linatuma ujumbe kwa wale wote ambao kila uchwao wanaisema vibaya elimu ya Tanzania, akisema kipimo cha utu ni wewe mwenyewe.
Hata hivyo, amewata washindi hao pamoja na wanafunzi wengine kutokata tamaa kushiriki katika mashindano mengine ya kimataifa yatakayotokea kwani yanawajenga kuwa viongozi wa baadaye katika nafasi hizo.
Naye mratibu wa mashindano ya uandishi wa insha za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sylvia Chinguwile ametoa wito kwa wazazi pamoja na walimu kuzidi kuwahimiza wanafunzi wao kushiriki mashindano hayo na mengine, akisema kwa uzoefu wake inaonyesha washindi wa mashindano hayo wamekuwa wakifanya vizuri hata kwenye mitihani yao ya mwisho.
Amewapongeza walimu wa wanafunzi walioshiriki kwa usimamizi uliowawezesha kufikia hatma ya kupata ushindi katika mashindano hayo.
Akitoa ushauri juu ya waandaaji wa mashindano hayo, mmoja wa wanafunzi walioshiriki mashindano, Inocce Shirima wa shule ya Moshi sekondari amewaomba kuweka lugha ya kiswahili kuwa miongoni mwa lugha zinazotumika katika shindao la SADC ili kukuza lugha hiyo katika mataifa mengine.