Prime
Serikali ilivyojibu hoja za bajeti, yatetea ushuru wa pikipiki
Muktasari:
- Serikali iliwasilisha mapendekezo ya bajeti yake Juni 11, 2026 ikilenga zaidi kuifanya Tanzania yenye uchumi wa kujitegemea.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imejibu hoja zilizoibuliwa na wabunge na Kamati ya Bunge kuhusu bajeti yake ya mwaka wa fedha 2026/27, ikiweka msisitizo kuhusu ushuru wa bidhaa kwa pikipiki zinazoingia nchini na kudokeza hatua za kubana matumizi.
Bajeti hiyo ya Sh62.3 trilioni iliyowasilishwa Juni 11, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ilisisitiza safari ya Tanzania kujitegemea kiuchumi, huku ikikazia mabadiliko ya matumizi ya nishati kutoka mafuta hadi umeme na gesi.
Wabunge walijadili kwa siku saba za kazi kuanzia Juni 15. Baadhi yao walipinga mapendekezo hasa ya ushuru wa bidhaa kwenye pikipiki, wengine wakataka mipango zaidi ya Serikali kubana matumizi na wapo waliotaka malipo ya madeni ya makandarasi.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti nayo iliwasilisha mapendekezo yake, ikionyesha mikakati iliyoelezwa na Serikali katika bajeti hiyo kuhusu kubana matumizi ni ileile ambayo imekuwa ikiieleza na baadhi haitekelezeki.
Majibu ya Serikali kuhusu hoja hizo za kamati na wabunge yametolewa bungeni jijini Dodoma leo, Jumanne Juni 23, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Omar, alipohitimisha na Bunge kuipitisha bajeti hiyo kwa kura 385 sawa na asilimia 97 ya kura zote 393 zilizopigwa. Nane zimeikataa.
Kubana matumizi
Baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo, Juni 15, 2026 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilisema imebaini hatua za kubana matumizi zilizowasilishwa ni zilezile ambazo Serikali imekuwa ikizitaja miaka yote na baadhi hazitekelezeki.
“Baadhi ya hatua hizo hazilengi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, baadhi ya maofisa masuuli kutekeleza vema Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma na maandalizi hafifu ya miradi ya maendeleo yanayosababisha gharama za miradi kutoendana na thamani ya fedha,” alisema.
Katika majibu yake kuhusu hilo, Balozi Omar amesema Serikali inakubaliana na maoni ya kamati hiyo na wabunge kuhusu kubana matumizi yake kwa kuwa yanaendana na mapendekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kudhibiti matumizi, lakini bado tunakiri ipo fursa kubwa ya kuongeza udhibiti zaidi na kuimarisha usimamizi wetu,” amesema.
Amesema udhibiti wa matumizi ni sehemu muhimu ya nidhamu ya fedha na Serikali inaendelea kutekeleza miongozo ya usimamizi wa matumizi ya umma, ununuzi wa umma na kuimarisha mifumo ya Tehama ili kuongeza ufanisi katika utendaji.
“Kudhibiti matumizi kupitia safari za nje na ndani, kupunguza semina, warsha na makongamano yasiyo na tija. Tunaahidi kupitia tena bajeti ya Serikali na kuhakiki maeneo yote ili kujiridhisha kama kuna fedha tunazoweza kuziokoa zikatumike katika maeneo mengine,” amesema.
Madeni ya makandarasi, wazabuni
Kuhusu hoja iliyowasilishwa na baadhi ya wabunge ya kuitaka Serikali kulipa madeni ya makandarasi na wazabuni, Waziri huyo amekiri kupokea hoja hizo akisisitiza Serikali haipendi kubaki na deni na imekuwa ikichukua hatua kwa kadiri hali inavyoruhusu.
Kwa madeni ya makandarasi na wazabuni, amesema tayari uhakiki umeshafanyika wa madeni ya Sh2.2 trilioni, yakiwemo ya wazabuni wa mbegu, mbolea na Bohari ya Dawa (MSD).
Kwa mwaka wa fedha 2025/26, amesema Serikali ilitenga Sh700 bilioni kwa ajili ya kulipa madeni ya wazabuni na makandarasi na kwamba kiasi hicho ni kidogo na wanapaswa kuongeza kasi ya ulipaji.
Katika bajeti ya mwaka 2026/27, amesema Serikali imetenga Sh1.2 trilioni kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya wakandarasi, wazabuni na watoa huduma na kwa wastani kila mwezi italipa Sh100 bilioni.
“Azma yetu ni kuwalipa kwa wakati wakandarasi na wazabuni wote na kuwawezesha kuendelea kutekeleza miradi na kuchochea shughuli za kiuchumi. Serikali inaangalia uwezekano wa kutafuta vyanzo mbadala vya kifedha kwa ajili ya kugharamia madeni ya wakandarasi,” amesema.
Amesema Serikali inatarajia kuanza kutekeleza uamuzi wa kupeleka moja kwa moja fedha za mifuko yenye vyanzo maalumu kwenye akaunti za mifuko hiyo ili kuimarisha usimamizi wa miradi, ikiwemo kulipa madeni ya wakandarasi.
Kwa upande wa deni la Bohari ya Dawa (MSD), amesema kwa mwaka 2023 hadi 2026, Serikali imetoa Sh945.04 bilioni kwa bohari hiyo kwa ajili ya gharama za ununuzi na usambazaji wa dawa.
Mwaka 2023, amesema bajeti ilikuwa Sh200 bilioni na ikatolewa Sh236.67 bilioni. Mwaka 2024/25 bajeti ilikuwa Sh200 bilioni na zilitolewa Sh391.98 bilioni, na mwaka 2025/26 zilitengwa Sh419.2 bilioni ambapo tayari Sh316.39 bilioni zimetolewa.
Amesema Serikali inakiri kudaiwa deni linalotokana na fedha za usambazaji wa dawa chini ya Mradi wa Msonge, uliotokana na fedha za msaada kutoka kwa wahisani.
Deni hilo, amesema hadi Juni 2025 lilifikia Sh220 bilioni baada ya kulipa Sh150 bilioni.
Amesema awali Serikali haikuwa inatenga fedha kwa ajili ya usambazaji wa dawa na ndiyo sababu ya kuzaliwa kwa malimbikizo hayo.
“Lakini kwa mwaka wa fedha 2026/27 Serikali imetenga Sh439.8 bilioni, kati ya hizo Sh148.2 bilioni kwa ajili ya mchango wa kugharamia usambazaji wa dawa.”
Maboresho ya PPP
Eneo lingine lililojengewa hoja na wabunge na Kamati ya Bajeti ni kuimarishwa kwa mfumo wa ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP), ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo bila kuigharimu Serikali.
Kuhusu hilo, Balozi Omar amesema Serikali inatambua tangu kutungwa kwa Sheria ya PPP bado Tanzania haijaonekana kunufaika na miradi hiyo ingawa hadi sasa ipo tisa inayotekelezwa.
Amesema mwaka ujao wa fedha utakapoanza, Serikali itapitia upya mfumo wa PPP na kama kutakuwa na mapendekezo watayachukulia hatua.
Kurasimisha sekta isiyo rasmi
Katika michango ya wabunge kuhusu bajeti hiyo, walisisitiza umuhimu wa kurasimishwa kwa sekta isiyo rasmi ili kupanua wigo wa kodi, badala ya kuvilimbikizia mzigo wa kodi vyanzo vichache vilivyopo.
Katika ufafanuzi wake, Waziri huyo amesema Serikali itachukua hatua ya kutoa msamaha wa kodi ya mapato kwa wafanyabiashara wapya kwa mwaka mmoja.
Pia, amesema itatenga asilimia tano ya mapato ya halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa masoko na maeneo mengine ya biashara.
Kuhusu kila Mtanzania bila kujali anafanya biashara au la kuwa na ulazima wa kuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi, amesema kuna namba za aina tofauti.
“Pale ambapo Mtanzania anaanza biashara anapaswa kubadili namba yake kutoka kuwa binafsi na kuwa ya biashara,” amesema.
Mikataba ya madini
Kamati ya Bajeti, katika uchambuzi wake ilisema pendekezo la Serikali kubadili Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Sura ya 147, Sheria ya Kodi ya Mapato Sura ya 332, Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta Sura ya 220 na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura ya 148 ni hatari.
Ilisema pendekezo hilo litairudisha nchi kupata hasara katika mikataba ya madini itakayokuwa inaingia kama ilivyowahi kutokea awali.
Akijibu hilo, Balozi Omar amesema Serikali inaendelea kuyafanyia kazi kwa kujadiliana na kamati hiyo na sasa wamefikia mahali pazuri pa kulitatua.
Ushuru kwenye bodaboda
Miongoni mwa maeneo yaliyoibua mjadala zaidi bungeni ni pendekezo la kutozwa asilimia tano ya ushuru wa bidhaa kwa pikipiki zinazoingia nchini.
Baadhi ya wabunge, akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini, Revocatus Chipando maarufu Baba Levo, alisema pikipiki zimeajiri vijana wengi na ndizo zilizotumika wakati wa kampeni za uchaguzi, hivyo vyombo hivyo vikitozwa ushuru itawapa ugumu vijana.
Kuhusu hilo, Waziri huyo amesema ushuru huo haukupendekezwa kutozwa kwenye kila pikipiki inayoingia nchini bali zile zinazotumia mafuta.
Amesema hoja hiyo ililenga kuendana na mpango wa Serikali kuongeza kasi ya matumizi ya vyombo vya moto vinavyotumia nishati safi yaani umeme na gesi.
“Kwenye hili litasaidia zaidi watumiaji wa pikipiki. Vyombo vya moto vinavyotumia nishati ya gesi na umeme vina gharama nafuu katika uendeshaji wake.
“Hili awali linaweza kuonekana kama changamoto lakini litawasaidia wamiliki wa pikipiki kupata faida kubwa zaidi,” amesema.
Eneo lingine ambalo Balozi Omar amelifafanua ni pendekezo la kuongeza ada ya uhakiki wa mafuta kutoka asilimia 0.5 hadi asilimia moja. Amesema linajadiliwa na Kamati ya Bajeti kwa ajili ya hatua zaidi.
Ameeleza kuna mambo watakayokuja nayo kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha kuhakikisha mambo yanaendana na hali inavyokuwa.
Katika mjadala wa kuimarisha mapato, amesema wabunge walitoa maoni kuhusu mzabuni mwenye mkataba na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa kusambaza stempu za kielektroniki za kodi. Wapo waliopendekeza aendelee na wengine wakataka aondolewe.
Balozi Omar amejibu, “Tutatangaza upya mkataba na kampuni iliyopo sasa na nyingine zozote zinazoona zitaweza kutimiza vigezo vitakavyowekwa ziombe, utafanyika uchambuzi na atakayeonekana ana vigezo atashinda.”
Kuhusu pendekezo la kutoza asilimia sifuri kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani, amesema hilo liliwekwa maalumu kwa ajili ya kuchochea usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.
Amesema kwa bidhaa zinazotumika ndani ya nchi hakukuwa na utaratibu wa kuwekwa VAT na utaratibu huo ulitumika katika bidhaa za mafuta hasa ya alizeti na nguo za pamba.
Pendekezo la Serikali kutoza ushuru wa asilimia 15 katika mafuta ya mchikichi yaliyochakatwa kwa kiwango cha kati, amesema viwango vya ushuru wa forodha ni vile vilivyokubaliwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kuhusu deni la Taifa
Wakati wa uchangiaji wa bajeti hiyo, baadhi ya wabunge walionyesha hofu ya kukua kwa deni la Taifa.
Balozi Omar amesema Serikali inatumia utaratibu wa matumizi ya mikopo katika kutekeleza bajeti kwa tahadhari na tathmini inaendelea kufanyika ya uhimilivu wa deni na watakopa kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo.
Amesema zaidi ya asilimia 40 ya deni ambalo Serikali inalipa linatokana na mikopo iliyoelekezwa kwenye sekta za maji, nishati na reli.
“Tunapobaki na asilimia 25 kwenye mfuko mkuu inakwenda kusaidia ulipaji wa deni katika maeneo yaleyale ambayo Serikali ilikuwa inakopa,” amesema.
Kuhusu mashirika ya umma yenye sura ya kibiashara kutafuta fedha kwenye masoko ya mitaji, amesema Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada inaruhusu mashirika kukopa endapo yatapata idhini ya Waziri wa Fedha.
“Utaratibu upo, waombe na waziri atakapoona kuna haja na kwa maslahi ya Taifa ataruhusu wakope,” amesema Balozi Omar.
Akijibu hoja ya kupitiwa upya kwa utaratibu wa kutoza kodi kwenye michango ya asilimia 15 inayotolewa kwa mashirika yaliyo chini ya Msajili wa Hazina, amesema wameangalia mapendekezo ya mwaka huu na watayafanyia kazi bila kuathiri mashirika au kuacha mengine yapate mapato makubwa bila kutoa mchango.
Aidha, Balozi Omar amesisitiza Serikali itahakikisha maoni yote yaliyotolewa na Kamati ya Bajeti na wabunge inayachukua na kuyafanyia kazi.