Serikali ilivyojizatiti kusambaza nishati safi
Muktasari:
- Serikali imedhamiria kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, Watanzania wasiopungua asilimia 84 wanatumia nishati safi ya kupikia
Dar es Salaam. Serikali imedhamiria kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, Watanzania wasiopungua asilimia 84 wanatumia nishati safi ya kupikia ili kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, hatua inayolenga kulinda afya za wananchi na mazingira.
Mkurugenzi Mkuu wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, amesema mkakati huo unahusisha pia kupunguza kodi kwenye bidhaa za nishati safi, ili gharama za mitungi ya gesi zipungue na kila mwananchi aweze kumudu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa kampeni ya Gesi Yente iliyoandaliwa na Oryx Gas, Mlay alisema matumizi ya kuni na mkaa yamesababisha ukataji miti kwa kasi na kuathiri afya za wananchi.
“Watu wengi wanatumia kuni na mkaa kwa kupikia. Hii inaleta madhara makubwa kiafya na kimazingira. Serikali kwa kushirikiana na wadau kama Oryx Gas tumeweka mkakati wa kuhakikisha ifikapo 2034, asilimia 84 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia,” alisema.
Mlay aliongeza kuwa tayari rasimu ya mapendekezo ya kupunguza kodi kwenye bidhaa hizo imeshawasilishwa ili bei ishuke. “Tukipunguza kodi, mitungi na gesi vitakuwa kwa bei nafuu na kila mmoja ataweza kumudu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania, Araman Benoit, alisema bado maelfu ya familia nchini hutegemea kuni, mkaa na mafuta ya taa, hali inayoongeza hatari ya magonjwa ya njia ya hewa na kuharibu mazingira.
Kupitia kampeni ya Gesi Yente, Benoit alisema kampuni hiyo itakusanya mitungi ya gesi isiyotumika majumbani na kuirudisha sokoni kwa matumizi, sambamba na kutoa zawadi kama pikipiki, baiskeli, seti za sufuria na mabegi ya shule kwa washiriki.
“Huu ni wakati wa kuamka kama taifa na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kupeleka nchi viwango vipya kwenye matumizi ya nishati safi,” alisema.
Alisisitiza kuwa Watanzania wanaomiliki mitungi ya gesi nyumbani bila kuitumia wairejeshe sokoni ili iweze kusaidia familia nyingine na washiriki wajipatie zawadi.
“Nishati safi ni salama, nafuu na rafiki kwa mazingira. Tunaweza kuijenga Tanzania yenye afya bora na mazingira yaliyohifadhiwa,” alisema Benoit.