Serikali inavyokabili upatikanaji gesi kwenye magari

Muktasari:

  • Serikali imeeleza mipango ya kuongeza vituo vya gesi iyo jijini Dar es Salaam pamoja na mikoani.

Dar/Mikoani. Unaweza kusema hatua hii itapunguza kiu ya wengi, baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Petroli Tanzania (TPDC),   Mussa Makame kueleza uwepo wa vituo vya gesi ya kwenye magari (CNG) vitano vinavyohama vitakavyosambazwa kwenye baadhi ya mikoa kwa lengo la kupunguza changamoto ya upatikanaji wa nishati hiyo nchini.

Amesema hadi kufikia Agosti, mwaka huu  vituo hivyo vitakuwa vimewasili nchini na vitasambazwa katika mikoa kadhaa, japo hakuweka wazi ni mikoa ipi.

Kwa sasa, mkoa wa Dar es Salaam pekee ndiyo kuna vituo rasmi vitatu --- Ubungo, Tazara na kilichopo Uwanja wa Ndege. Kituo cha Ubungo kilichojengwa mwaka 2011 kinatajwa kuelemewa na foleni ya magari  yanayofuata huduma hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi wa Pan African, hivi sasa kituo cha Ubungo pekee kinahudumia magari 700 mpaka 800 yanayojaza gesi kwa siku.

TPDC imebainisha kuwa kwenye mchakato wa kujengwa kwa vituo vingine viwili katika eneo la Mlimani City na la Chuo cha Posta, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Mwananchi Digital imeshuhudia, baadhi ya madereva wakisubiri kwa saa moja hadi mbili kwenye foleni, ili kupata huduma hiyo ambayo ni Sh1,550 kwa kilo moja, ambayo ni nusu ya bei ya lita moja ya petroli au dizeli.

Leo, Machi 15, 2024 wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanya ukaguzi wa miradi ya usambazaji wa gesi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TPDC, Mussa Makame amesema shirika hilo liko kwenye mchakato wa kununua vituo vitano vinavyohama, ili kusaidia kusambaza huduma hiyo mikoani.

"Hadi kufikia Agosti, vituo hivi vitakuwa vimewasili nchini," amesema Makame na kufafanua mbali na vituo hivyo vya kuhama, pia wameanza mchakato wa kujenga vituo vingine viwili Dar es Salaam eneo la Mlimani City na kingine jirani na eneo la Viwanja vya Posta, Kijitonyama.

“Vitakapokamilika, Dar es Salaam itakuwa na vituo vitano vya kujaza gesi," amesema na kuongeza kwamba kituo cha Mlimani City kinajengwa na TPDC na kile cha Viwanja vya Posta kitajengwa na kampuni ya Taqa Dalbit ambayo ndio inamiliki kituo cha gesi cha Uwanja wa Ndege.

Kwa mujibu wa Makame, mbali na vituo hivyo, vingine vinatarajiwa kujengwa Mwenge, Mbezi na Tegeta, ambavyo vikikamilika vitapunguza msongamano kwenye upatikanaji wa nishati hiyo jijini Dar es Salaam.

Mmoja wa watumiaji wa mfumo wa gesi kwenye gari, Edward Alex amesema kuna changamoto hasa ya kusubiri kwenye foleni kwa muda mrefu kupata huduma hiyo tangu alipoanza kuitumia mwanzoni mwa mwaka jana.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali imeweka mkakati wa kuwaondolea wananchi usumbufu kwa kujenga vituo vingine 15, jijini Dar es Salaam.

"Serikali inashirikiana na sekta binafsi kuongeza vituo, matumizi ya nishati ya gesi kwenye magari yanaongezeka kila siku," amesema.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, David Mathayo ameshauri Serikali na sekta binafsi kuongeza vituo na karakana za kuweka mifumo ya gesi kwenye magari, ili kutumia gesi asilia inayopatikana nchini.

Amesema nchi ikijikita kwenye matumizi ya gesi haitatumia fedha za kigeni kuagiza mahitaji ya nishati za petroli na dizeli, huku akiishauri Serikali kuondoa kodi kwenye vifaa vinavyotumika katika kufunga mfumo huo kwenye magari, ili gharama za kuunganishiwa ziwe rafiki.

"Sasa hivi kuweka mfumo wa gesi kwenye gari moja ni Sh1.8 milioni hadi Sh2 milioni, vifaa hivyo vikipunguzwa bei ni dhahiri watu wengi watakuwa na uwezo wa kufunga mfumo huo,” amesema.

Aidha, ameshauri, Serikali na waagizaji binafsi wa magari kuagiza yenye mifumo ya gesi ili kuepuka gharama kubwa za kuweka mifumo hiyo hapa nchini.

"Moja ya matumizi makubwa kwenye magari ya Serikali ni mafuta, Serikali ifikirie kuagiza magari ambayo tayari yamefungiwa mfumo huu ili kupunguza matumizi,"

Kilwa

Katika mji wa Kilwa, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imetembelea miradi ya kufungua utalii wa Malikale kwenye magofu ya Kilwa Kisiwani ikiwa ni juhudi mpya za kuongeza zao jipya la utalii huo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Timotheo Mnzava ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) kwa kusimamia utekelezaji wa miradi  kwa umahiri na faida imeonekana.

“Kutokana na uboreshaji wa miradi hiyo tumeona idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii 2,000 kwa mwaka 2018/2019 hadi kufikia watalii 6,000 kwa mwaka 2022/2023 na mapato kuongezeka” amesema akiioongoza kamati hiyo kufanya ziara kwenye Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara yanayosimamiwa na TAWA.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki  ameema maeneo ya  Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ni moja ya maeneo saba yaliyotangazwa  na kuorodheshwa kuwa moja ya maeneo ya urithi wa dunia chini ya Mkataba wa Kimataifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Amesema Serikali itaendelea kuibua mazao mapya ya utalii, ili kupanua wigo wa utalii akitolea mfano hivi karibuni ambapo Wizara ya Maliasili na Utalii imegundua mapango 130 katika ukanda wa Pwani na matatu yapo katika wilaya ya Kilwa.

Imeandikwa na Victor Tullo, Florah Temba na Imani Makongoro