Serikali kuacha kupeleka wagonjwa nje ya nchi kutibiwa

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla akizungumza kwenye wodi mpya ya ICU iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Rais wa Gastroenterology kutoka Ujerumani, Profesa Meinhard Classen na katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa MNH, Profesa Lawrence Mseru. Picha na Salim Shao

Muktasari:

Hospitali ya Muhimbili ina vitanda 25 vya ICU kati ya vitanda 150 vinavyohitajika

Dar es Salaam. Serikali imesema ina mpango wa kusitisha kupeleka wagonjwa nje ya nchi kupatiwa matibabu na kuhakikisha kila kitengo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kinakuwa na chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).

Serikali imechukua uamuzi huo, wakati taarifa ndani ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wazee na Watoto zikieleza inadaiwa deni la Sh.28.74 bilioni za malimbikizo kutokana na ongezeko la wagonjwa wanaopelekwa nje kwa matibabu.

Akizungumza wakati wa kuzindua chumba cha ICU kilichopo jengo la Mwaisela hospitalini hapo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk Hamis Kigwangalla alisema lengo la Serikali ni kuanzisha vyumba hivyo kwa kila kitengo ili kupunguza vifo.

Alisema hospitali hiyo ina vitanda 25 vya ICU, lakini lengo ni kuwa na vitanda 150 vya wagonjwa mahututi na wataalamu wa kutosha.

Alisema Serikali ina mpango wa kutoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi watakaokuwa wamebobea katika fani ya vyumba hivyo.

Madaktari na wauguzi hao watapata mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Cairo na mengine yatatolewa kupitia Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas).

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Mseru alisema kuzinduliwa kwa ICU hiyo kunaifanya hospitali hiyo kuwa na vyumba vya aina hiyo viwili vyenye vitanda 25, kutoka chumba cha awali kilichokuwa na vitanda vinane.

Alisema uwapo wa vitanda hivyo ni ongezeko la asilimia 200 ikilinganishwa na uwezo wa awali.

“Fedha za ndani zilizotumika kwa ajili ya ukarabati wa chumba hiki ni Sh230 milioni ikiwa ni pamoja na kutafuta ufadhili kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Ujerumani iliyowekeza vifaatiba vya Sh600 milioni.

‘‘Mfadhili huyu ndiye aliyetununulia vifaa vyenye thamani ya Dola 800,000 za Marekani,” alisema Profesa Mseru.