Serikali kuajiri watumishi wa afya 400

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Ligula, Dkt Lobikieki Kissambu alipokuwa akitoa maelezo kuhusu hospitali hiyo leo Ijumaa Julai 7, 2023.

Mtwara. Katika kukabiliana na upungufu wa wahudumu wa afya Serikali inatarajia kuajiri watumishi wapya 400 katika mwaka huu mpya wa fedha wa 2023/2024.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema leo Ijumaa Julai 7, 2023 wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika hospita ya Kanda ya Kusini ya Mitengo iliyopo mkoani hapa.

Dk Mollel amesema tayari amepata kibali cha kuajiri watumishi wapya 400 ambao watasambazwa kuanzia ngazi ya mkoa hadi Taifa.

Naibu Waziri alitoa ufafanuzi huo baada ya kuelezwa kuwa kuna upungufu wa madaktari katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini ya Mitengo.

Awali, Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa, Dk Lobikiek Kissambu amesema hospitali hiyo ina madaktari bingwa watano huku mahitaji ni madaktari 15.

Akizungumza katika ziara yake hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali inafahamu kuwa kuna msongamano mkubwa wa wagonjwa katika hospitali mbali mbali na watumishi wa afya ni wachache lakini inafanya jitihada kuziba mianya.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa ametembelea hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Ligula na ya Kanda ya Kusini ya Mitengo.